Makada watatu wa CCM jana walijitokeza katika makao makuu yake mjini hapa kuchukua fomu kuomba kupewa ridhaa na chama hicho ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waliochukua fomu jana ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kada wa chama hicho, Leonce Mulenda na Ofisa Mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Peter Nyalali na kufanya idadi ya wanaCCM waliokwisha fanya hivyo kufikia 18.
Nyalandu ambaye alisindikizwa na wabunge wa viti maalumu, Mary Chatanda na Martha Mlata alisema amechukua fomu akifahamu umuhimu wa kuyaendeleza yote yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne… “Ninafahamu changamoto zinazotukabili. Nazitazama, naziona hatua ambazo zipo tangu wakati wa Baba wa Taifa alipomkabidhi kijiti Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete.”
Alisema anafahamu changamoto zinazolikabili Taifa na anaitazama nchi iendelee kulinda misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa kwa kuendeleza amani.
Alisema umoja, undugu na mshikamano atakaoulinda, utaifanya Tanzania iwe na nguvu ya kutatua changamoto za sasa na za kesho.
Huku akipigiwa makofi na wapambe wake, Nyalandu alisema waliambiwa zamani kuwa wazee wanaotawala vyema wanastahili heshima maradufu.
“Tutaendelea kuwaenzi wazee waliotutawala, wamekuwa wakitulea katika miji na vijijini, tutaendelea kuwaangalia vijana na wanawake kwa kuangalia nini ambacho tumefanikiwa katika awamu hii ya Rais Kikwete. Tutaangalia mageuzi tutakayoyafanya ili kijana wa Kitanzania aonekane si mzigo,” alisema.
Alisema endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo, serikali yake itajikita katika kuinua uchumi wa nchi.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, ametangaza rasmi nia ya kuutaka urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2015 akisema anatosha na kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko aliko atafurahi endapo atakuwa rais.
Membe aliyasema hayo jana kwenye Viwanja vya Ofisi ya CCM Mkoa wa Lindi katika hotuba yake ya saa moja kutangaza nia yake hiyo huku kwa kujiamini kabisa akisema kuwa yeye ndiye Rais wa Tanzania kwa miaka 10 ijayo.
Alisema katika urais wake, ataboresha elimu, ataweka msisitizo katika utawala bora, maendeleo ya jamii, uchumi na masuala mbalimbali ya kisiasa na kidiplomasia.
Huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliofika kumsikiliza, alisema amejipima na kuona anaweza.
“Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.
“Sikukurupuka, zipo nafasi za kukurupuka na wapo wanaokurupuka, lakini si vyema kukurupuka kwa nafasi ya urais,” alisema.
Membe aliyesindikizwa na mkewe Dorcas, alisema Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu na kupiga goti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
“Nilipiga goti nikamwambia Mwalimu, navitaka viatu vyako, alivivaa Mzee Mwinyi (Ali Hassan), Mzee Mkapa (Benjamin) na Kikwete (Jakaya), sasa nataka kuvaa mimi na nina hakika vinanitosha.
“Ninaamini vitanitosha. Nikamwambia chondechonde, kama havitanitosha, niambie… timu yangu ya mikoani ikawahi kuniambia unatosha,Membe.
Alisema alialikwa na Mzee Mwinyi katika ‘birthday’ yake ya miaka 91 na kati ya mambo aliyomwambia ni kwamba ameongoza nafasi mbalimbali, lakini hakuwahi kununua uongozi.
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba jana alitangaza nia kwa mara nyingine ya kuwania urais akiahidi serikali yake kuunda baraza la mawaziri wasiozidi 18 wasiotiliwa shaka na wananchi juu ya uwezo na uadilifu wao.
Makamba ambaye alishatangaza nia hiyo mwaka jana akiwa London, Uingereza alisema ametafakari kwa kina kuhusu changamoto zinazoikabili nchi na aina mpya ya uongozi inayohitajika na kuamua kuomba ridhaa ya urais ili azitatue.
Mwanasiasa huyo aliwaambia wananchi waliojitokeza kumsikiliza kuwa kesho atakwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuomba ridhaa hiyo na kuongeza kuwa; “sijagombea kugombana na watu, nimegombea kupambana na changamoto za watu. Naiomba nafasi huku nikielewa kiu ya Watanzania kupata aina mpya ya uongozi wa zama za sasa utakaotoa matumaini mapya yatakayozaa Tanzania mpya. Naelewa misingi iliyojenga nchi yetu ya haki, umoja, amani na upendo na mshikamano… inayotakiwa kulindwa kwa gharama zote.”
Alisema aina ya uongozi wa utakaochaguliwa Oktoba ndiyo utakaoamua mustakabali wa nchi na majawabu mapya yatakayomtofautisha yeye na wengine.
Makamba ambaye aliyohutubia kwa takribani saa 1.17, alisema atainadi ilani ya CCM kwa nguvu zote na serikali atakayounda itaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
“Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu… nitaunda serikali ya mawaziri 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake,” alisema Makamba huku akishangiliwa.
Alisema serikali yake itakuja na vipaumbele vitano vya kukuza vipato vya watu kwa shughuli zote, huduma bora na za uhakika za kijamii; utawala bora, haki, utawala wa sheria, usimamizi wa uchumi na kulinda amani, umoja na usalama wa nchi.
Makamba alieleza namna atakavyotekeleza vipaumbele vyake kama alivyokwisha eleza katika mahojiano yake yaliyomo katika kitabu cha Padri Privatus Karugendo kiitwacho Maswali na Majibu 40 juu ya Tanzania Mpya.
Kuhusu ukuzaji wa uchumi, mbunge huyo wa Bumbuli alisema ataunda baraza la uchumi litakalojumuisha wataalamu kutoka taasisi za umma, magwiji wa uchumi na wawakilishi wa sekta binafsi, litakalohakikisha uchumi unawekewa mipango ya muda mfupi na mrefu kutatua changamoto zinazoikabili nchi.
Alisema pia ataziboresha taasisi za kifedha, tume ya mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kudhibiti matatizo yanayoikabili nchi ukiwamo mfumo wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.
Katika mipango yake ya kulinda amani na umoja alisema ataanzisha jukwaa maalumu litakalojumuisha Baraza za Maaskofu Tanzania (TEC) Jumuiya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) litakalokuwa linakutana na rais kila baada ya miezi miwili kujadili namna ya kuimarisha umoja, amani na upendo nchini.
Alitaja mambo mengine atakayoyatekeleza kwa kuyaita majawabu mapya kuwa ni kutatua tatizo la ajira, rushwa, miundombinu, elimu, maji na umeme.
MTANZANIA
Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, imeitaka Serikali kulieleza Bunge matumizi ya zaidi ya Sh trilioni 1.5 ambazo hazina maelezo kutoka Hazina ingawa zinaonekana zimetumika kulipa sehemu ya deni la taifa. Deni a Taifa limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh trilioni 40 kwa miaka miwili.
Akiwasilisha maoni ya kamati yake kwa mwaka 2015/2016, mwenyekiti wake, Luhaga Mpina alisema kwa mujibu wa vielelezo vilivyotolewa mbele ya kamati, zilionyesha katika kipindi cha Julai 2014 hadi Machi 2015 fedha zilizokuwa zimelipiwa deni la taifa ni Sh trilioni 2.636 tu.
Alisema taarifa ya utoaji fedha inaonyesha fedha zilizokuwa zimetolewa katika kipindi hicho ni Sh trilioni 4.123 ikiwa ni tofauti ya Sh trilioni 1.5.
“Kamati inaitaka Serikali kulieleza Bunge kiasi hiki cha fedha Sh trilioni 1.5 kililipwa wapi na kwa kazi gani na kama fedha hizo ziliidhinishwa na Bunge,” Mpina.
Aidha kamati pia ilihoji taarifa ya Waziri wa Fedha kuamua kufuta mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo ambao ulipaswa kutekelezwa takribani miaka saba iliyopita, huku watendaji katika wizara nyingine mtambuka wakiwa hawana taarifa.
Mpina alisema mradi huo kiuhalisia una tija kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa Singida, lakini umekuwa ukipigwa danadana na kikwazo kikubwa ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Mwenyekiti huyo alisema mradi huo wa umeme wa upepo ulikubaliwa kupata mkopo katika Benki ya Exim ya China tangu Februari 2014 kwa thamani ya dola za Marekani 136, lakini hadi leo wizara kupitia Hazina imeshindwa kukamilisha mchakato wa mkopo huo licha ya maelekezo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kuhusu deni la taifa, Mpina alisema hadi kufikia Machi 31, mwaka huu limefikia zaidi ya Sh trilioni 35 ikilinganishwa na deni la mwaka 2013/14 ambalo lilikuwa Sh trilioni 30.
Katika deni hilo, zaidi ya Sh trilioni 26 sawa na asilimia 73.75 ni deni la nje na deni la ndani likiwa ni zaidi ya Sh trilioni 9 sawa na asilimia 26.25.
MTANZANIA
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla, ametangaza rasmi nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akitaja vipaumbele vikuu vitatu ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya.
Kigwangalla ambaye alitangaza nia yake hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Nzega mkoani Tabora, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwani ana dhamira njema, hofu ya Mungu na anachukia rushwa.
Alisema Tanzania ya sasa inahitaji kuongozwa na vijana ambao wana fikra mpya ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi na sio watu ambao wameongoza kwa kipindi kirefu.
Alisema vipaumbele vyake ni kuondoa umaskini, kutoa huduma bora kwa jamii na kudumisha utawala bora.
Dk. Kigwangalla alisema akichaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano, atahakikisha nchi inakuwa na rasilimali za kutosha na kuondokana na utegemezi.
Alisema Serikali atakayoiongoza akipewa ridhaa, haitategemea hata Sh 1 kutoka kwa wahisani na kwamba atahakikisha kila mtu anakuwa na bima ya afya.
Dk. Kigwangalla alisema ili kuhakikisha uchumi unakua kwa kiwango kinachostahili, asilimia 5 ya bajeti itapelekwa kwa wanasayansi kwa ajili ya utafiti.
Alisema atahakikisha anaanzisha mfuko wa kukopesha wafanyabiashara wadogo ili kukuza uchumi wa nchi na taifa kwa ujumla kwani Tanzania ina uwezo wa kujenga matajiri wa ndani ya nchi.
Dk. Kigwangalla anayetumia kaulimbiu ya ‘Fikiri tofauti, amua mabadiliko sasa’, alisema Serikali ina uwezo wa kukusanya bilioni 20 kila mwaka kutokana na utawala bora.
“Natamani kuijenga Tanzania ambayo wabunge watapeleka watoto wao kusomea katika shule za kata na sio kama ilivyo sasa ambapo wanawapeleka kwenye shule za watu binafsi,” .
Pia alisema Watanzania waishio vijijini wanahitaji kujengewa mazingira mazuri kwani wengi wao wanategemea sekta ya kilimo.
Alisema endapo atapata ridhaa hiyo atahakikisha anadhibiti urasimu na kuweka uwajibikaji ili kuwa na mfumo mzuri wa uongozi.
MTANZANIA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameingia visiwani Zanzibar na kupokewa kwa maandamano makubwa ya wana CCM.
Lowassa aliwasili Zanzibar juzi akitokea jijini Mwanza, ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini wa kumdhamini ili agombee urais kupitia CCM.
Lowassa na ujumble wake waliingia Zanzibar kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume saa 1:30 jioni, ambapo alipokewa kwa shangwe na wana CCM, vikundi vya ngoma, waendesha pikipiki na magari na kuelekea mjini.
Jana alitembelea ofisi ya makao makuu ya CCM ya Kisiwandui na kupokewa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini, Borafya Silima, ambapo alitia saini kitabu cha wageni kisha akaelekea kwenye kaburi la hayati Abeid Karume lililopo karibu na ofisi hiyo.
Alitembelea pia ofisi ya CCM Mkoa wa Mjini alikopewa saini za wanachama 90 katika wilaya za Mjini na Amani.
Lowassa aliwataka wanachama kuchagua mgombea anayefaa kuwa mwenyekiti wa chama, huku pia akisisitiza kuyaenzi mapinduzi ya Zanzibar.
“La kwanza nawashukuru kwa kunidhamini na ninaahidi kutowaangusha. Unapochagua rais, unachagua pia mwenyekiti wa CCM, unapochagua Rais wa Zanzibar unachagua makamu mwenyekiti wa chama. Tutafute mtu anayekijua chama, maana kuna watu wamechupia tu.
“Nathamini Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano. Kuna watu wanabeza Muungano, mimi ninaahidi kuulinda.”
Lowassa alisema lengo la kugombea urais ni kutetea sera ya CCM ya kupambana na umasikini.
“Nimeamua kugombea urais ili nipambane na umasikini, nachukia umasikini. Nimekuwa mwanachama wa CCM kwa karibu nusu ya umri wangu. Nataka kutekeleza sera ya CCM ya kupambana na umasikini,” .
Lowassa alitembelea mikoa ya Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini na Mkoa wa Kusini ambako kote alipata saini 360 za wana CCM.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, mgombea anatakiwa kukusanya saini ya saini 450 kutoka mikoa 15 ambapo kati yao mitatu inatoka Zanzibar.
NIPASHE
Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotafuta dhamana ya chama hicho ili wawanie nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano, watachuana kwenye mdahalo ulioandaliwa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi (CEOrt).
Hata hivyo, pamoja na kwamba Lowassa alialikwa kushiriki mdahalo huo ambao umepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam leo hatoshiriki kwa kuwa yupo kwenye ziara ya kutafuta wadhamini wa chama ili aweze kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Umoja huo, Ali Mufuruki, ilieleza kuwa makada hao watapata fursa ya kueleza vipaumbele vyao kwa taifa.
Mufuruki aliwataja watakaochuana katika awamu hii ya kwanza ya mdahalo kuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Balozi Amina Salum Ali na Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Wengine ni Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
“CEORT tunayo furaha kuwa mwenyeji wa mdahalo wa kwanza na wa aina yake wa wagombea urais katika historia ya Tanzania. Uchumi utakuwa kiini cha mjadala mwaka huu na siyo haiba wala rangi ya chama…kwa masikitiko Edward Lowassa amekataa,” alisema Mufuruki katika taarifa hiyo.
Hata hivyo, alisema midahalo miwili zaidi itafuata ambayo itawajumuisha wagombea urais wa vyama vya upinzani na wale wa CCM.
Wagombea ambao wamekwishatangaza kuwania nafasi hiyo kupitia CCM na wengine kuchukua fomu ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Wengine ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Balozi Ali Abeid Karume na Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere.
Mbali ya vigogo hao sita, pia yupo kada mwingine wa chama hicho, Amosi Siyatemi, anayelezwa kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Aidha, hadi jana, makada ambao wameshachukua fomu kuwania nafasi hiyo ni 18.
NIPASHE
Tanzania inaongoza kwa kuuza bidhaa nyingi kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kulinganisha na nchi zingine za wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha, imeelezwa kuwa kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara wadogo kutoka Tanzania wanaoshindwa kuuza bidhaa zao katika EAC kutokana na kutokujua vigezo na masharti katika soko hilo.
Hayo yalielezwa na mtaalamu wa masuala ya kibiashara kutoka taasisi ya Diligent Consultant, Rebeca Muna wakati wa mafunzo kwa wafanyabiashara wadogo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (Tango).
Muna alisema kuna changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wadogo wa Tanzania kuingia katika soko la kibiashara la Afrika Mashariki.
Alisema sababu kubwa ya kuwapo kwa hali hiyo ni wafanyabiashara hao kutojua masharti na vigezo vya kuuza bidhaa zao, pamoja na kutokujua ushindani wa soko.
“Mafunzo haya yatawasaidia kujua fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ijapokuwa Tanzania inaonekana kuongoza katika soko la biashara,” alisema Muna, akiongeza kuwa Tanzania inafuatiwa na Kenya lakini bila kufafanua nafasi za nchi nyingine kwa mfuatano.
Mbali na Tanzania na Kenya, nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Uganda, Rwanda na Burundi.
Kadhalika, Muna alisema licha ya Tanzania kuongoza kwenye soko Afrika Mashariki, lakini wanaonufaika zaidi ni wafanyabiashara wakubwa.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Kilimanjaro, Rose Swai, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kutofautisha na kujua vikwazo vya kisera katika biashara vilivyopo kwenye eneo la Afrika Mashariki.
“Tutajua jinsi ya kuuza bidhaa zetu, ushuru wa mipakani, namna ya kuboresha bidhaa zetu na pia kujua ni kwa namna gani ziingie katika ushindani kwenye soko la Afrika Mashariki,” Swai.
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Abdulrahman Kinana, amewahakikishia wananchi wa Kanda ya Ziwa kuwa meli zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2010 zitafika nchini Septemba mwaka huu kutokea nchini Sweden.
Kinana aliwahakikishia pia wananchi wa maeneo mengine nchini wakati akiwa Bukoba jana kuwa, meli hizo zitakuwa tatu na zitapelekwa katika maziwa makuu matatu nchini ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Katibu huyo wa CCM ambaye hivi sasa yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku 10, alisema, serikali ya Rais Kikwete bado inakumbuka ahadi ya kununua meli mpya kwa ajili ya maziwa hayo makubwa zaidi nchini.
“Wananchi wasidhani kuwa ahadi hiyo ilikuwa hewa. Tayari meli hizo zimeshaanza kutengenezwa nchini Sweden na kuanzia Septemba vipuri vyake vitaanza kuwasili tayari kwa ajili ya kuunganishwa… na baada ya miezi mitatu, zitakuwa zimekamilika na kuanza kutumika..Kazi ya CCM ni kutenda, kazi ya wapinzani ni kusema. Tuliahidi, tutatekeleza,” Kinana.
Kinana alifafanua zaidi kuwa awali, kuna nchi mbili ambazo zilikubali kutengeneza meli hizo, Sweden wakikubali kutengeneza meli mbili ambazo ni kwa ajilli ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika na Korea Kusini wakitengeneza meli itakayopelekwa Ziwa Nyasa.
NIPASHE
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imehoji serikali kutochukua hatua madhubuti na za kuridhisha katika kukabiliana na kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania na pia upotevu wa mapato utokanao na misamaha ya kodi.
Imesema kwa mujibu wa tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ya Oktoba 1, 2014, dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa Sh. 1,674 lakini hadi kufikia Juni 5, 2015, dola hiyo imeuzwa kwa Sh. 2,054 za Tanzania, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.
Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo kuhusiana na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Fedha, James Mbatia, alisema thamani ya Shilingi ya Tanzania inaendelea kudhoofika kulinganisha na fedha za nchi nyingine zikiwamo nchi jirani kama Kenya, Rwanda na Burundi.
“Tunaomba serikali ituambie, je, imeshindwa kutafuta vyanzo vya mapato au kusimamia vyanzo vilivyopo kiasi kwamba imeamua kutegemea hali hii mbaya kiuchumi ili kuongeza mapato yake? Je, serikali ikituhumiwa kuwa imeporomosha shilingi kwa makusudi ili ikusanye mapato bila kuangalia athari zingine inaweza kukwepa tuhuma hizi?” Alihoji.
Alisema imeoneshwa kwamba thamani ya shilingi dhidi ya Paundi ya Uingereza imeshuka kwa asilimia 13 kwa kutumia takwimu za Benki Kuu na asilimia 24 kwa kutumia takwimu za kisoko dhidi ya Euro, ikiwa ni anguko la asilimia 8.
“Inasikitisha kuona hata nchi ya Burundi, ijapokuwa ipo kwenye misukosuko mingi lakini bado shilingi yetu imeanguka dhidi ya faranga yao kwa asilimia 20…hii ni aibu na fedheha kubwa,” Mbatia.
Alisema athari za kushuka kwa shilingi ni wawekezaji kushindwa kuwekeza nchini kwa kuwa wengi hawapendi mazingira yasiyotabirika na athari nyingine ni kushuka ghafla kwa pato la taifa kutokana na kutegemea bidhaa zinazoagizwa nje.
Mbatia alisema baadhi ya wastaafu wanalipwa fedha kidogo ambazo hazilingani na gharama za maisha ya sasa na kutoa mfano kuwa wapo wazee wanaolipwa Sh. 50,000 tu kwa mwezi.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.