NIPASHE
Askari Polisi na wa Magereza, wametiwa mbaroni mkoani Simiyu kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia ambazo kama halali zingekuwa na thamani ya Shilingi milioni moja.
Hali kadhalika, askari hao wanadaiwa kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Charles Mkumbo, alisema jana kuwa askari hao walikamatwa juzi saa 9:00 alasiri mtaa wa Old Maswa, kata ya Nyakabindi wilayani Bariadi.
Kamanda Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu H 2420 PC Seleman Juma (25) na askari namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28), wa Magereza wilayani Bariadi.
Alisema askari hao walifika katika kibanda cha kuweka na kutoa fedha cha M-Pesa kinachomilikiwa na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Old Maswa, Cassian Luhende, wakiwa katika pikipiki aina ya Sunlg kwa lengo la kuweka fedha hizo kwenye simu.
Alisema baada ya mwalimu huyo kupokea noti hizo ‘feki’ 10, alizitilia shaka na alipozikagua zaidi aligundua kuwa siyo halali.
Kamanda Mkumbo alisema Mwalimu Luhende baada ya kugundua kuwa fedha hizo ni bandia, aliwajulisha jirani zake kwa lengo la kuomba msaada wa kuwakamata askari hao.
Aidha, alisema baada ya mwalimu kutoa taarifa kwa jirani, wananchi walikusanyika na kuanza kuwahoji askari hao na ndipo mmoja alipotoa kitambulisho chake kikionyesha ni askari huku mwingine akijitambulisha ni dereva wa bodaboda.
Aliongeza kuwa wananchi baada ya kuambiwa hivyo waliwatilia shaka zaidi na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi na ndipo askari hao walipotiwa mbaroni.
Kamanda Mkumbo alisema baada ya askari hao kukamatwa, PC Selemani Juma, alipekuliwa katika mfuko wa suruali na kukutwa na noti nyingine bandia za elfu kumi-kumi ambazo kama halali, zingekuwa na thamani ya Sh. 1,920,000.
Alifafanua kuwa askari huyo alipopekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni kaptura nne, fulana mbili, sare za kivita (combat) jozi moja pamoja na kitambaa chake.
Kamanda Mkumbo alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa huo huku akielezea baada ya uchunguzi kukamilika askari hao watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
NIPASHE
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imejiondoa katika kesi ya kikatiba iliyoifungua Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga utekelezaji wa maazimio nane yaliyopitishwa na Bunge baada ya kushindwa kupinga mapingamizi yaliyowasilishwa na upande wa serikali.
Mbali na IPTL kampuni nyingine zilizohusika kupinga maazimio hayo ni Pan Africa Power Solution Ltd (PAP) mmiliki wa IPTL, Habinder Sethi , na mmiliki wa kamapuni VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira.
Mbele ya Jaji Stella Mugasha, wakili wa upande wa utetezi, Gabriel Munyele, akisaidiana na wakili Joseph Sungwa, aliiambia mahakama kuwa hakuna haja ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwani zuio la muda waliloomba lilikuwa limeshaanza kutekelezwa na Bunge.
Upande wa serikali ukiongozwa na naibu Mwanasheria Mkuu, Gabriel Malata, ulidai kuwa ulipwe gharama za kesi kutokana na usumbufu uliofanywa na IPTL kung’ang’ania kupinga maazimio ambayo yalikuwa yalishaanza kutekelezwa.
Malata alidai kuwa IPTL inatakiwa kulipa gharama za uendeshaji wa kesi zikiwamo uchapishaji wa majalada na muda waliotumia kuja mahakamani.
Aidha aliiomba Mahakama itumie vifungu vya sheria vinavyoelezea na masuala ya gharama za kesi kuiamuru IPTL kulipa gharama hizo.
Malata aliiomba mahakama itende haki ili kukomesha usumbufu unaofanywa na kampuni au watu wanaofungua kesi wakati wakijua hawawezi kushinda.
Jaji Mugasha aliitaka kampuni ya IPTL iwajibike kwa kulipa gharama za kesi kwa kushindwa kujiondoa mapema kupinga maazimio hayo, huku wakijua fika yalishaanza kutekelezwa.
Wakili Malata alisisitiza kuwa upande wa serikali utafuatilia ili kuhakikisha IPTL inalipa gharama za kesi kwa wakati mwafaka.
Desemba 31 mwaka jana serikali iliwasilisha mapingamizi matano katika mahakama hiyo kupinga maombi ya IPTL juu ya maazimio yaliyopitishwa na bunge.
Katika kesi hiyo namba 57 iliyosajiliwa mwaka jana IPTL ilifungua kesi ya maombi kupinga ya maazimio nane yaliyopitishwa na bunge yakiwamo.
Miongoni mwa maazimio hayo ni Bunge kuitaka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusika na kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetakiwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete, kusitisha upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa Aprili 30, mwaka huu, kwa maelezo kuwa kulazimisha suala hilo kutasababisha mpasuko na hatimaye kuzua vurugu na kuvunja amani ya nchi.
Pia imetakiwa kutokubali kuingiliwa katika utendaji wake wa kazi ikiwamo kulazimishwa kuendesha mchakato wa kura ya maoni katika tarehe hiyo.
Matamko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dar es Salaam Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) jana.
Wazee hao wakimtaka Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, kumshauri Rais Kikwete, kusitisha upigaji kura hiyo, Jukata limeitaka serikali kuacha kuingilia utendaji kazi wa Nec kuhusu daftari hilo na kuilazimisha kuendesha mchakato huo katika tarehe hiyo.
Pia wamemwandikia Jaji Lubuva barua kumsisitiza kutekeleza ombi lao hilo.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Ester Samanya, alisema wanamshauri hivyo Jaji Lubuva kwa kuwa wanaamini kuwa hadi ifikapo tarehe hiyo, uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la kudumu la wapigakura unaoendelea mkoani Njombe kwa kutumia mfumo mpya wa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) utakuwa haujakamilika kote nchini.
Alisema hali hiyo inatokana na nyenzo za kufanikisha kazi ya uandikishaji wapigakura katika daftari hilo, ikiwamo muda, vifaa na wataalamu, kutoandaliwa.
Samanya alisema kauli zinazokinzana kati ya Jaji Lubuva na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, juu ya uwezekano wa kura hiyo kupigwa katika tarehe hiyo au la, zinaashiria kuwa serikali inataka mtu wa kufa naye.
Hivyo, alimshauri Jaji Lubuva kutokubali kuingia kwenye kashfa ya kujivunjia heshima, badala yake amshauri Rais Kikwete kusitishwa mchakato huo.
“Ili kuiepusha nchi na uvunjifu wa amani, uandikishaji usitishwe. Hilo siyo msiba, lazima liandaliwe. Kulilazimisha, ni sawa na kulazimisha jogoo kutaga. Lubuva asiwe mbuzi wa kafara,”Samanya.
Aliongeza: “Tunachokiona ni fujo inayotaka kutokea, kwani hilo (la kura ya maoni) haliwezi kutekelezeka.”
Kaimu Katibu Mkuu Baraza hilo Taifa, Erasto Gwota, alisema uandikishaji wapigakura kwa kutumia mfumo wa BVR katika nchi nyingi umefeli na kwamba, unafanywa nchini ili kuvuruga uchaguzi mkuu ujao.
“Lubuva amshauri Rais jambo hili lisitishwe. Tukilazimisha hili, wengine watakosa kupiga kura,” alisema Gwota na kushauri kura ya maoni ipigwe baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katika barua yao yenye kichwa cha habari: “Uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia BVR hapa nchini, ambayo ilitarajiwa kupelekwa Nec jana, walimtaka Jaji Lubuva kuangalia upya uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwazuia wananchi kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma jana wakati alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali mkoani Mbeya waliokwenda kumshawishi atangaze nia kugombea urais.
Lowassa ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema kuwa kwa kuandaa makundi ya kumshawishi, mbunge huyo wa Monduli anajua adhabu yake na anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea urais kupitia CCM.
“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu jana kuna watu wamesema maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo vya habari. Mnazungumza, mnaelewana mnatoka pale,” alisema.
“Na utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni vigumu kuuzuia, utazuiaje mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu nazuia kwa mikono nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema.
Lowassa ambaye hivi karibuni aliweka bayana kuwa ameshawishika kuwania nafasi hiyo, alisema, “Lakini mambo ya chama hayawezi kuwa kwenye ma-TV, magazeti na maredio, mara huyu hivi, mara huyu vipi. Mkiona chama kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari sana, CCM ninayoijua mimi ni ya vikao.”
“Niseme mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti nawaiteni, nakupeni fedha, mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi nikiweka maturubai hapa ni kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na wanasema nawapeni chakula mambo ya ajabu sana na yanasemwa na watu wazima wenye heshima zao,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Juzi walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia chakula nitawaweza? Nyie kwa wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya unamdhalilisha binadamu mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria tumbo. Hamna cha kufikiri isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa awapeni chakula, ni kudhalilisha watu.”
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’ kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15 hadi 20 ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda, akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete alisema, “kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake kwa wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo hivyo kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini sasa itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema Tanzania imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na bahari. “Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa Kati wa Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga hatua kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura (Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha kuwajibika katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka bandari ya Dar es Salaam bila tatizo.
MWANANCHI
Mkazi mmoja wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwabaka watoto wake wawili wadogo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Habari zilizolifikia gazeti hili, zilisema kuwa katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi na watoto wenyewe, baba huyo alianza kuwafanyia binti zake vitendo hivyo mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe ambaye nimama wa wasichana hao hakuwapo hadi usiku wa Machi 19, mwaka huu. Kwa sasa tunayahifadhi majina ya familia hiyo.
Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 15 anayesoma darasa la saba na mdogo wake mwenye umri wa miaka 11 aliyeanza kubakwa akiwa darasa la tatu.
Kwa mujibu wa watoto hao, baba huyo alikuwa anamuita mmoja wa watoto wake chumbani kwake na kumtaka alale na mdogo wao wa kiume wakati huo akiwa na mwaka mmoja na binti akipitiwa na usingizi humvua nguo za ndani na kumwingilia huku akimtaka kukaa kimya na kuvumilia maumivu.
Mke wa mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa akizimia mara kwa mara kutokana na kulia baada ya kubaini mchezo huo, alisema aligundua watoto wake wanabakwa Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa mabinti zake hao kumweleza kuwa baba yake alikuwa amembaka Machi 19, mwaka huu.
Alisema kabla ya binti huyo kumweleza hivyo, alimwomba asimpige kwani kuna kitu anataka amweleze, japo ni kibaya lakini yeye amechoshwa na kimekuwa kikimuumiza kichwa.
“Alisema kila ninapokwenda katika biashara zangu, anatamani nisiwe ninawaacha hapo, nikamwahidi sitamfanya kitu ili mradi aseme ukweli tu,” alisema mama huyo.
Baada ya kuhakikishiwa kulindwa, ndipo binti huyo aliposimulia jinsi ambavyo baba yake amekuwa akiwafanyia na kuwatishia wakipiga kelele atawaua.
“Niliposikia mwili ulisisimka na ghafla binti yangu mwingine naye akatokea akilia na kuniambia, ‘hata mimi baba ananifanyiaga hivyohivyo kila siku unapokuwa umepeleka mboga sokoni Kariakoo,” alisema mama huyo.
Mwanamke huyo ameomba sheria ichukue nafasi yake katika tukio hilo kwa kuwa ni la kinyama na pia wataalamu wa saikolojia wamsaidie binti yake mdogo wa darasa la tano kwani yeye ameathirika zaidi.
Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.
uu
MWANANCHI
Wanaharakati nchini wamesema rais ajaye anaweza kuwa mwanamke kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo wingi na hamasa waliyonayo wanawake katika upigaji kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema ingawa wanatambua uchaguzi ni mapambano, wanaamini kama wanawake na jamii itakubali mabadiliko, nchi itaongozwa na rais mwanamke.
Wanaharakati hao kutoka vyama vya Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walisema hakuna kinachoshindikana kama wanawake wataamua.
Ulingo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Anna Abdallah alisema, baada ya wanawake kuangaliwa kama kundi duni katika nyanja za siasa kwa muda mrefu, sasa ni zamu yao kujitokeza wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya urais.
“Lengo letu sisi ni mwanamke kujitokeza, akijitokeza tutamuunga mkono kwa umoja wetu bila kujali anatoka chama gani cha siasa,” alisema mwenyekiti huyo aliyeeleza kuwa jamii ya sasa ina imani kubwa na mwanamke.
Aliongoza “Iwapo wanawake watafanya kile tunachotaka , kwa maana ya kuwaunga mkono wagombea, kupiga kura, wakati wa kupata rais mwanamke umefika. Hilo halina ubishi na linawezekana.” Anna alitaja sababu nyingine za kuwashawishi wanawake wajitokeze kugombea urais kuwa ni kuongezeka kwa uelewa wa wanawake katika masuala ya siasa.
TGNP
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, (TGNP), Lilian Liundi alisema wanawake kuwa viongozi siyo ajabu kwani tayari wameshafanya hivyo katika nafasi mbalimbali. Isipokuwa wanahitaji kuungwa mkono katika nafasi za kisiasa.
MTANZANIA
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),imesema vijana wenye umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea, wanaongoza kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,Mkurugenzi wa NIMR,Dk.Mwele Malecela alisema kwa sasa tatizo hilo ni kubwa ambalo linawakumba vijana wengi hususan barani Afrika.
Alisema hali hiyo,imesababisha vijana hao kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume aina ya Mundex,ili waweze kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.
“Vijana wengi wenye umri wa kuanzia miaka 30 na kuendelea wana matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume, jambo ambalo limewafanya kutafuta dawa za kuongeza nguvu ili waweze kuzitumia na kupunguza ukubwa wa tatizo.
“Tangu tugundue dawa hii, idadi kubwa ya wanaokuja kununua ni vijana hasa wenye umri wa miaka 30,hali ambayo inaonesha wazi kuwa tatizo hili linakua kwa kasi,”alisema,”alisema Dk Mwele.
Alisema kipindi kilichopita, matatizo hayo yalikuwa yanawapata wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, lakini sasa hivi ni tofauti kabisa ambapo vijana wenye umri huo ndiyo wenye matatizo hayo.
“Miaka iliyopita tatizo hili lilionekana ni la watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea,sasa hivi ni tofauti kabisa ambapo matatizo hayo yameshamiri kwa vijana, jambo ambalo limewafanya kutafuta dawa ndani na nje ya nchi ili waweze kujitibia,”alisema.
Alibainisha kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na tiba mbadala walifanya utafiti na kubaini kuwa dawa ya Mundex inaweza kuwasaidia kupunguza ukubwa wa tatizo.
Taasisi hiyo,pia imebaini idadi kubwa ya wanawake wakiwamo watoto, wana matatizo ya uvimbe tumboni(Fibrous) hasa kwa waafrika.
Alisema dawa hiyo imethibitishwa kisheria na kwamba inaweza kutumika mahali popote kwa sababu haina madhara kwa binadamu.
HABARILEO
Watu watano wamekufa katika matukio matatu tofauti, wakiwemo watatu waliouawa na miili yao kuchomwa moto na wananchi wanaojiita wenye hasira, baada ya kutuhumiwa kuiba ng’ombe 40 katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi, tukio la kwanza lilitokea Machi 24 mwaka huu, majira ya saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Kunanga wilayani Bunda.
Alisema watu hao watatu waliuawa kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe 40, mali ya Julius Malima (56), mkazi wa kijiji cha Kenkombyo Neruma kata ya Neruma wilayani Bunda, baada ya kuvunja zizi na kuanza kuswaga ng’ombe hao, majira ya saa 10:00 usiku.
Alitaja waliouawa kuwa ni Mayala Buluma (29) mkazi wa kijiji cha JinivaKyabakari Wilaya ya Butiama na Mukina Buluma (25), mkazi wa kijiji cha Namhura wilayani hapa, ambao wote ni watoto wa mzazi mmoja.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza>>>twitter Insta Facebook