Hatimaye mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema “ameshawishika” na kuweka bayana kuwa atachukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa makada wa CCM wanaowania urais, lakini hakuwahi kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Lakini jana, alilazimika kufunguka kuhusu suala la urais ambalo lilimfanya yeye na wenzake watano wafungiwe kwa kipindi cha miezi 12 kujihusisha na harakati hizo baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kuwa walianza kampeni mapema kabla ya muda kufika.
“Nimepata barua za ushawishi kutoka kwa watu wengi, lakini nyinyi nimeshawishika,” alisema Lowassa nyumbani kwake mjini Dodoma wakati alipokuwa anazungumza na masheikh wa misikiti ya Wilaya ya Bagamoyo wanaokadiriwa kuwa kama 50 hivi ambao pia walikuja mjini hapa kwa ajili ya kumshawishi aingie kwenye kinyang’anyiro cha urais na kumkabidhi mchango wa Sh700,000 za kuchukulia fomu.
“Lakini bado kuna taratibu za chama za kuheshimu. Nangojea pale watakaposema sasa tuwe, basi itakuwa.”
Lowassa alifungiwa na CCM Februari 18, 2014 pamoja na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Kilimo, Chakula na Ushirika), na January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine waliofungiwa ni Frederick Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu na William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema).
Pamoja na adhabu hiyo kumalizika Februari 18, CCM imesema Kamati ya Maadili inaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kujiridhisha kama miongoni mwao kuna waliokiuka adhabu hiyo kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati Kuu ambayo itafanya uamuzi.
Masheikh waliofika jana nyumbani kwake wanatoka maeneo ya Mlingotini, Kondo, Kaole, mjini Bagamoyo, Lugoba na Chalinze wilayani Bagamoyo.
Mbali na kumuomba atangaze nia, masheikh hao pia walimsomea dua ya kumtakia heri katika harakati hizo.
“Nyie ni special (maalum), mnatoka Bagamoyo na inajulikana kwa historia na ni nyumbani kwa Rais (Jakaya Kikwete). Namimi nimepata baraka zake na nyie mmemuwakilisha,”Lowassa.
“Tumetoka naye mbali sana, lakini Mwenyezi Mungu akinijalia nitaanzia pale alikomalizia. Amefanya kazi kubwa na ya heshima kwa kweli. Kwa hiyo kitendo cha kutoka nyumbani kwenu kuja kuniona kwa kweli kimenipa nguvu kwamba wenzangu wa Bagamoyo wako pamoja na mimi.”
MWANANCHI
Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.
Kuondoka kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo atalipwa mafao yake yote.
“Unajua Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando. Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,” Joel.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za vyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa familia na aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
“Alitufanya kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ijayo,”Ismail Aden Rage .
MWANANCHI
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira aliyepewa jukumu la kuandaa Ilani ya CCM kwa ushirikiano na timu ya watu 23 wa chama hicho itakayotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 hadi 2020, amejitokeza na kusema kazi hiyo ipo ukingoni kukamilika.
Kauli hiyo Wasira ameitoka siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwaeleza waandishi wa habari mjini Arusha kuwa Ilani hiyo inasimamiwa na Wasira na inatarajia kutoa Dira ya Mwelekeo ya chama hicho tawala katika kutatua matatizo ya wananchi.
Alisema Ilani hiyo itaangazia pia mambo ambayo yaliahidiwa ndani ya Ilani iliyopita na hayakutekelezwa ipasavyo. Baadhi ya mambo ambayo hayakufanikiwa ni tatizo la maji, migogoro ya ardhi na suala la ajira.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa njia ya simu, Wasira alisema: “Unajua labda ninyi mtakuwa mmechelewa kupata taarifa kuwa tumeanza lini, lakini sisi tulikwishaanza kazi hii na tuko hatua za mwisho za kutoa Rasimu ya Ilani yenyewe.”
Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alisema Ilani hiyo inaandaliwa kwa kuangalia changamoto gani zilizojitokeza kwa miaka 10 nyuma na ndiyo wanayoipa kipaumbele katika maandalizi hayo.
“Ukiangalia uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia saba kila mwaka lakini si kiwango kikubwa ukilinganisha na maisha ya wananchi yalivyo hivyo Ilani hii itatakiwa kuja na majibu ya tatizo hilo na kuhakikisha wananchi wetu wanakuwa na maisha bora,” Wasira.
