Muswada wa Mahakama ya Kadhi umeondolewa bungeni na sasa hautajadiliwa katika Mkutano wa 19 wa Bunge unaohitimishwa leo mjini hapa.
Huu ni muswada wa tatu kuondolewa Bungeni baada ya ile miwili ya sekta ya habari ambayo ni muswada wa Sheria ya kupata Taarifa wa mwaka 2015 na ule wa sheria ya huduma wa Vyombo vya Habari iliyoondelewa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Muswada huo ulipangwa kuwasilishwa Bungeni leo, lakini serikali imeamua kuuondoa kutokana na hofu ya kutokea mpasuko nchini.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, akizungumza jana ofisini kwake alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautakuwapo tena katika mkutano huo.
Dk. Kashilila alisema haijulikani ni lini utawasilishwa bungeni kwa sababu Mkutano wa Bunge ujao unaotarajia kufanyika Mei, utakuwa mahsusi kwa ajili ya bajeti.
“Waziri Mkuu alivyosema wataangalia na kushauriana kimsingi, alitoa maneno ya busara tu au ilikuwa kauli ya mtu mzima, lakini huu muswada hautakuwapo,” alisema.
Dk. Kashilila alisema hali iliyojitokeza Jumapili iliyopita wakati wa semina ya wabunge haikuwa nzuri kutokana na mvutano mkali miongoni mwa wabunge.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alipoulizwa kuhusu kama muswada huo utawasilishwa bungeni, alisema hakuwa na majibu badala yake alitaka suala hilo iulizwe ofisi ya Spika.
“Suala hili usiniulize, nenda Ofisi ya Spika au muulize huyu (Magati) ambaye yupo sekretarieti,” alisema huku akiwa na haraka kuelekea ofisini kwake.
Naibu Spika, Job Ndugai, akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya kuahirisha Bunge, alisema muswada wa Mahakama ya Kadhi hautawasilishwa bungeni leo.
“Huo muswada hauwezi kuletwa bungeni kutokana na hali ilivyo,” alisema Ndugai bila kufafanua zaidi.
Naye Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro, alipoulizwa kama muswada huo utawasilishwa bungeni alimtaka mwandishi asimuulize maswali yanayohusiana na muswada wa Mahakama ya Kadhi.
“Sitaki kabisa kuulizwa suala la Muswada wa Mahakama ya Kadhi, kwanza wewe unatoka gazeti gani, “alijibu Dk. Migiro kwa hasira huku akiingia kantini.
Katika hatua nyingine, juzi jioni maaskofu zaidi ya 40 kutoka mikoa yote nchini, walikutana na wabunge katika ukumbi wa Kanisa La Kiinjili la Kilutheli (KKKT) mjini Dodoma kujadiliana suala la muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa katika mkutano, maaskofu walitoa azimio kuwa muswada huo usiwasilishwe bungeni kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha amani iliyoko nchini.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Watu hao wanatuhumiwa kufukua kaburi la mtu huyo na kuchukua kila kiungo cha mwili wa mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Bartazar John, aliyefariki mwaka 1991.
Hatua hiyo imechukuliwa na jeshi hilo zikiwa zimepita siku saba tangu watu wengine wawili kutiwa nguvuni kwa tuhuma za kuhusika kuuza viungo vya marehemu Wilaya ya Muleba, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, alisema watu hao walikamatwa Machi 27, mwaka huu, katika nyumba moja ya kulala wageni, iliyoko eneo la Kyaka, Wilaya ya Missenyi baada ya kukutwa wakiwa na baadhi ya viungo hivyo, ambavyo walikuwa wanakwenda kuviuza.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Laston Faustine (41), ambaye ni mkazi wa Lukulaijo aliyekutwa na mfuko uliokuwa umehifadhi mifupa mitatu ya binadamu na mwingine ni January Korongo (43), mkazi wa Kadengesho, wiyani Karagwe.
Kamanda Mwaibambe alisema baada ya kumbana, mtuhumiwa wa kwanza, Laston aliliambia Jeshi la Polisi kuwa aliyempa viungo hivyo ni mwenzake, January, kwa ajili ya kuviuza kwa Sh. milioni 20.
Baada ya kuhojiwa, January alikiri kufukua kaburi la mjomba wake, aitwaye Baltazari aliyekuwa na ulemavu wa ngozi albino pia mlemavu wa viungo, ambaye alifariki dunia mwaka 1991 na walifukua kaburi lake mwaka 2009.
Mwaibambe alisema baada ya kumhoji zaidi mtuhumiwa huyo, alikubali kuongozana na polisi hadi nyumbani kwake, ambako alionyesha fuvu la kichwa, mifupa mitatu ya miguu pamoja na mifupa ya sehemu mbalimbali, ambayo ilikuwa imefungwa kwenye mfuko nje ya nyumba yake.
Polisi waliomba kibali cha Mahakama Wilaya ya Karagwe kuruhusiwa kufukua kaburi hilo ili kuhakikisha kama kweli kuna mabaki ya mwili huo, lakini hakuna kilichopatikana.
NIPASHE
Jukwaa la Wakristo Tanzania, limesema linashangazwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali wenye tabia ya kuitisha mikutano wanayoiita ni ya viongozi wa dini huku ikiwa siyo rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Jukwaa hilo, imeeleza kuwa viongozi hao wamekuwa chanzo cha mvutano uliopo baina ya dini mbili na kwamba watakuwa chanzo cha kuvurugika kwa amani nchini.
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mkuu Habari na Mawasiliano wa Baraza la Kikiristo Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo, ilisema jopo la Maaskofu kutoka TEC, CPT lilikutana Machi 30, mwaka huu, mjini Dodoma, kuondoa dhana kuwa linaongozwa na hasira na mihemko katika kufikia maamuzi linavyoyafanya kama wengine wanavyotafsiri bali linasukumwa kwa upendo wa wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano.
Kamoyo alisema Machi 03, 2015 Waziri Mkuu aliitisha mkutano kupitia Mchungaji mmoja ambapo hakuna kiongozi wa taasisi au Kanisa aliyeshiriki, na kwamba Machi 28, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete, alikutana na kikundi ambacho sio rasmi yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Maaskofu tuliokutana Dodoma hatuongozwi na hasaira wala mihemko katika kufanya uamuzi kama wengine wananavyotafsiri, tunafikia uamuzi baada ya maombi kwa upendo wa wananchi na kujenga taifa lenye umoja na amani,” alisema Mchungaji Kamoyo.
Kamoyo alisema walikewenda Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada wa Sheria mbalimabali za mwaka 2014 pamoja na mrekebisho mengine ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964.
MWANANCHI
Siku tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.
Katika tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana juzi mjini Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo itakayolaumiwa.
Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Tamko hilo la maneno 921, limeendelea kuwataka waumini wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya ‘hapana,’ msimamo ambao tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya kura wanayostahili kupiga.
Pia, Jukwaa hilo limewataka viongozi wakuu wa Serikali –Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu waliokutana nao si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au kukubaliana juu ya jambo la kitaifa.
“Maaskofu tuliokutana hapa (mjini Dodoma) hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga Taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano,” lilisema tamko hilo likihitimishwa kwa maneno ya Biblia kutoka Mithali 29: 1, “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, atavunjika ghafla, wala hapati dawa.”
Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao… hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
Maaskofu hao walikuwa Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964 unaotambua Mahakama ya Kadhi.
“Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa,” Ilieleza taarifa hiyo.
MWANANCHI
Askari polisi wawili wameuawa na mmoja kujeruhiwa baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa na viashiria vya ama ugaidi au ujambazi katika kizuizi cha barabara ya Kilwa, Kipara Mpakani, Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Tukio hilo ambalo tayari limelaaniwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu, limekuja katika kipindi ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amepangua makamanda na maofisa wa polisi 160 nchini kote.
Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ikisema inachunguza chanzo cha vifo vya askari hao ambao ni wa kanda hiyo, Chikawe alisema tukio hilo linawezekana kuwa la kigaidi au ujambazi lenye lengo la kuchukua silaha kwenda kufanyia matuko mbalimbali.
Askari waliouawa ni D.2865 SGT Francis na E.177 CPL Michael wakati aliyejeruhiwa ni D 5573 D/SGT Ally.
Walioshuhudia tukio hilo walisema lilitokea juzi saa mbili usiku na kudumu kwa dakika 10 na kufanya eneo hilo kuwa kama uwanja wa vita kutokana na milio ya risasi.
Mkazi wa eneo hilo, Mohamed Ali alisema aliwaona watu watano wakitokea katika Pori la Kipara Mpakani, mmoja akiwa ameshika bunduki na mwingine panga.
“Niliwaona wakiwafuata askari karibu na kizuizi, mmoja alimpiga polisi risasi kifuani na mwingine akamkata polisi kwa panga shingoni,” alisema na kuongeza kuwa aliwaona askari hao wakiwa wamelala chini baada ya kuuawa… “Baada ya tukio hilo, watu wote waliokuwa karibu na eneo hili walikimbia kujificha wakihofia usalama wao.”
Shuhuda mwingine, Shiraz Abdul alisema alimwona mmoja wa askari mwingine akikimbia pamoja na wananchi baada ya tafrani hiyo… “Niliwaona askari watatu wakiwa wamelala chini, mmoja akiwa analia kuomba msaada,” aliongeza.
Shuhuda, Rehema Yusuph ambaye anaishi karibu na barabara kilipo kizuizi hicho alisema, walianza kusikia watu wakipiga kelele na kuhisi kwamba ilikuwa ajali.
“Mara nyingi huwa ajali zinatokea hapo barabarani, kwa hiyo sisi tulidhani kwamba ilikuwa ajali. Lakini baada ya sekunde chache tulianza kusikia milio ya risasi. Mara nikaona watu wanakimbilia kwenye veranda yangu, baada ya kuuliza wakasema kuna watu wamevamia hicho kituo na wameua na kujeruhi askari.”
MTANZANIA
Ni maumivu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kutoka Hospitali ya TMJ alikokuwa amelazwa kwa siku tano kwa kutumia baiskeli ya wagonjwa (wheelchair) kwenda Kituo cha Polisi Oysterbay kuhojiwa kwa mara ya pili.
Askofu Gwajima, alipandishwa kwenye baiskeli hiyo, baada ya kupelekewa na mmoja wa wafuasi ambaye alikuwa amevalia mavazi ya kichungaji.
Wakati akipelekwa katika gari Askofu Gwajima, alionekana akigugumia kutokana na maumivu makali ambayo haikujulikana mara moja chanzo chake.
Baada ya wafuasi wake kukamilisha taratibu zote, ilipofika saa 6:15 mchana, gari la polisi aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili KX 06 EFY liliwasili hospitalini hapo.
Gari hilo, lilikuwa na askari wanne, mmoja akiwa ni ofisa wa polisi aliyekuwa amevalia sare za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wengine wakiwa wamevalia kiraia.
Askari hao ambao walikuwa wamebeba bunduki walikwenda moja kwa moja wodini na baadae kutoka pamoja na kiongozi huyo wa kiroho.
Baada ya muda kidogo, askari hao walishuka chini na ilipofika saa 06:34 chana, gari nyingine ndogo aina ya Yutong MG 6 Turbo yenye namba STL 110 iliwasili eneo hilo ikiwa na askari mmoja.
Ilipofika saa 6:45, Askofu Gwajima alishushwa katika lifti ya hospitali hiyo, akiwa anasindikizwa na zaidi ya watu wane, huku yeye akiwa amekaa kwenye baiskeli hiyo na kupandishwa moja kwa moja kwenye gari la polisi.
Akiwa anainuliwa kwenye kiti na kupandishwa katika gari, Askofu Gwajima alionekana akikunja uso na kufungua mdomo kama mtu anayegugumia kutokana na maumivu makali.
Baada ya kutoka hospitalini, msafara huo ulielekea moja kwa moja Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
Alifikishwa kituoni hapo saa 6:55 na kupelekwa chumba kilichokuwa kimeandikwa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni.
Alipofika mlangoni alikutana na ofisa mmoja, ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja, alimuaru asubiri ili wakili wake afanye taratibu za dhamana.
“Subiri hapa mfanye taratibu za dhamana mkishamaliza hakikisha Alhamisi (kesho) unaripoti Central Polisi (kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam),”alisikika ofisa huyo akisema.
Wakati taratibu za dhamana zikiendelea, wafuasi wa Askofu Gwajima waliendelea kukusanyika eneo hilo kwa madai kuwa wanamsubiri kiongozi wao.
Wakiwa wamekusanyika makundi makundi, huku wengine wakiwa wameshikilia makaratasi yenye maandishi na picha ndogo kwa ajili ya kusaidia udhamini kama ukihitajika.
MTANZANIA
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umelaani na kusikitishwa na kauli za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuitupia lawama CCM kwa kudai imehusika katika kushambuliwa wafuasi wao.
Wakati CCM wakitoa kauli hiyo, CUF kimemtupia lawama Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Balozi Seif Ali Idd kuwa ndiye amekuwa akitoa kauli za kuchochea vurugu visiwani humo.
Taarifa ya UVCCM Zanzibar kulaani matamshi hayo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu wake, Shaka Hamdu Shaka.
Wafuasi wa CUF walivamiwa na kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa CCM, ambapo katika vurugu hizo watu 25 waliokuwa wakitokea katika mkutano uliokuwa unafanyika Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja walijeruhiwa.
Shaka alisema katika taarifa yake kwamba baadhi ya viongozi wa CUF wakiwamo wawakilishi wa chama hicho, kwa nyakati tofauti wamesikika na kunukuliwa na vyombo vya habari wakidai shambulio hilo la kudhuru limepangwa na kufanywa na vijana wa CCM jambo alilosema si kweli na halina ushahidi.
“Shutuma za CUF kwa namna moja au nyingine zimejiegemeza katika kuficha ukweli wa chanzo halisi kwani itakumbukwa hivi karibuni Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad katika moja ya mikutano yake ya hadhara alioufanya Kiembesamaki, sehemu kubwa ya hotuba yake ililenga kuwahamasisha na kuwachochea vijana wa chama chake kujiandaa kwa vurugu na kutotii sheria za nchi.
“UVCCM tunaamini vitendo hivyo viovu na vya kikatili vilivyofanyika ni matokeo ya matamshi ya uchochezi yaliyotolewa na katibu mkuu huyo na kuonyesha ni chimbuko la kuanza kushamiri matukio ya uvunjaji wa sheria kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema.
Alisema mara kadhaa UVCCM imekuwa ikihimiza na kuwataka viongozi wa juu wa kisiasa kuchunga ndimi zao ili kuendesha siasa za kuvumiliana, kushindana kwa nguvu ya hoja, pia kuyaenzi na kuyalinda maridhiano ya kisasa yaliyofikiwa kati ya vyama vya CCM na CUF hadi kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010.
“Inashangaza hivi leo kumuona mmoja kati ya viongozi wanaojinasibu ni muumini na waasisi wa maridhiano akipanda majukwaani na kuanza kurejesha siasa za “mti kwa macho” na kushupaliana huku akitoa semi za uvunjaji wa sheria, akisema yuko tayari hata kupigwa mabomu na kuwa wa kwanza kuuawa hali inayoonyesha anakumbatia uvunjaji wa sheria,” alisema Shaka katika taarifa yake.
Chama cha CUF kimesema kutokea kwa vurugu kisiwani Unguja juzi, kumesababishwa na kauli iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Salum Bimani, alisema dalili za kutokea kwa vurugu na watu kujeruhiwa zilianza muda mrefu.
HABARILEO
Polisi mkoani Katavi inamshikilia mkazi wa kitongoji cha Ntumba, kijiji cha Mnyengele wilayani Mpanda, Deogratius Pastory (30) kwa kumjeruhi vibaya mkewe kwa kumkata mkono wake wa kushoto na kupasua tumbo la mpenzi wa mkewe kwa panga.
Mtu huyo aliwatendea unyama huo baada ya kuwafumania mkewe aitwae Tabu Nestory (20) na mpenzi wake wa kiume aitwaye Masaga Elias (28) wakifanya mapenzi katika jiko la nyumbani kwake kijijini humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha mkasa huo.
Alisema tukio hilo ni la Machi 23, mwaka huu saa tano usiku katika kitongoji cha Ntumba katika kijiji cha Mnyengele. Akielezea mkasa huo, Kidavashari alidai kuwa jioni ya siku hiyo ya tukio, mtuhumiwa alimuaga mkewe Tabu kuwa anakwenda kijiji ambacho kiko umbali mrefu kutoka kijijini hapo kwa ajili ya kuangalia shamba lao.
Inadaiwa mtuhumiwa huyo alitumia baiskeli yake katika safari yake hiyo. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, wakati mtuhumiwa huyo akiendelea na safari yake ghafla baiskeli yake aliyokuwa akiitumia katika safari yake hiyo iliharibika, wakati huo ilikuwa tayari imetimu saa tatu usiku .
“Kwa sababu alikuwa bado amebakiza mwendo mrefu kufika alikokuwa akienda aliamua kugeuza na kuanza kurejea nyumbani kwake, ambako alifika saa tano usiku …na alipofika kwake alimkuta mkewe na mpenzi wake wakifanya mapenzi katika jiko nyumbani kwake,” alieleza.
Inadaiwa kuwa kitendo hicho kilimkasirisha mtuhumiwa, ambaye alimwamuru mkewe na mgoni wake kuingia ndani, ambapo alimkamata mwanamume huyo na kumfunga kamba mikononi, kisha akachukua panga na kumchana tumbo chini ya kitovu hadi utumbo wake ‘ukamwagika’ nje .
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, mtu huyo alitumia panga hilo alilotumia kuchana tumbo la mgoni wake, kukata mkono wa kushoto wa mke wake.
HABARILEO
Wazazi 19 wa wanafunzi walioshindwa kuripoti kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2014/2015 wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi mitatu kila mmoja kutokana na kosa la kushindwa kuwapeleka watoto wao shuleni.
Wazazi waliohukumiwa kifungo hiki ni wale wa kata za Mpindimbi na Lukuledi zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Mtwara Aidha, wametakiwa kuripoti kwenye Mahakama ya Mwanzo ya Lisekese wilayani hapa kila baada ya wiki mbili wakati wote watakapokuwa wanatumikia adhabu yao.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Lisekese wilayani Masasi, Gloria Mkwera karani wa mahakama hiyo, Agnes Hanga alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo mwanzoni mwa mwaka huu kwa waliposhindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto wao shuleni huku wakijua ni wajibu wao.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook