Benki ya NMB imezindua kampeni mpya ya Jihudumie yenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa haraka wa huduma mbalimbali za benki hiyo. Akizindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bw. Mark Wiessing alisema mbali ya upatikanaji wa huduma haraka, kampeni hiyo itawezesha huduma kupatikana muda wowote na mahali popote.
Sasa wateja wa NMB wanaweza kupata huduma bila kwenda katika tawi la NMB. “Tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kwamba sasa wanaweza kupata huduma za kibenki kupitia simu za mkononi na njia nyingine mbadala kama mashine za ATM, huduma za benki kwa njia ya intaneti, PesaFasta na Akaunti ya Chap Chap,” alisema Wiessing.
Kupitia kampeni hiyo, NMB imeweza kuzingatia mahitaji ya msingi ya wateja wake, ikiwemo uhakika wa huduma za kibenki na uwezo wa kuzipata wakati wowote na mahala popote.
“Kwa kubonyeza tu kitufe cha simu, fedha itaweza kutoka kwenye akaunti yako ya NMB kwenda mahala pengine popote kama vile kwenye malipo ya LUKU, kulipia muda wa maongezi wa simu na hata kuweza kutoa kiasi kinachofikia shilingi milioni moja kupitia mashine za ATM,” alisema.
Baada ya uzinduzi huo mwendelezo ulifanywa kwa matawi yote ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, wateja wa benki hiyo walisifia kampeni hiyo, wakisema imelenga kuwapunguzia adha, usumbufu na kuokoa muda wa kupata huduma za kibenki.