MWANANCHI
Zaidi ya watoto 600 wakimbizi kutoka Burundi wamepotezana na wazazi wao katika harakati za kukimbia nchi yao au kuhamishwa kutoka kambi moja kwenda nyingine mkoani Kigoma.
Baadhi ya watoto hao, walipotezana na wazazi wao wakati wa kupanda meli za Mv Liemba na Mv Malagarasi kutokea Burundi na wengine katika harakati za kwenda Kambi ya Nyarugusu.
Toka Mei Mosi, mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linawasafirisha wakimbizi hao kutoka kambi moja hadi nyingine kwa kutumia meli za Mv Liemba na Mv Malagarasi. Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi katika kambi zote pamoja na utaratibu mbovu wa kuwahamisha kutoka kambi moja kwenda nyingine.
Mfanyakazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM), Frederick Moses alisema uhamishaji ulikuwa haufuati utaratibu maalumu kwa kuwa meli moja kutoka Kagunga kwenda mjini Kigoma ilikuwa inabeba wanaume tu au wanawake tu na nyingine watoto pekee hali iliyosababisha familia kupotezana.
Takwimu kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii iliyopo katika kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika, zinaonyesha kuwa Mei 18, mwaka huu, watoto 53 walipotea, Mei 19 walipotea 124, Mei 20 (160), Mei 21 (81), Mei 22 watoto 145 na Mei 24 walipotea watoto zaidi ya 20.
Hata hivyo, Mollel alisema Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Shirika la Plan International, Unicef na Kamati ya Uokoaji ya Kimataifa (IRC), wanafanya kazi ya kuwatambua watoto waliopotea au waliotengana na wazazi wao na kuwatafutia wazazi wa muda wa kuwalea.
Msemaji wa Plan International, Emmanuel Kihaule alisema watoto hao huhifadhiwa hadi pale wazazi wao watakapopatikana na wale wagonjwa huwekwa katika uangalizi maalumu wa tiba.
“Wapo pia walioathirika kisaikolojia kutokana na kufanyiwa ukatili wa kijinsia, wako kwenye uangalizi maalumu,”.
Baadhi ya watoto hao walisema waliondoka Burundi peke yao huku wengine wakisema walikuwa wanaishi mitaani mjini Bujumbura na waliposikia mapigano wakaamua kufuata mkumbo wa kukimbia.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu kwamba Agosti 21, mwaka huu itakuwa ni siku ya uteuzi wa wagombea urais, ubunge na udiwani.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema tume hiyo imetoa ratiba hiyo kwa mamlaka iliyopewa na sheria.
“Tume inapenda kuviarifu vyama vya siasa na wananchi wote kuwa ratiba hii inatolewa kwa mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa vifungu vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Lubuva alisema vyama vya siasa vitafanya kampeni za uchaguzi kwa siku 64 kuanzia Agosti 22 hadi Oktoba 24, mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema siku ya kupiga kura itakuwa Oktoba 25 kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano inavyosema.
Katiba inasema Uchaguzi Mkuu utafanyika Jumapili ya mwisho wa mwezi Oktoba ya mwaka wa tano tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa mwisho.
Wakati tume ikitangaza ratiba, vyama vya siasa vimeanza mchakato wa kupata viongozi wa ngazi mbalimbali huku CCM na Chadema vikitangaza siku ya kupata wagombea urais kupitia vyama vyao. Juzi, CCM iliweka ratiba ya kupata viongozi ndani ya chama hicho na ikatangaza kuwa kuwa Julai 12, mwaka huu mgombea urais kupitia chama hicho atajulikana.
Chadema pia kimeshatangaza ratiba ya uchaguzi ndani ya chama hicho kuwa mgombea urais atajulikana Agosti 4, mwaka huu. Mgombea huyo ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Chama cha Tanzania Labour (TLP), kimeshamteua, Macmillan Lyimo kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Lyimo alipitishwa kuwania nafasi hiyo katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa chama cha NCCR – Mageuzi, fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zimeanza kutolewa na Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Dk George Kahangwa amechukua fomu za kugombea urais.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana wa CCM kutokuwa makuwadi na madalali wa wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Rais Kikwete aliyasema hayo mjini hapa jana alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu wa CCM.
“Vijana wasigeuke kuwa makuwadi wa kuwahonga vijana wenzao ili wamchague mtu fulani. Kwa kufanya hivyo watakuwa wametoka kabisa nje ya mstari…“Tunataka vijana watakaosema tunatafuta viongozi wa Taifa hili, ila watu wa aina hii hapana,” Kikwete.
Alisema lengo la kuanziasha shirikisho hilo ni kuwaandaa vijana hao ili waujue uongozi na waweze kuwa viongozi wazuri katika siku za baadaye.
“Viongozi wa vijana wanasafirishwa wanaletwa hapa Dodoma kwa ajili ya kumsikiliza mzee fulani, ndiyo maana siku hizi hoja ya vijana siyo tishio kwa mtu yeyote kwa sababu hawana mawazo ya kutoa kwa ajili ya kukijenga chama na Taifa,” .
Pia, aliwataka vijana hao kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hana mpango wa kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo.
Lowassa alitoa kauli hiyo alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana ambako alieleza mambo mbalimbali kuhusu afya yake, suala la Richmond, elimu, ajira, utajiri wake na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mbunge huyo wa Monduli hakutaka kujibu maswali mengi kwa madai kuwa atazungumza Jumamosi mjini Arusha atakapotangaza nia yake ya kugombea urais.
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kuhama CCM na kwenda upinzani asipopitishwa na chama hicho kuwania urais alisema: “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina plan B, mimi ni plan A tu, tangu nimemaliza Chuo Kikuu mwaka 1977 nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.
Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Richmond, alisema kimya chake baada ya tukio hilo kilitokana na siasa nyingi za uhasama na kutishiana.
“Nilinyamaza ili kuipa muda Serikali ifanye kazi yake…. sikupenda kuzungumza kwa sababu ya siasa nyingi za uhasama na kutishiana kwingi, kuna kusingiziana kwingi, kufitiniana kwingi. Kukaa kimya ni jambo gumu sana kwa mwanasiasa, lakini nashukuru Mungu niliweza hilo,” alisema Lowassa ambaye Jumamosi atatangaza nia ya kuwania urais mjini Arusha.
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa afya yake inaterereka, alisema anaamini yupo fiti na akashauri wagombea urais wote wakapimwe.
“Hata nikikimbia kilomita 100 watasema mimi mgonjwa. Hivi karibuni nilitembea kilomita tano na albino jijini Dar es Salaam, kuna watu wakasema nimechoka sana, nimepata ‘stroke’ na nimekimbizwa Ujerumani kutibiwa, huo ni upuuzi mtupu.Kuna chuki imeingia katika siasa zetu na kutakiana mabaya.
Afya ni neema kutoka kwa Mungu tu. Napenda kuwahakikishia kuwa nipo fiti na nipo fiti na kwa lolote. Nadhani ni wakati sasa kwa chama chetu waweke utaratibu wanaogombea nafasi hii ambayo nitaitangaza Jumamosi, tukapime wote afya na mimi nitakuwa wa kwanza kujitokeza kwenda kupima.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amemteua Anthony Peter Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kuanzia jana.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uhamisho wa wakuu 10 wa wilaya kwa nia ya kuongeza ufanisi katika uongozi wa Wilaya mbali mbali nchini.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kuwa, katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amemhamisha Luteni Edward Ole Lenga kutoka Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kwenda kuwa mkuu wa wilaya mpya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera.
Luteni Lenga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Kanali Benedict Kulikela Kitenga ambaye alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu, 2015.
NIPASHE
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ameeleza kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na gazeti la Taifa Imara Machi 20, mwaka huu.
Dk. Mengi, alisema jana kuwa majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza usalama wa maisha yake.
“Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,” alisema Dk. Mengi na kuongeza:
“Ukiangalia, ukisoma kiundani majibu ya barua ya Rweyemamu, nina kila sababu ya kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake Ikulu ni za kuheshimiwa, lakini awe na busara katika shughuli zake….kunishauri eti niende polisi kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina busara kama yeye.”
Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala siyo la kupuuzwa na kwamba busara ilihitajika katika kushughulikia suala hilo, lakini haikuwa hivyo kwani majibu hayo yamesababisha tatizo hilo dhidi ya usalama wa maisha yake kuwa pale pale.
Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara, lilichapisha habari iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara wa kuihujumu serikali yake na alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na mipango hiyo.
Habari hiyo iliendelea kudai kuwa, Dk. Mengi aliapa kumshughulikia Rais Kikwete kwa nguvu zake zote amalizapo muda wake wa urais huku Rais Kikwete naye akiapa kupambana na yeye (Dk. Mengi).
Dk. Mengi alisema majibu yaliyotolewa na kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa Rais hakuwahi kuwa na mawasiliano na Zitto Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba haikufanya lolote kutokana na kubanwa na majukumu, hivyo kupuuza habari hizo kwa kuziona ni ndogo na za upuuzi.
NIPASHE
Unyonge na umaskini uliopo nchini kwa sasa umechangia kusababisha Watanzania wengi kuendelea kuonewa na kunyanyasika na wengi wao wakijazana magerezani kwa kukosa fedha za kuwahonga wenye mamlaka mbalimbali ili wasionewe.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara juzi katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
Lissu alisema unyonge ulioambatana na umaskini wa Watanzania, ndiyo unaowasababishia maumivu makubwa katika maisha yao na kufanya Taifa lililokosa mwelekeo.
Alisema mbali na kukabiliwa na unyonge huo, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliojaa magerezani ni wale maskini walioshindwa kutoa rushwa kwa askari polisi, wakuu wa vituo na mahakama pindi walipokamatwa kwa kutenda kosa au kusingiziwa.
Lissu alifafanua asilimia hiyo 80 ya waliopo gerezani ni wale ambao walishindwa kutoa rushwa kutokana na hali walizokuwa nazo za kukosa fedha ili kesi zao zifutwe na zisifikishwe mahakamani.
Hata hivyo, alisema chanzo cha hayo yote ni nchi kuongozwa na viongozi wasiojali maslahi ya wananchi.
Aliongeza kuwa nchi imebadilika na kuwa ya unyonyaji, uonevu na yenye kupuuzia mawazo na maamuzi ya Watanzania.
“Ninapozungumzia nchi imebadilika, namaanisha nchi inaongozwa na baadhi ya wanaoiba fedha za wananchi katika mbolea, pembejeo, dawa, karo za watoto wa Watanzania, barabara na maji… kwa hali hii tunataka mapinduzi ili tuondokane na haya,” alisisitiza.
NIPASHE
Serikali imelaumiwa kuwa imeshindwa kuweka mkazo katika kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kama inavyofanya kwa wanyama kama tembo hali inayosababisha mauaji ya watu hao kuendelea nchini.
Aidha, Serikali imelalamikiwa kwa kuzitengea fedha kidogo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Kazi na Ajira ambazo haziwezi kusaidia kutekeleza miradi ya maendeleo katika wizara hizo.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Omari Juma, alisema mauaji ya albino yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara hali inayozua maswali kwa wananchi kuhusu mahali Taifa linapopelekwa.
Juma aliitaka serikali iweke utaratibu wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi badala ya kuendelea kufanya uchunguzi kusaka wahalifu kila unapotokea uhalifu.
“Kila siku matukio ya albino kukatwa viungo na wengine kuuawa yanatokea, lakini hatuoni serikali ikichukua hatua kuwalinda, tembo wanalindwa sana na ikitokea ameuawa mmoja tu wahalifu wanasakwa, lakini albino akiuawa hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema.
Juma aliitaka serikali kufuatia wafanyakazi wa ndani ambao wamekuwa wakinyanyaswa na mama na baba mwenye nyumba kwa kulipwa ujira kidogo.
HABARILEO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ametangaza rasmi nia yake ya kuwania Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, akizungumza katika kipindi cha Nyumba ya Jirani kinachorushwa na televisheni ya taifa, TBC I juzi usiku, Membe alisema ataanika kila kitu akiwa kijijini kwao Rondo, Lindi Vijijini mkoani Lindi.
“Nitatangaza nia yangu kijijini kwetu nilikozaliwa. Kule ambako nilianza kupata mwanga wa elimu niliyonayo. “Kule nilikotokea hadi kwenda Usalama wa Taifa, kule nilikotokea na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hata safari nyingine (ya kuwania Urais), ni vyema ikawa na baraka za wazee kule ninakotoka, ndiyo maana nasema nakwenda kutangazia nia kijijini kwetu.”
Membe ni mmoja wa makada mashuhuri wanaotajwa kuwania Urais kwa tiketi ya CCM.
Wengine wanaotajwatajwa ni Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Steven Wassira, Lazaro Nyalandu, Profesa Mark Mwandosya na January Makamba waliomo katika Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete na William Ngeleja, aliyewahi kuwa waziri katika serikali ya Kikwete na Dk Hamisi Kigwangallah, Mbunge wa Jimbo la Nzega.
MTANZANIA
Mjadala wa Kikao cha 12 cha Bunge la Bajeti jana ulitawaliwa na vilio vya kamati za Bunge na wabunge kuhoji sababu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kupewa fedha kidogo ya maendeleo, huku Wizara ya Kazi na Ajira ikikosa kabisa fungu kutoka Hazina.
Wamesema hali hiyo inasababisha wizara hizo kutokuwa na jipya katika kuiendeleza nchi, ikiwa ni pamoja na kumaliza tatizo la ajira nchini.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira, mjumbe wa kamati hiyo Maua Daftali alisema katika bajeti ya mwaka 2014/15, wizara hiyo haikupewa hata shilingi moja ya fedha za maendeleo.
“Bajeti ya wizara hii mwaka 2014/15 ni Sh17 bilioni, kati ya hizo Sh5.8bilioni zilikuwa kwa ajili ya kulipa mishahara, Sh8.9 bilioni kwa ajili ya matumizi mengine na Sh2.9 bilioni kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa hadi Aprili mwaka huu, fedha za mishahara zilizotoka ni Sh4.7bilioni, matumizi mengine zilitoka ni Sh2.6 bilioni na hakukuwa na fedha yoyote ya bajeti ya maendeleo iliyotolewa.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.