Siri mpya juu ya Mtanzania Rashid Charles Mberesero, anayehusishwa na tukio la kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya zimeibuka.
Kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari vya Kenya, Mtanzania huyo anayedaiwa kuwa miongoni mwa magaidi wa Al-Shabaab walioua watu 148 katika chuo hicho, endapo angesalimika baada ya tukio hilo, angepelekwa Somalia yalipo makao makuu ya kundi hilo la kigaidi.
Hayo yalibainishwa jana na mwendesha mashtaka wa nchi hiyo, Daniel Karuri katika mahakama ya jijini Nairobi.
Mahakama hiyo imeamuru Rashid akae kizuizini kwa siku 30 akisubiri uchunguzi wa tuhuma zake.
Pia watu wengine 14 wanaotuhumiwa kuhusika na kundi la Al Shabaab wameamuriwa wakae rumande kwa muda wa siku 30 wakisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Polisi inaendelea kuchunguza mawasiliano ya simu waliyokuwa wakifanya watuhumiwa hao kwa ajili ya kutafuta ushahidi zaidi wa wahusika wote wa shambulio hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka husika, Rashid alikamatwa akiwa amejificha juu ya dari la chuo hicho akiwa ameshikilia silaha na mlipuko.
Mmoja miongoni mwa watuhumiwa hao alikamatwa katika chuo kikuu hicho, akiwa anafanya kazi kama mlinzi na wengine walikamatwa wakati wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia Somalia.
Wakati walipovamia chuo hicho, wauaji waliwatenga wanafunzi wa Kiislamu na wale waliobainika kuwa Wakristo waliuawa kwa kupigwa risasi.
Kundi la Al Shabaab limedai kuhusika na mauaji hayo na kwamba tukio hilo lilidhamiria kutuma salamu kwa Serikali ya Kenya ambayo imehusika kutuma majeshi yake Somalia kupambana na kundi hilo.
Mama mzazi wa Rashid, jana alilieleza gazeti hili kuwa wakati Mkuu wa Shule ya Bihawana, Mbilinyi Joseph akisema tangu Novemba mwaka jana mtoto huyo alitoroka shuleni, yeye anajua mwanawe huyo kwa kipindi cha mwisho wa mwaka alibaki shule ili asome masomo ya ziada.
“Alisema hakuona sababu ya kusubiri hadi shule ifungwe kwa sababu wakati huo wenzao wakifanya mtihani, wao hawakuwa wakisoma, kwa hiyo ameamua kurudi nyumbani,”
MTANZANIA
Mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amejiunga na Chama cha Alliance for Change &Transparency-Tanzania (ACT).
Binti huyo aliyejiandikisha kwa jina la June Warioba, alichukua kadi ya kujiunga na chama hicho makao makuu ya chama hicho Kijitonyama mjini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, June alikataa kupigwa picha wala kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwapo ofisini hapo.
Aliingia ofisini hapo saa 4 asubuhi ambapo alitumia takribani nusu saa kufanikisha usajili wa chama hicho na kutoka ndani akiwa ameongozana na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa.
June alikuwa amejiziba uso kwa mkono ili asipigwe picha wala kuulizwa maswali ambapo aliingia kwenye gari na kuondoka.
Alipoulizwa kwanini amejiunga na chama hicho kimya kimya na kwa haraka, alisema huo ni uamuzi wake.
Naye Mwenyekiti wa ACT, Anna Mughwira alisema June hakutaka kuandikwa kwenye vyombo vya habari,hivyo waliheshimu uamuzi wake huo.
Alisema kila mwanachama ana uhuru wa kuamua namna ya kujiunga, kwani wapo wanataka waandikwe au kutangazwa na vyombo vya habari na wengine hawapendi.
“Si mtoto wa Warioba, ni mwanachama wa kawaida tu hajasema chama alichotoka wala hajaweka wazi kama anataka kugombea nafasi yoyote ya uongozi na hakupenda kuandikwa ni kama mimi nilivyoingia” Mughwira.
Jaji Warioba alikiri June ni mtoto wake wa kumzaa na kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na ACT alisema aachiwe mwenyewe.
“Yule ni mtu mzima, hayuko chini yangu na ana uamuzi wake… siwezi kumwingilia uhuru wake,” Jaji Warioba.
MWANANCHI
Sasa ni dhahiri kwamba polisi wamemshika pabaya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kumhoji na kisha kumtaka arejee katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Aprili 16, mwaka huu akiwa na vitu 10 vinavyohusu usajili, umiliki, uongozi na mali za kanisa analoliongoza.