“Suala la ajira ukiangalia wanafunzi wengi wanaanza shule za msingi na wanapomaliza wanaendelea sekondari na baada ya hapo wanakwenda vyuoni hivyo wahitimu wa vyuo vyetu wanaongezeka jambo hapa ni kuja na mkakati wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu.”
HABARILEO
Mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta kwa ajili ya kufua umeme nchini, imetajwa kuwa kikwazo katika maendeleo ya Taifa, kutokana na kutumia rasilimali fedha za kigeni nyingi katika kuzalisha nishati hiyo nchini, ambayo ingeweza kutumika katika maendeleo.
Taarifa za uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Benki Kuu (BoT), zimebainisha kuwa suluhisho pekee la tatizo hilo, ni kukamilika na kuanza kazi kwa bomba la gesi kutoka Madimba Mtwara, hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.
Trilioni 1.6 Taarifa ya TPDC kwa umma iliyotolewa mwishoni mwa wiki kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia kutoka Madimba, Mtwara hadi Kinyerezi Dar es Salaam, imeeleza kuwa ununuzi wa mafuta hayo ya kufua umeme umekuwa ukigharimu Taifa zaidi ya Sh trilioni 1.6 kila mwaka.
“Itakapokamilika miundombinu hiyo (ujenzi wa bomba la gesi), itaokoa zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja sawa na Sh trilioni 1.6 kwa mwaka, zinazotumika kwa sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya kufua umeme kwa kutumia mitambo ambayo tayari ipo nchini,” imeeleza taarifa hiyo.
Mitambo hiyo ni pamoja na mtambo wa IPTL uliopo Tegeta Dar es Salaam unaotumia mafuta mazito na mitambo ya Agreko na Symbion iliyopo Dar es Salaam, inayotumia gesi inayoagizwa kutoka nje.
Mwingine ni mtambo wa Symbion wa Dar es Salaam pia, ambao unatumia mafuta ya kurushia ndege na mitambo mingine miwili ya Symbion ya Dodoma na Arusha, ambayo inatumia gesi inayoagizwa kutoka nje.
Tanesco inavyonyonywa Taarifa kutoka Tanesco zimebainisha kuwa kitendo cha mitambo hiyo kutumia mafuta mazito, mafuta ya ndege na gesi kutoka nje ya nchi, badala ya gesi asilia kufua umeme, kimekuwa ‘kikitafuna’ shirika hilo, kwa kuwa wamiliki wa mitambo hiyo huuza umeme kwa shirika hilo kwa bei ya juu, kuliko bei ambayo Tanesco inalazimika kuuza kwa wananchi.
HABARILEO
Shamba la miwa inayokadiriwa kufikia tani 6,000 baada ya kuvunwa lenye ukubwa wa hekta 240, limechomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha hasara ya Sh milioni 280.2, mali ya wakulima wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, wakulima hao walisema kuwa vitendo hivyo vya jamii kuendelea kuchoma moto hovyo nyikani vimeanza kurejea.
Mmoja wa wakulima hao, Anas Swaibu alisema uchomaji moto hovyo umekuwa changamoto kuu inayorudisha nyuma maendeleo ya mkulima na kumsababishia kutotimiza malengo yake.
Alisema kuwa athari ya moto mashambani, imekuwa ikisababisha mkulima kulazimika kuvuna miwa yake kabla haijakomaa, huku uamuzi huo ukimuingiza hasara kwani malengo ya mavuno yake hushindwa kukamilika ipasavyo.
Kutokana na athari zinazoendelea kusababishwa na vitendo vya uchomaji moto hovyo, mkulima huyo ameuomba uongozi wa serikali ya wilaya kuangalia upya jinsi gani utawala utaweza kushirikisha jamii katika kutokomeza majanga hayo.
“Tunaomba Serikali ifanye utaratibu wa kukutanisha wadau wa maendeleo, wakulima na jamii kwa ujumla ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza kutokomeza vitendo hivi kwani kila siku mkulima anazidi kuumia jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yake,”alisisitiza.
Alisema kuwa kwa sasa bei inayotolewa na mnunuzi mkuu ambaye ni kiwanda cha Sukari cha Kagera kilichopo wilayani humo ambayo ni Sh 46,700 kwa tani moja, kiasi ambacho kiko chini na hakiendani na gharama za uzalishaji katika kilimo hicho.
Alisema shughuli za kilimo cha miwa zinachukua gharama nyingi ukilinganisha na bei inayotolewa kiwandani, japo angalau bei inapaswa kufikia kiasi cha Sh 55,000 kwa tani ili mkulima aweze kupata faida na kukidhi mahitaji yake ya msingi ukilingaisha na gharama za kilimo kupanda.
“Mitaji ya wakulima ni mikopo, hivyo tunalilia bei kwa mnunuzi tukiwa na maana ya kwamba tuweze kurudisha mikopo ya benki na sisi tunufaike na kilimo hiki, kuliko kushindwa kurudisha hata mikopo na kufilisiwa na waliotukopa,” alisema.
Hata hivyo, licha ya kutoridhika na bei hiyo inayotolewa na mnunuzi wa kiwanda hicho, mkulima huyo ametoa shukrani kwa uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera Sugar kwa kutoa msaada mkubwa kwa wakulima vinginevyo kama uongozi usingekuwa karibu na wakulima hao, hakuna ambaye angelikuwa anaendelea na shughuli za kilimo hadi sasa.
MTANZANIA
Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda amekimbilia nchini Marekani kuomba hifadhi ya kisiasa.
Chanzo cha kuaminika kutoka Marekani kilisema Banda ameshapewa hifadhi na Serikali ya Marekani ingawa inafanywa kwa siri.
Banda akiwa nchini humo amekuwa akishiriki hafla mbalimbali anazoalikwa na moja ya hafla aliyoalikwa ni ile ya utoaji tuzo ya kimataifa ya uongozi ya taasisi ya GB Group Global ya Marekani ya mwaka 2015 iliyofanyika katika jiji la Washington.
“Ni kweli Joyce Banda yupo nchini Marekani kwa muda mrefu sasa,na katika hafla hiyo alisema alipokuwa rais kwa muda mchache alijenga wodi za wazazi zilizowasaidia wanawake nchini Malawi kujifungua katika mahali salama” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine kilisema Juni mwaka jana baada ya Peter Mutharika kuapishwa kuwa rais mpya wa Malawi ndipo Banda alipokimbilia Marekani.
JAMBOLEO
CHADEMA imesema aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe angerithi mikoba ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe au Dk. Slaa kama angekuwa na nidhamu na kutokuwa msaliti.
Pia kimesema hakitamsahau Zitto kwa kwani alikuwa na mchango mkubwa ndani ya chama hicho.
Mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani Tundu Lissu alisema Zitto alikuwa na mazuri yake ndani ya chama hicho na ni miongoni mwa watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya viongozi wetu wa ngazi ya juu.
Pia Lissu alifafanua kuwa aliamua kutompa Ziito mkono wa kumuaga baada ya kutangaza uamuzi huo bungeni kwa kuwa kufanya hivyo kungemfanya aonekane mnafiki.
Amesema anasimamia anachokiamini kuhusu kasoro alizozifanya Zitto za kumfanya atimuliwe na aliamua kuondoka kwa kuwa alijua kinachofuata kwa kuwa alikiuka katiba ya chama inayokataza mambo ya chama kupelekwa mahakamani.
NIPASHE
Polisi Jijini Arusha wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananachi wenye hasira waliochoma nyumba na magari baada ya kijana wao anayetuhumiwa kufumaniwa akifanya mapenzi na mfanyakazi wa ndani kuuawa na anayedaiwa kuwa bosi wa mfanyakazi huyo.
Bosi huyo mkazi wa mtaa wa Olasiti Arusha pamoja na wenzake wawili wanatuhumiwa kumuua kijana huyo Melita Mokosio baada ya kumfumaini akifanya ngono na msichana huyo hatua iliyosababisha wakazi wenye hasira kuchoma nyumba yake na magari matatu ya waliohusika na mauaji hayo.
Watu walioshuhudia tukio hilo lililotokea majira ya saa3 asubuhi walimtaja anayedaiwa kumuua kijana huyo ambaye anajulikana kwa jina la baba Tony.
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Edward Balele aliyekuwa eneo la tukio alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na uharibifu wa mali lakini alisema jeshi lake linafanya uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kutoa taarifa rasmi.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook