MWANANCHI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema atakuwa bega kwa bega na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika mbio zake za kuwania urais.
Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza nia kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”, ameshasema siku ikifika atachukua fomu lakini anatarajia kutangaza rasmi mpango wake jimboni kwake Mtama, sasa anaungwa mkono na mmoja kati ya viongozi wa juu wa Serikali na CCM kutoka Zanzibar ambayo ina nafasi ya pekee katika kuamua mgombea urais wa chama hicho.
Balozi Iddi ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2006, alitoa msimamo huo wa kwanza kwa kiongozi wa juu wa Serikali jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyeshindwa kuhudhuria kutokana na msiba wa dada yake.
“Namtakia Membe safari njema na ninamuahidi kuwa tutakuwa naye bega kwa bega katika safari hii ngumu kwake,” alisema Balozi Idi bila ya kutaja neno urais.
Kauli ya makamu huyo wa Rais ilikuja baada ya Membe, ambaye amesema wakati ukifika atachukua fomu za kugombea urais, kuwaaga mabaozi hao kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa mabalozi hao, Membe aliweka wazi kuwa hatarudi tena bungeni akiwa waziri baada ya kuongoza wizara hiyo kwa takriban miaka minane.
Alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa mara kwa mara kuwa ameamua kuondoka wizarani hapo ili kujaribu nafasi kubwa zaidi katika siasa na kuwakaribisha bungeni mjini Dodoma ili wasikilize hotuba ya bajeti yake ya mwisho.
MWANANCHI
Bunge la Bajeti lililokuwa livunjwe Juni 27, mwaka huu litaongezwa siku 10 ili kutoa nafasi ya kujadiliwa kwa miswada takriban 10 kinyume na historia yake.
Mkutano huo wa 20 wa Bunge la 10 ni wa mwisho katika uhai wa chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuvunjwa, kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Ofisi ya Bunge na Rais Jakaya Kikwete, zilieleza kuwa tayari makubaliano yamefikiwa baina ya Bunge na Serikali ili kuwezeshwa kufikishwa miswada hiyo katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), juzi usiku, Rais Kikwete alisema makubaliano hayo yamekwishafanyika na miswada itakayojadiliwa mmojawapo ni wa kuanzishwa tume ya utumishi ya walimu, ambayo inawezesha walimu nchini kuwa na chombo kimoja cha kuwasimamia.
“Tayari tumezungumza na Spika wa Bunge na tumekubaliana katika kikao kinachoendelea kitaongezwa siku 10 ili kuwezesha kumaliza shughuli za serikali ikiwamo miswada,”.
Chanzo kingine cha habari ndani ya Serikali kilieleza kuwa moja kati ya miswada itakayowasilishwa na Serikali ni pamoja na marekebisho ya sheria ya uchaguzi pamoja na muswada wa sheria ya vyombo vya habari.
Sababu nyingine inayotajwa kuhusu kuongezwa muda kwa Bunge hilo ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, ambao utafanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11 hadi 12.
Wabunge wote wa CCM ni wajumbe wa mkutano huo, hivyo kama Bunge litavunjwa Juni 27, 2015 watapoteza sifa za kuwa wajumbe wa mkutano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu chama hicho tawala kuhusishwa na nyongeza ya siku za Bunge hilo alisema, “Huo ni upuuzi mwingine sasa. Vikao vya CCM vimepanga ratiba kabla hata ya huo uamuzi wa Bunge unaousema. Hakuna ukweli katika hilo.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alipoulizwa kuhusu suala hilo alishindwa kukubali wala kukataa na kutaka atafutwe Katibu wa Bunge.
Tayari Chama cha Wamiliki wa vyombo vya Habari Tanzania (Moat), kimeunda timu maalumu itakayokwenda bungeni kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa sheria wa vyombo vya habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali ulitakiwa kuwasilishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge kwa hati ya dharura bila mafanikio na tayari Rais Kikwete amesema atausaini kabla hajaondoka madarakani.
Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa alisema: “Hilo jambo bado hatujakaa katika kamati ya uongozi kulijadili vizuri. Bado hatujajua Serikali inaleta miswada gani. Ila pamoja na hayo, hicho kitu (kuongeza muda) kitakuwapo.”
NIPASHE
Wabunge wameishukia serikali kwa kushindwa kutatua tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam ambalo sasa linaigharimu serikali hasara ya Sh. bilioni nne kila siku.
Aidha, wameitupia lawama Wizara ya Ujenzi kwa kusababisha vifo vya makandarasi wanne ambao walifikwa na umauti huo kutokana na serikali kushindwa kuwalipa madeni wanayodai.
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia, akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2015/2016, alisema tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam limekuwa sugu bila kuwapo mipango yoyote ya serikali katika kulipatia ufumbuzi.
Alisema Januari 13, mwaka 2009, alimwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu tatizo la msongamano wa magari na kutoa mapendekezo 10 ambayo yangesaidia kukabiliana na tatizo hilo, lakini bahati mbaya hakuna kilichofanyika hadi sasa hali inayoonyesha serikali kutokuwa makini katika kushughulikia mambo ya msingi.
Mbatia alisema moja ya mapendekezo hayo ni kuitaka serikali isimamishe au kutoendelea kutoa vibali vya kujenga ofisi, maduka makubwa na madogo katikati ya Jiji.
Alisema pendekezo lingine lilikuwa ni kutaka Ofisi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ujenzi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Makao Mkuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na uwanja ndege vihamishwe katikati ya Jiji.
“Hali ni mbaya Dar es Salaam, watu wanakaa kwenye foleni kwa zaidi ya saa nane, foleni hii inaigharimu serikali zaidi ya Sh. bilioni nne kwa siku ambazo zingetumika kujenga zahanati na kununua madawati ambayo yangesaidia watoto shuleni,” alisema.
Alisema Sh. bilioni nne ambazo serikali inapata hasara kila siku kutokana na foleni zingetumika kununua madawati 80,000 kwa bei ya Sh. 50,000 kwa dawati moja.
Mbatia alisema pia fedha hizo zingetumika kujenga vituo viwili vya afya vya kisasa, ambavyo gharama zake kila kimoja ni Sh. bilioni mbili.
NIPASHE
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Wizara ya Ujenzi kutoa majibu ya deni la zaidi ya Sh. bilioni 800 inayodaiwa wizara hiyo na makandarasi katika bajeti ya mwaka 2014/2015.
Akiwasilisa hotuba ya Kambi hiyo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Felix Mkosamali, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, wizara hiyo ilitengewa Sh. 662,234,027,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Januari 2014, madeni ya makandarasi na washauri yalikuwa Sh. 663,870,636.26.
Alisema mfano mzuri ni bajeti 2014/2015 wizara ilikuwa na madeni yaliyofikia Sh. bilioni 760 huku bajeti ya maendeleo kwa wizara na taasisi zake ikiwa ni Sh. bilioni 762.
“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inamtaka waziri kueleza ukweli Bunge lako tukufu kwamba kwenye bajeti ya 2014/2015 ni fedha kiasi gani zimelipa madeni na fedha kiasi gani zimekwenda kwenye miradi ya maendeleo,” alisema.
Mkosamali alisema hata kwa mwaka huu wa fedha, Bajeti ya Maendeleo ni Sh. 890,572,000.00 kwa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara huku madeni yakiwa zaidi ya Sh. bilioni 800. “Hakuna uhalisia kati ya fedha za maendeleo zinazoombwa na madeni husika.”
Alisema wizara hiyo imekuwa kiandika hotuba ndefu kuwachanganya wabunge kwa kuonyesha barabara zilizojengwa miaka ya 80 na miaka 90 kama vile zimejengwa hivi karibuni.
Alisema wizara haijatoa ufafanuzi unaoridhisha juu ya fedha zinazotengwa na kilomita zinazojengwa, mfano wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro (kilomita 200), sehemu ya Dar es Salaam Chalinze imetengewa Sh. bilioni 2.45. “Hakuna ufafanuzi kwani kilomita 100 haziwezi kujengwa kwa Sh. bilioni mbili tu.”
Kambi hiyo ilisema licha ya mbwembwe nyingi za waziri, madaraja yaliyoahidiwa kujengwa mwaka 2014/15 likiwamo la mto Sibiti lililotengewa Sh. bilioni tatu, lakini fedha hizo hazijatolewa na Hazina na mkandarasi ameondoka eneo la ujenzi na Daraja la Kigamboni ambalo liliahidiwa kukamilika mwezi Juni, mwaka huu, ambalo linaonyesha ahadi haitatekelezeka.
Kambi hiyo ilisema licha ya wizara na hata Waziri Mkuu kujigamba kujenga kilomita 13,000 za lami katika awamu ya nne, zimejengwa chini ya kiwango na zinabomoka na kuharibika miezi sita au pungufu au mwaka mmoja baada ya matengenezo.
Alitoa mifano hiyo kuwa ni Dar es Salaam – Dodoma ambayo imebonyea upande wa kushoto na inatengenezwa kila wakati, lakini inaharibika, Bagamoyo – Msata, ambayo imeanza kuharibika kabla haijamalizika, Dodoma – Iringa, imejaa mashimo maeneo kadhaa na Dodoma – Mwanza hasa maeneo ya m lima wa Sekenke iliyobomoka muda mfupi mara tu ya kukabidhiwa serikalini.
Kambi hiyo ilikiponda kivuko hicho chenye kubeba abiria 300 kwa karibu Sh. bilioni nane, lakini kinatumia saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo.
“Ni jambo la ajabu kununua kivuko cha kizamani chenye spidi ndogo. Azam Bakhresa ana meli inayotoka Dar kwenda Zanzibar kwa muda wa dakika 90 tu na kinabeba abiria 500, ambacho kwa taarifa tulizonazo kimenunuliwa kwa kati ya Sh. bilioni nne hadi tano tu,” alisema.
Kambi hiyo ilisema inaamini juu ya ujenzi wa barabara zipitazo juu ili kuepusha kero kwenye maeneo ya Tazara, Moroco, Ubungo, Magomeni, Selander bridge na maeneo mengine yenye msongamano.
Hata hivyo, ilisema serikali haina nia ya dhati ya kuonyesha msongamano huo kwa kujenga angalau barabara moja inayopita juu.
Mkosamali alisema licha ya mbwembwe za uwasilishaji wa waziri wa bajeti hiyo, kila inapofikia mwaka wa uchaguzi, serikali imekuwa ikiahidi kujenga barabara kwa lengo la kupata kura, lakini haitimizi ujenzi wa barabara hizo.
Alitaja barabara hizo kuwa ni ya Nyakanazi, Kibondo, Kasulu, Kidahwe zenye urefu wa kilomita 310 ambayo ilikuwa ahadi ya Serikaliya awamu ya tatu na awamu ya nne.
MTANZANIA
Hali ya njaa imeikumba Burundi hasa katika mji mkuu wa Bujumbura baada ya wasafirishaji wa mazao kusimamisha huduma yao kuhofia usalama wao.
Kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa ikihaha kuwaomba wananchi hasa waliokimbia wa mikoa ya milimani ya Makamba na Ngozi kurejea nchini humo waendelee na kilimo.
Mkazi wa Bujumbura ambaye jina lake linahitafadhiwa kwa sababu za usalama, alisema kwa wiki moja sasa huduma muhimu za vyakula zimekuwa adimu nchini humo.
“Hali imekuwa ni mbaya na sasa nchi inakabiliwa na njaa na hatujui la kufanya, fedha zipo lakini bidhaa hakuna hasa chakula, yakiwamo mahindi na mchele.
“Awali tulikuwa tukipata chakula bila tatizo nchi ilipokuwa imetulia lakini tangu yalipoingia machafuko ya kupinga hatua ya Nkurunziza (Pierre, Rais) kuwania urais kwa muhula wa tatu, tunaoana nchi ilipofika sasa,” alisema mkazi huyo wa Bujumbura.
Juzi, Rais Nkurunziza alifanya ziara ya kushtukiza katika mpaka wa Kagunga nchini Tanzania na Burundi na kuwataka warundi wasiikimbie nchi yao akisema kwa sasa ina amani.
Pia aliwataka wananchi kuchangia gharama za kuendesha uchaguzi wa nchi hiyo baada ya wahisani kusimamisha misaada yao kwa Burundi.
Nchi hiyo imekumbwa na machafuko kwa wiki kadhaa sasa ambako waandamanaji wakiwa wakipambana na polisi wakipinga hatua ya Nkurunziza kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Wanasema kitendo hicho ni kukiuka katika ya nchi hiyo inayotamka mtu atagombea urais kwa vipindi viwili tu.
Lakini Nkurunziza na chama chake cha CNDD-FDD amekuwa akidai kwamba hicho kitakuwa kipindi chake cha pili kuchaguliwa na wananchi kwa sababu katika muhula wa kwanza alichanguliwa na Bunge.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema atahakikisha anamaliza matatizo yote yanayowakabili walimu kote nchini katika kipindi kilichobaki cha utawala wake.
Alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na walimu wapatao 1,500 kutoka wilaya 153 na mikoa yote ya Tanzania Bara, pamoja na wawakilishi kutoka Visiwani.
Akizungumza kwa hisia kali katika eneo la Ngurdoto wilayani Arumeru mkoani hapa katika Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Walimu (CWT), Rais Kikwete alisisitiza kuwa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza, kinaendelea kujali maslahi ya walimu kama watumishi muhimu zaidi katika Taifa.
Alisema kwamba kilio chao ni cha umma na ni wajibu wa viongozi wote kutilia maanani. “Nimeyasikia matatizo yenu kupitia risala maalumu, na mengi tulikwishaanza kuyafanyia kazi.
Nawaahidi kutatua matatizo yenu kabla sijaondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na hata kama nitastaafu hapo baadaye, mengine yaliyosalia yataendelea kutatuliwa na viongozi wa serikali ijayo nami binafsi nitaacha maagizo hayo,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete aliyeingia madarakani mwaka 2005, anatarajiwa kumaliza muda wake wa uongozi Oktoba mwaka huu, baada ya kuitumikia nchi katika awamu mbili za miaka mitano mitano.
Kikwete pia aliwashauri walimu kuunda chombo kimoja, kitakachowasajili na kuwawakilisha kama Bodi, badala ya hali iliyopo sasa, ambapo kuna utitiri wa vyombo vinavyowawakilisha kiasi cha kusababisha usumbufu wakati mwingine.
Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Taifa (CWT), Yahaya Msulwa alisoma risala ya walimu iliyomuomba Rais Kikwete awatatulie matatizo yao kadhaa kabla hajaondoka rasmi madarakani, kwani mengi ni yale yaliyodumu muda mrefu.
Miongoni mwa madai ya walimu ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, posho, malipo ya uhamisho, ucheleweshwaji wa barua za ajira na likizo, na pia maombi yao ya kulipwa posho za muda wa ziada wanaolazimika kuwa kazini.
Wawakilishi kutoka nchi sita pia wako hapa kuhudhuria mkutano huo ambazo ni Uganda, Kenya, Denmark, Rwanda na Ghana, ambapo pia viongozi wastaafu wa CWT taifa na wale wa kutoka visiwa vya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch alisema chama hicho kimekuwa kikipata ushirikiano mzuri kutoka Serikali ya Awamu ya Nne, na kwamba wanatarajia uhusiano huo mzuri kuendelea hata katika serikali ijayo ya Awamu ya Tano.
Malengo ya mkutano mkuu wa taifa wa CWT ni pamoja na kujadili taarifa za kazi ya chama na taarifa za mapato na matumizi na kupitia mpango mkakati wa miaka mitano 2015-2020.
Uchaguzi mkuu CWT Mkutano mkuu wa CWT leo unatarajiwa kukamilishwa kwa uchaguzi mkuu, ambao umevutia wagombea 28 wa nafasi ya urais wa chama hicho chenye nguvu, kutokana na kuundwa na idadi kubwa ya watumishi wa umma.
Miongoni mwa wagombea hao ni Rais wa sasa wa chama hicho, Gratian Mukoba ambaye pia Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA).
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli hiyo ya Ngurdoto, huku wajumbe wa mkutano huo na jamii ya walimu kote nchini ikisubiri kwa hamu matokeo.
HABARILEO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeachiwa jukumu la kuamua siku ya kufanyika Uchaguzi Mkuu baada ya wabunge kutaka uchaguzi usiwe unafanyika katika siku za kuabudu ambazo ni Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Mbali ya Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama (CCM), kuhoji katika swali lake la msingi, lakini wabunge wengi walisimama kutaka kuuliza maswali ya nyongeza kuhusu siku hiyo ya kufanyika Uchaguzi Mkuu.
Katika swali lake, Mshama alihoji ni lini Serikali itaacha kutumia siku ya Jumapili kwa ajili ya uchaguzi (kupiga kura) ili watu wa madhehebu ya Kikristo wapate muda wa kushiriki ibada kikamilifu.
Pia alihoji Serikali inapoteza kitu gani, kama itapanga upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu kufanyika siku za kawaida za kazi. Kwa kawaida, Tanzania hupiga kura siku ya Jumapili katika chaguzi zake mbalimbali na mwaka huu, Uchaguzi Mkuu umepangwa kuwa Jumapili ya Oktoba 25.
Katika maswali yao ya nyongeza, Mshama na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), walitoa mifano ya nchi zilizofanya uchaguzi wao katika siku za kawaida, wakizitaja Malawi, Kenya, Uganda na India.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama alisema suala hilo ni la Kikatiba na kuwa NEC ndiyo yenye jukumu la kuamua kama inaweza kubadili tarehe hizo.
“Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake yaliyoainishwa katika Ibara hii, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni Taasisi huru inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao na Mtendaji Mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa Mujibu wa Masharti ya Sheria iliyotungwa na Bunge.”
“Hivyo, Tume ya Uchaguzi kwa mamlaka haya iliyopewa Kikatiba inaweza kufanyia kazi ushauri huo kwa kuzingatia wakati, hali halisi na mazingira yaliyopo kwa wakati husika,” Mhagama.
Hili litawezesha kufanyika uchaguzi kwa amani kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.”
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.