Hatua hiyo imekuja kinyume na matarajio yake na ya wengi kuwa kiongozi huyo angekuwa anahojiwa tu kuhusu matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa kuripoti polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu lakini kabla ya mahojiano yao kukamilika aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa na kuhojiwa taarifa binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.
Hata baada ya kutoka hospitalini, Gwajima aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia hadi Aprili 6 alipohubiri katika Ibada ya Pasaka.
Siku iliyofuata askofu huyo alitupa kiti hicho akidai kuwa amepona baada ya maombi ya wachungaji wageni waliofika kanisani hapo kutoka Japan.
Baada ya mahojiano ya jana, wakili wake, John Mallya alilalamikia hatua ya polisi akisema mahojiano kuchukua mkondo wa mambo binafsi badala ya kile alichoitiwa na kusema watakwenda kulalamikia hatua hiyo mahakamani.
Wakili huyo alitaja mambo yanayotakiwa kuwasilishwa polisi kuwa ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Mallya alisema watalalamika suala hilo litakapofika mahakamani kutokana na mteja wake kuhojiwa masuala tofauti na kile kinachodaiwa kutoa lugha ya matusi.
Alisema mteja wake amehojiwa muda mrefu kwa sababu alikuwa akihojiwa masuala binafsi yakiwamo ya familia yake, watoto wake, ndugu zake hadi waliokufa.
“Mahojiano yamekuwa ya muda mrefu, cha kushangaza kaulizwa maswali binafsi badala ya kile anachodaiwa kukifanya, mahakamani tutahoji hilo,” Mallya.
MWANANCHI
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi kwa sasa wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kila kukicha.
Mahita aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na kuongezeka kwa uhalifu, inafikia hatua wahalifu wanawaingilia polisi kwa kuvamia vituo vya polisi na kupora silaha ilhali zamani hakukuwa na matukio hayo.
Hata hivyo, IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo akisema: “Siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho, kwa sasa hakipo.”
Kauli ya Mahita imekuja miezi minane baada ya askari 10 kuuawa na bunduki zaidi ya 20 kuporwa katika matukio mbalimbali ya uvamizi wa polisi na vituo vya polisi.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita, Oysterbay Dar es Salaam juzi, Mahita alisema: “Ili kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyozidi kuongezeka kila kukicha, ni lazima askari warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu popote walipo.
“Askari lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Mahita alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa hilo ni suala lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani ya jeshi hilo na polisi… “Unambembelezaje mhalifu? Hawa ni watu wanaostahili kubanwa kwa kila namna ili kukomesha vitendo vyao katika jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa, madhara yake ni makubwa katika jamii.”
Licha ya suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza umuhimu wa doria katika kudhibiti uhalifu wa kila siku ambao hupunguza amani miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ratiba waliyojiwekea.
Alitolea mfano wa vikundi vya uhalifu vilivyojitokea hivi karibuni kama ‘Panya Road’, ‘Mbwamwitu’ na ‘Libya’ kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa doria inayotakiwa ifanywe na jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya mijini.
“Enzi zangu doria ilipewa kipaumbele. Magari na pikipiki yalikuwa yanazunguka kote katika jiji hili na kwingineko mikoani karibu kila siku na walikuwa wanaogopeka… kwa sasa yapo lakini sidhani kama wanafanya kazi kama ilivyokuwa enzi zile,” Mahita.
MWANANCHI
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza mgawo wa umeme kwa siku tisa katika baadhi ya maeneo kutokana na upungufu wa nishati hiyo katika Gridi ya Taifa.
Hali hiyo imetokana na maombi ya Kampuni ya Pan African Energy (PAT) inayosimamia uzalishaji wa gesi asilia Songosongo kusimamisha uzalishaji kwa nyakati tofauti ili kufanya matengenezo na kubadilisha baadhi ya vifaa kwenye mitambo yake.
Taarifa ya shirika hilo kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilisema shughuli hiyo itafanyika kwa siku tofauti kati ya Aprili 6 na Mei 10.
“Hivyo Shirika linawatangazia wateja wake waliounganishwa kwenye mfumo wa gridi ya Taifa kwamba kutakuwa na upungufu wa umeme kwa baadhi ya maeneo kutokana na matengenezo hayo yanayofanyika kila mwaka,” ilisema.
Tanesco inategemea gesi hiyo kuendesha mitambo yake ya Ubungo 1, Ubungo 2 na Tegeta yenye uwezo wa kufua megawati 245 na kuendesha mitambo mingine ya umeme ya Songas yenye uwezo wa megawati 180.
Taarifa hiyo ilisema pamoja na kutumia vyanzo vingine vya kufua umeme kama maji na mafuta, katika kukabiliana na matengenezo hayo, ukosefu huo wa gesi utaathiri ufuaji wa umeme kwa siku tisa. Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema upungufu huo kwa kila siku utagawanywa kidogokidogo kwenye mikoa iliyopo kwenye gridi na hautaathiri upatikanaji wa umeme kwa mkoa mzima.
Akizungumzia mgawo huo, Meneja wa Mawasiliano Tanesco, Adrian Severin alisema ukiondoa tatizo hilo la ukarabati wa miundombinu ya gesi, shirika lake halina tatizo la kuilazimisha nchi kuingia katika mgawo kwa sasa.
Pia, aliitaja mikoa ambayo haitaathiriwa na mgawo huo kuwa ni Kagera, Ruvuma, Kigoma, Lindi, Mtwara na Wilaya ya Loliondo, Arusha.
NIPASHE
Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye sifa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa kuwa na watu 2,932,930.
Ripoti ya makadirio ya idadi ya watu na wapiga kura kwa mwaka 2015 iliyowekwa kwenye mtandao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyoonyesha idadi ya watu watakao kuwa na sifa ya kupiga kura mwaka huu kimajimbo na kitaifa kuwa ni watu 24,253,541.
Taarifa hiyo ilisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Mohamed Hafidh Rajab.
Kwa upande wa Zanzibar mkoa wenye wapiga kura wengi ni Mjini Magharibi wenye watu wenye sifa ya kupiga kura 346,524 na wenye wapiga kura wachache ni Kusini Unguja 63,546.
Pia, imeeleza kuwa hadi kufika siku ya uchaguzi mkuu, Tanzania itakuwa na watu wapatao 48,522,228, ikiwa ni watu 47,110,506 wa Tanzania Bara na 1,411,722 wa Zanzibar.
Taarifa hiyo imeainisha kuwa idadi ya wenye sifa ya kupiga kura kati ya hao kwa Tanzania Bara ni 23,533,050 na Zanzibar ni 720,491.
Taarifa hiyo imeanisha majimbo ya Tanzania bara ni 189, Zanzibar ikiwa na majimbo 50, huku kwa Tanzania Bara mikoa inayoongoza kwa majimbo mengi na idadi kwenye mabano ni Tanga (11), Mbeya (11), Morogoro (10) na mingine ikiwa na majimbo chini ya kumi, na wenye majimbo machache ni Katavi ambayo ni matatu.
Upande wa Zanzibar mkoa wenye majimbo mengi ni Mjini Magharibi majimbo 19 na Kusini Unguja majimbo matano.
NIPASHE
Zaidi ya watoto milioni 2.7 nchini bado wanakabiliwa na tatizo la utapiamlo kutokana na lishe duni na iwapo hatua hazitachukuliwa mapema kudhibiti hilo, watoto zaidi ya 500,000 watapoteza maisha ifikapo mwaka 2025.
Hayo yalibainishwa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa dunia kuhusu masuala ya lishe duniani, jana jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na utapiamlo nchini ukiwamo wa 2011/12 hadi 2015/2016 ambao umesaidia kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.7 mwaka uliopita.
Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine, inalenga kuweka viini lishe kwenye vyakula na kwamba tangu kuzinduliwa kwake, takribani watu milioni 20 wamefikiwa na mazao ambayo tayari yamewekewa viini lishe.
Hata hivyo, alisema bado nchi ipo katika safari ndefu katika kufikia malengo ya milenia ya mkutano wa afya wa dunia na yale ya Tanzania ya mwaka 2025.
Rais Kikwete alisema wasiwasi wa kutofikiwa kwa malengo hayo ya kidunia na yale ya kitaifa, unatokana na taifa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye tatizo la utapiamlo ambao kwa sasa ni takriban milioni 2.7.
Alisema, asilimia 58 ya watoto hao, wanatoka katika mikoa 10 nchini ambayo inakabiliwa na tatizo kubwa la lishe.
Rais Kikwete alisema ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na wadau wengine zikiwamo sekta binafsi katika kukabiliana na suala hilo, vinginevyo, watoto takriban 580, 687 nchini wapo hatarini kupoteza maisha ifikapo mwaka 2025.
NIPASHE
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, amewajia juu baadhi ya viongozi wa dini kwamba wanawapotosha wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa inapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Mangula amesema kuwa katiba hiyo haina ibara inayozungumzia masuala ya dini na Mahakama ya Kadhi na kuwataka wamuonyeshe kipengele kinachotaja masuala hayo.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wa sekondari, wanachuo na walimu wa Shule ya Sekondari Hagaf.
Mangula alifafanua kuwa ameisoma Katiba yote na hajaona ibara wala sura inayozungumzia masuala ya udini wala Mahakama ya Kadhi.
Mangula alisema kuwa viongozi wa dini wanawaelekeza wananchi kuikataa katiba hiyo, lakini walichofanya maaskofu ni kutoa matamko ya kupinga kuwasilishwa bungeni na kupitishwa kwa muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Maelekezo yao kwa waumini wao kutokuipigia Katiba kura ya ndiyo, yalitokana na kutoridhishwa kwa viongozi hao na mchakato mzima ikiwamo kusuasua kwa uandikishaji wa wapigakura, kuchelewa kupelekwa kwa nakala za Katiba na mgawanyiko katika Bunge Maalum la Katiba.
“Katiba hii inayopendekezwa nimeisoma yote, lakini sijaona mahali hata panapozungumzia masuala ya dini fulani, lakini nashangaa katika makanisa wananchi wanashawishiwa kutoipigia kura kwa sababu inaunga mkono Mahakama ya Kadhi, hakuna kitu kama hicho,” Mangula.
Alisema alikuwa katika kanisa moja anakosali na Mchungaji aliwaeleza waumini wasiipigie kura Katiba inayopendekezwa kwa kuwa ina masuala ya Mahakama ya Kadhi na kwamba alipomuuliza ni ibara gani inayozungumzia mahakama hiyo, mchungaji huyo alishindwa kuitaja na kusema haifahamu.
Mangula aliwaeleza walimu na wanafunzi hao kuwa kiongozi yeyote atakayewataka kutoipigia kura katiba hiyo kwa maelezo kuwa ina mrengo wa dini fulani, wamwambie aeleze ni ibara gani inayozungumzia suala hilo.
Alisema kilichomo katika Katiba hiyo ni ibara inayozungumzia utawala wa sheria na kuwapo kwa Mahakama huru.
Alisema kuwa kuna ibara inayoeleza kuwa Jamhuri ya Tanzania itakuwa na utawala wa sheria na huru isiyofungamana na dini yoyote.
HABARILEO
Watu wawili akiwemo jambazi mmoja na askari mwanafunzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamekufa na wengine kunusurika kuuawa katika tukio lililotokea juzi, mjini Mafinga mkoani Iringa wakati majambazi wakirushiana risasi na askari wa Jeshi la Polisi.
Risasi hizo zilipigwa wakati Polisi hao wakijaribu kuokoa fedha za mfanyabiashara Salama Semwaiko zilizoporwa na majambazi wawili waliotumia pikipiki wakati wakifanya uporaji huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema mfanyabiashara huyo aliporwa fedha hizo juzi majira ya saa 2.45 asubuhi alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda kwenye biashara zake.
Tukio hilo la kusikitisha lililovuta hisia za watu wengi na kufanya baadhi kuzimia wengine kukimbia hovyo na kujifungia ndani kwa ajili ya kuokoa maisha yao lilitokea katika eneo la Kinyanambo B, nje kidogo ya mji wa Mafinga.
Kamanda Mungi alisema; “mfanyabiashara huyo akiwa katika gari lake akielekea kwenye biashara zake mjini Mafinga, mfanyabiashara huyo alisimamishwa na mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi na baada ya kusimama alimtolea silaha na kumtaka atoe fedha na vitu vyote vya thamani alivyokuwa navyo .”
“Baada ya kuona hana msaada mfanyabiashara huyo alijikuta akilazimika kutoa Sh 700,000 alizokuwa nazo, simu ya mkononi na baadaye ilitokea pikipiki ambayo haikufahamika namba za usajili na kumpakia mtu huyo na kuanza kukimbilia eneo la Kinyanambo,” alisema.
Alisema mara baada ya majambazi hao kutoweka, Jeshi la Polisi lilipewa taarifa na kuwahi eneo la tukio na kwa kushirikiana na wananchi walianza kuwakimbiza majambazi hao na ndipo majibizano ya risasi yalipoanza.
Katika hekaheka hiyo, Kamanda Mungi alisema Said Ngudi (25) ambaye ni askari wa JKT Makutupora, Dodoma alipigwa risasi na kufa papo hapo wakati akisaidia kupambana na majambazi hao.
Hakuna Stori itakayokupita mtu wangu,niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook