Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato TRA, Loicy Appollo anayedaiwa kupokea Tshs. Mil 80.8/- katika sakata la ESCROW jana amegoma kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa madai ya kuwepo kwa zuio la Mahakama Kuu ambapo anafanya idadi ya waliogoma kufikia watatu.
Wengine waliotangulia kugoma kuhojiwa na Baraza hilo ni Mbunge Andrew Chenge na Afisa Mtendaji wa RITA, Philipo Saliboko.
Appollo analalamikiwa kwa kupokea mgawo huo wa fedha kutoka kwa Rugemalila ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering ambayo ina mahusiano na TRA kama mlipakodi.
NIPASHE
Mafuta feki ya kula aina ya Oki na Premier Gold madumu 300 yenye ujazo wa lita 20 ambayo yalikamatwa Bandari bubu Bagamoyo yanatarajiwa kurudishwa Malaysia chini ya uongozi wa Shirika la Viwango TBS.
TBS iliyazuia mafuta hayo kungia sokoni mpaka yakapokaguliwa katika maabara ambapo chanzo cha gazeti la NIPASHE kimesema mafuta hayo yalikutwa hayana ubora na mwagizaji wa mafuta hayo alipewa taarifa kuyarudisha yalikotoka chini ya usimamizi wa TBS.
Chanzo hicho kimesema mzalishaji aliyepewa kibali kuzalisha mafuta hayo nchoni anayatengeneza kwa kiwangokinachotakiwa lakini haya yaliyoingizwa kwa njia ya panya hayakuwa na kiwango kinachotakiwa ikiwemo kutokuwa na tarehe ya kutengezwa na mwisho wa matumizi.
TANZANIA DAIMA
Jeshi la Polisi Morogoro linamshikilia Josephat Asenga kwa kujifanya padre wa Kanisa Katoliki Jimbo la New York Marekani ambaye alifikia parokiani hapo Mei mwaka jana na kujitambulisha kwa viongozi wa kanisa la Modeko kuwa amekuja kwa ajili ya mapumziko na kuomba kuendesha ibada kanisani hapo.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 5 katika Kanisa Katoliki la Modeko Jimbo la Morogoro akiwa na majoho saba ya upadri.
Padri huyo alionesha kitambulisho kilichofanya wampe ruhusa kuendesha misa bila matatizo, baada ya kumaliza misa walianza kumtilia shaka na kuanza kumfuatilia na kupata taarifa kwamba alikuwa akiishi na mwanamke kinyume na sheria za kipadri za kanisa hilo.
Baada ya kukamatwa alihojiwa na kukubali kwamba ni kweli yeye sio padri, Polisi wanaendelea na uchunguzi japo tayari taarifa za kutoka Makao Makuu ya Kanisa hilo wamethibitisha kwamba Asenga sio padri wa Kanisa hilo.
TANZANIA DAIMA
Vijana waliohitimu Mafunzo ya JKT wamemwomba Mkurugenzi wa Mashtaka DPP katika Mahakama ya Kisutu awaondolee masharti ya dhamana ili waweze kutibiwa kwa kuwa baadhi yao ni wagonjwa na wanakosa matibabu.
Maombi yao yaliwasilishwa jana baada ya wakili wa Serikali kudai kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo aliomba tarehe ya kuahirishwa ambapo Hakimu Moshi alisema mshtakiwa ambaye ni mgonjwa anapaswa kumwandikia barua DPP ama wenzake kuandika kwa niaba yake lakini pingamizi la dhamana lililowekwa na DPP Mahakama haina mamlaka ya kutengua.
Mshtakiwa mwingine Jacob Mang’ita amesema yeye sio miongoni mwa watuhumiwa ila alikamatwa alipokwenda kumjulia hali mgonjwa wake katika Hospitali ya Muhimbili ambapo Hakimu Moshi alisema shauri hilo litatolewa wakati ambao itafikia hatua ya ushahidi.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amewataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuwajengea uwezo waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo kila mara, pamoja na kuboresha maslahi yao kwani wakishindwa kuwalipa vizuri, waandishi hao watalipwa na watu wa mtaani jambo ambalo linaweza kupunguza weledi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua rasmi kituo cha Televisheni cha Azam kinachomilikiwa na Kampuni ya Said Salim Bhakresa (SSB) huku akimmwagia sifa Mwanyekiti wa Kampuni hiyo Said Salim Bakresa kwa kueleza kuwa uwekezaji alioufanya utaongeza ushindani katika sekta ya habari na kukitaka chombo hicho kuweka mbele maslahi ya utaifa kama wanavyofanya mashirika makubwa ya habari duniani kama vile BBC na CNN nao wanazingatia utaifa wao kwanza.
“Tanzania ni moja ya nchi zilizofanya vizuri katika kuhama kutoka kwenye mfumo wa habari wa analogia kwenda digiti kwa ubora wa hali ya juu hivyo kuzinduliwa kwa Studio za Azam TV kutaendeleza kuongeza ufanisi wa ubora wake,”Amesema Rais Kikwete.
Amesema sekta ya habari ni moja ya mhimili mkubwa hapa nchini ambao kazi yake ni kuhakikisha kuwa suala la Demokrasia linaendelea kukua na kuthaminiwa, hivyo Serikali itaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari kwa kutunga sheria zisizo kandamizi.
“Siku zote penye bidii penye maarifa penye mipango ya uhakika hakuna kisichowezekana, hawa jamaa wameanzia mbali sana bidiii imewafanya wafikie mahali hapa walipo:- aliongeza, Tumezoe kula vitu vya Azam, kunywa vitu vya Azam, kushabikia timu ya Azam na sasa tutasikiliza Azam, hii ni kazi nzuri kwa taifa hili”– alipongeza Rais Kikwete“
MTANZANIA
Mpango wa ugawaji wa vyakula vya msaada na vifaa vingine kwa waathirika 250 wa mafuriko Kahama uligeuka shubiri baada ya Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Hamis Mgeja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Benson Mpesya kutaka kupigana mble ya Mkuu wa Mkoa, Ali Rufunga.
Mtafaruku huo ulizuka wakati viongozi hao walipoanza kushutumiana ambapo Mgeja alianza kumshambulia Mpesya akidai DC huyo ametoa kauli za kuwakejeli ambapo Mpesya akajibu kwamba hana kawaida ya kujibizana na Mwenyekiti wa Chama Mkoa.
Licha ya Taasisi kadhaa kutoa misaada kwa waathirika hao wa mafuriko kumekuwa na malalamiko kwamba misaada hiyo ya vitu ikiwemo mablanketi na magodoro imekuwa ikiuzwa, alipoulizwa DC Mpesya amesema kuwa hana taarifa na suala hilo lakini kwa kuwa limemfikia basi atalifanyia kazi wakati wowote.
Ripoti ya Hospitali walikolazwa majeruhi wa maafa hayo inaonesha kuwa mpaka sasa idadi ya majeruhi waliobaki ni 37 kati ya 100 waliofikishwa kutibiwa.
MTANZANIA
Kitendo cha watu wenye ulemavu wa ngozi kupigana Ikulu kimezua gumzo sehemu mbalimbali ambapo tafrani hiyo ilitokana na mvutano wa kugombea nafasi ya wawakilishi 18 waliotakiwa kuonana na Rais Kikwete.
Ofisa Mawasiliano wa Chama cha Albino (TAS), Josephat Torner amesema kitendo cha wao kupigana Ikulu ni ishara ya uchungu dhidi ya wenzao wanaouawa kikatili.
Akizungumzia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho Torner alisema unatokana na masuala ya Kikatiba ambapo wanachama walitaka kufanyika uchaguzi mapema lakini Azimio la Mkutano Mkuu liliagiza uchaguzi huo kufanyika mwezi Julai.
Torner aliipongeza Serikali kwa kuchukuliwa hatua ya kunyongwa kwa watu waliohusika na mauaji ya albino.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook