MWANANCHI
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA) ameanza kuonja joto la kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya watu wanane kujitokeza kwa siku ya kwanza kuitaka nafasi hiyo.
Kati ya waliojitokeza kuwania ubunge kupitia CCM ni mtoto wa waziri mkuu wa zamani Joseph Warioba, Kipi Warioba na Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jumaa Mhina ‘Pijei’.
Pia yumo Elias Nawela, Dk Walter Nnko, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Shuganga George na Edmund Lyatuu.
Mdee amekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema tangu mwaka 2010, lakini sasa atakuwa na kazi ya kupambana na baadhi ya makada hao wa CCM waliochukua fomu kulitaka jimbo hilo.
Wengine katika maeneo mbalimbali nchini waliochukua fomu ni pamoja na Moshi Mjini ambako makada wa CCM wameanza kupigana vikumbo kutaka kumrithi mbunge wake wa sasa, Philemon Ndesamburo.
Kada wa kwanza aliyechukua fomu ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Mwita na wafanyabiashara, Davis Mosha na Patrick Boisafi.
Mjini Mbeya, Mwenyekiti wa UVCCM, Amani Kajuna ameibuka na kutaka kuwania ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.
Katika Jimbo la Kinondoni Idd Azzan anayetetea jimbo lake anatarajiwa kuchuana na Wangota Salum, John Kalinjana na Goochange Msangi wakati Ubungo Didas Masaburi na Joseph Massana wamejitokeza kumvaa John Mnyika.
Katika Jimbo la Kibamba waliojitokeza ni George Shija, Dk Meshack Sabaya, Dk Fenella Mukangara na Rashid Kikazi.
Wanaowania kupitia viti maalumu Kawe ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki, Zarina Madabida, Getrude Lwakatare, Florence Masonga, Mary Daffa, Warda Maulid, Anna Matulu, Emelda Mwananga, Maria Kigalu, Angela Kizigha na Ummy Nderiananga.
Mkoani Dodoma, mbunge anayemaliza muda wake, David Malole na anayemiliki Kiwanda cha Magodoro ya Dodoma asili, Haidari Gulamali wamejitokeza kuchukua fomu pia.
Jimbo la Chilonwa waliojitokeza ni pamoja na Joel Makanyaga, Daniel Ligoha, Anderson Magolola, Deo Ndejembi na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Pololeti Mgema na Dk Kedimon Mapana.
MWANANCHI
Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), limeutaka uongozi wa chama hicho kusitisha uamuzi wa kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyama vinavyounda Ukawa hadi suala hilo litakapojadiliwa kikatiba ndani ya chama hicho Julai 25.
Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye uamuzi wa kutoa tamko la kuendelea kuwamo ndani ya Ukawa au kujitoa.
Taarifa hizo za CUF zinakwenda tofauti na taarifa iliyotolewa juzi na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia kwamba wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye atatangazwa kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo, alisema hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Hata hivyo, jana Sakaya alisema: ”Hili la kujiunga na Ukawa linatakiwa kujadiliwa kwa kina na Baraza Kuu na hata ikiwezekana kuwashirikisha na wanachama ndipo mwafaka wa kujiunga au la utolewe.”
Alisema hata baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza mbele ya viongozi wa Ukawa kwamba juzi wangemtangaza mgombea wa urais lilikuwa ni kosa kwani liliwashtua wajumbe wa Baraza Kuu kwa kuwa hawakushirikishwa.
Alisema kutokana na katiba ya chama hicho, hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kutangaza jambo kama hilo hadharani bila ya kushirikisha Baraza Kuu ili litoe baraka zake.
Alisema jambo jingine ambalo liliwashtua wajumbe wa baraza hilo na wanachama wao ni baada ya kusikia taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba tayari mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Ukawa ameshapatikana.
“Ni jambo la kushangaza kwani mpaka idadi ya kura ambazo mgombea huyo kupitia chama fulani alizozipata zimewekwa hadharani kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, suala hili lilitushtua sisi viongozi na hata wajumbe wa baraza Kuu hivyo tumeona tulijadili kwanza,” alisema.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge wa CUF, Shaweji Mketo alisema ni muhimu Watanzania wakatambua kwamba CUF haijajitoa Ukawa, bali ni mchakato tu unaoendelea kwa mujibu wa sheria ya chama hicho.
Alisema nchi inapitia kipindi kigumu na pia ongezeko la majimbo 26 ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa kampeni, ni changamoto kubwa kwa Ukawa.
Alisema CUF ina imani kwamba kwa maridhiano ya pamoja, Ukawa itajengwa imara na hatimaye kuwa na mgombea mmoja wa urais, wabunge na madiwani.
MWANANCHI
Wakati Ramadhani Gembe anafanya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita miezi miwili iliyopita, hakuwahi kufikiri angeshika namba moja kwa ufaulu kitaifa licha ya jitihada zake za kujituma.
Lakini siku zote Mungu hamtupi mja wake. Kama jina lake linavyosadifu mwezi mtukufu unaomalizika siku mbili zijazo, Ramadhani ambaye amehitimu Shule ya Wavulana ya Feza jijini Dar es Salaam, ameibuka mwanafunzi bora nchini kati ya waliofanya mtihani huo wa kujiandaa kwa masomo ya elimu ya juu.
“Nilitegemea ningefaulu lakini siyo kwa kiwango hicho… hii ni ‘surprise’ (shtukizo),” alisema Gembe alipohojiwa na Mwananchi baada ya matokeo ya kidato cha sita kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa.
“Nawashukuru wazazi, walimu, ndugu na wanafunzi wenzangu kwa kunipa ushirikiano. Nilikuwa nafanya sana ibada hivyo haya matokeo ni juhudi binafsi na majibu ya Mungu,” alisema Ramadhani aliyesoma mchepuo wa fizikia, kemia na baiolojia (PCB).
Historia ya Ramadhani darasani si haba kwani mwaka 2008 alikuwa ni mwanafunzi pekee aliyejiunga na shule ya vipaji maalumu ya Ilboru, Arusha akitokea shule ya Msingi Mombo na alipata daraja la kwanza akiwa na pointi 11 katika matokeo ya kidato cha nne.
“Siku zote kilichonifanya niongeze juhudi katika masomo yangu ni malengo ya baadaye… mimi nataka kuwa daktari wa binadamu hivyo sikutaka kulegalega kusoma. Pia, wazazi wangu pamoja na hali ngumu walijitahidi kunisaidia kimawazo, kirasilimali na kimaadili…naomba na wazazi wengine wawafanyie hivyo watoto wao,” alisema.
Nurdin Gembe, ambaye ni mzazi wa Ramadhani, alisema familia imepokea kwa furaha matokeo hayo na kwamba alikuwa akiyategemea kuwa mazuri kutokana historia ya kijana wake katika madarasa ya nyuma.
“Huyu mtoto namlea kawaida japo zamani alikuwa mtundu sana… ilibidi nimpe mafundisho mengi sana ya kidini bila kupoteza ratiba ya kusoma shuleni. Nashukuru kuwa alizingatia na amefika hapo alipofika,” alieleza Gembe ambaye ni bwana shamba kitaaluma.
Kwa upande wake Yonazi Senkondo, aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, alisema matokeo hayo ni majibu ya maombi kwa Mungu na juhudi zake kusoma na ushirika na wanafunzi wenzie.
“Siku zote nilikuwa naombea niingie 10 bora, najua leo Mungu amejibu maombi yangu. Nilikuwa nafanya mijadala na wanafunzi wenzangu hasa huyo aliyeshika namba moja. Sishangai yeye kuwa katika ngazi hiyo.
MWANANCHI
Wasanii na wanamichezo mbalimbali nchini wamejitokeza kuomba fursa ya kugombea ubunge, udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa ofisa michezo mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja aliyetangaza nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Liwale, Lindi.
Mwingine ni Rais wa Shirikisho la Muziki nchini, Addo Novemba Mwasongwe, msanii wa kizazi kipya anayemiliki pia bendi ya muziki wa Bendi ya Yamoto, kundi la TMK Wanaume na Mkubwa na Wanae, Said Fella anayewania udiwani.
Kiganja ambaye ni mratibu wa michezo ya shule nchini (Umisseta na Umitashumta) alieleza kuwa amejitosa kwenye kinyang’anyiro hicho akiwania ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Nimedhamiria kuingia bungeni kwa ridhaa ya wananchi wa Liwale, mbali na kwenda kutetea masuala ya michezo, pia nitashirikiana na wana Liwale kuhakikisha tunaboresha huduma bora katika afya, elimu, miundombinu na uchumi,” alisema.
Aliongeza kuwa endapo atafanikisha dhamira yake atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Sheria ya Michezo ya mwaka 1967 inayotumika hadi sasa inaboreshwa ili michezo iendeshwe kisasa.
“Bado kuna upungufu mwingi katika sekta hiyo, sasa tunatumia sheria ya mwaka 1967 na sera ya 1995 wakati ilipaswa kuanza sera kisha sheria, hili ni tatizo ambalo linahitaji kutofumbiwa macho kwa maendeleo ya michezo,” alisema.
Naye Mwasongwe, ambaye pia ni wakili wa kujitegemea alichukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Iringa Mjini.
Katika uchaguzi uliopita, Mwasongwe aliomba ridhaa hiyo licha ya kura kutokutosha, alisema ana imani CCM itampa nafasi hiyo ili kuwakomboa wakazi wa Iringa ambao alisema wamekosa mwakilishi mzuri bungeni kwa kipindi kirefu.
Kada huyo wa CCM alisema kutokana na nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzitumikia, ni ishara tosha kuwa anao uwezo wa kupambana na changamoto za Iringa Mjini na nchi kwa jumla.
“Natambua mpasuko uliopo na ambao umesababishwa na viongozi wa juu wa chama wilayani na mkoani kwangu na wengine wamepewa nafasi za Serikali, lakini bado wamekipasua chama kwa makundi, hivyo mtu pekee ni yule asiye na kundi. Natambua kuwa mafunzo ya uongozi tanatakiwa kuanzia ngazi za shina, kata na wilaya,” alisema.
MTANZANIA
Mkazi wa Kitongoji cha Kitukila , Kilombero Mkoni Morogoro Clemence Ligoma amenusurika kufa baada ya kutafunwa na fisi wakati akiwa usingizini kwenye makazi yasiyo rasmi.
Ligoma alikutwa na dhahama hiyo akiwa amelala nje usiku wa manane.
Inaelezwa kuwa fisi huyo alipita eneo hilo na kumtafuna mguu hadi kubakia mfupa ndipo alipozinduka kutoka usingizini na kaunza kuomba msaada.
Shuhuda wa tukio hilo Ibrahimu Muhamed alisema mzee huyo alipata jeraha kubwa katika mguu wake na kukimbizwa katika kituo cha afya kwa matibabu zaidi.
Alisema jitihada za kumsaka fisi huyo zinafanyika ili asiendelee kulata madhara kwa wananchi na kuwataka watu kuacha kukaa katikamazingira hatarishi kwa maisha yao.
NIPASHE
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), limetangaza matokeo ya kidato cha sita yakionyesha kiwango cha ufaulu kikiongezeka kutoka asilimia 98.26 mwaka 2014 hadi 98.87 mwaka huu huku shule za serikali na binafsi zikichuana kwa karibu.
Ongezeko hilo la ufaulu ni sawa na asilimia 0.61.
Kadhalika, asilimia 99.96 ya watahiniwa 37,777 wa shule wamefaulu masomo ya Kiswahili na Historia, huku ufaulu katika masomo ya sayansi ukiendelea kuimarika ikilinganishwa na mwaka 2014.
Hiyo ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana Visiwani Zanzibar na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde.
Dk. Msonde alisema watahiniwa 40,753 waliandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha sita wakiwamo wasichana 12,113 sawa na asilimia 29.72 na wavulana 28,640 sawa na asilimia 70.28, wakati mwaka 2014 watahiniwa walikuwa 41,968.
Alibainisha kuwa watahiniwa 35,375 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika nchini kote, Mei 4 hadi 27, mwaka huu na kati yake, 35,188 sawa na asilimia 99.47 walifanya mtihani huo na 187 hawakufanya.
Alifafanua kuwa watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 5,378 na 761 hawakufanya mtihani huo.
“Mwaka huu waliofaulu ni 38,853 sawa na asilimia 97.65 ya watahiniwa na wasichana walikuwa 11,734 sawa na asilimia 98.56, wavulana 27,119 sawa na asilimia 97.26, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na watahiniwa 38,905 sawa na asilimia 95.98 walifaulu mwaka jana,” alisema.
Alisema watahiniwa 34,777 sawa na asilimia 98.87 ya waliofanya mtihani, wasichana ni 10,576 sawa na asilimia 99.46 na wavulaba 24,201 sawa na asilimia 98.61 na kwamba mwaka 2014 watahiniwa wa shule walikuwa 34,645 sawa na asilimia 98.26.
Dk. Msonde alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 31,450 sawa na asilimia 89.41 wamefaulu katika madaraja kwanza, pili na tatu wakiwamo wasichana 9,876 sawa na asilimia 92.88 na wavulana 21,574 sawa na asilimia 87.90.
Alisema tathmini ya ufaulu inaonyesha kuwa kati ya shule 20 bora za serikali ni 13 na zisizo za serikali saba.
NIPASHE
Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru, amekosoa mchakato uliotumika kumpata mgombea urais wa chama hicho, akieleza kuwa ulifinyangwa na hivyo ni batili, haukubaliki na hauvumiliki.
Aidha, ameshauri kuwa ili chama hicho kiendelee na kampeni za uchaguzi kikiwa kimoja, ni lazima kasoro zilizotokea Dodoma zijadiliwe kwa kina kumaliza tofauti zinazoonekana kujitokeza na kupata maridhiano.
Jumapili iliyopita CCM ilimteua Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuwa mgombea wake wa urais na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea mwenza.
Kingunge alisema viongozi waandamizi wa CCM wamekiuka kwa makusudi katiba, kanuni na taratibu za chama kuanzia kwenye vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CC) hadi Halmashauri Kuu (Nec).
Hata hivyo, alisema maamuzi ya Mkutano Mkuu uliompitisha Dk. Magufuli anayaheshimu kwa kuwa kasoro zilijitokeza CC na Nec.
Alisema Katiba ya CCM pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa Kamati ya Maadili ambayo ameeleza ni kitengo ndani ya chama ina jukumu la kuandaa taarifa kuhusu wagombea na siyo kukata majina.
Alisema taarifa inayoandaliwa na kitengo hicho hupelekwa CC, ambayo kazi yake ni kumsikiliza mgombea mmoja mmoja na kumuuliza maswali yasiyopungua matatu, kisha wajumbe hukaa na kupendekeza majina matano ambayo yanapelekwa Nec.
“Kwa utaratibu wa kikatiba, sekretarieti kazi yake ni kuhudumia CC na Nec kwa kukusanya majina ya watu walioomba, inayapanga vizuri, ikikamilika inawasilisha taarifa yake kwenye Kamati Kuu…sekretarieti si kikao cha maamuzi wala si kikao cha mapendekezo, kwa hiyo mchakato hasa unatakiwa uanze kwenye Kamati Kuu,” alisema.
Kingunge alisema utaratibu ambao umetumika tangu mwaka 1995, kila mgombea atapaswa kuhojiwa na kamati kuu mmoja mmoja na kuulizwa maswali yasiyopungua matatu na kisha wajumbe huwajadili na kutoa mapendekezo ya majina matano kwenda Nec.
“Inaelekea kazi ya kupata wagombea watano ilifanywa na kitengo kinachoitwa Kamati ya Maadili na Kamati Kuu ikafikishiwa majina matano tu, kitendo hicho cha kuinyang’anya Kamati Kuu kazi yake si cha kawaida, ni uvunjifu wa taratibu na hakuna uadilifu ndani yake. Kamati ya Maadili yenyewe inavunja maadili,” alisema.
Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM na serikalini, alisema maadili ya chama yanaanzia kwenye kuheshimu muundo wa chama, sera na taratibu zake; hivyo ukiukwaji uliofanyika Dodoma ni kukinyonga chama hicho.
Alisema inasikitisha kwamba hata baada ya kupelekewa majina matano, CC ilifanya maamuzi yake bila kuwaona wagombea wote 38 waliorudisha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais na hata wagombea waliokatwa hawakuitwa kwenye hicho kitengo cha maadili badala yake walihukumiwa bila kusikilizwa.
“Kwa hiyo kuna mahala fulani watu wachache wamekaa wakatengeneza orodha yao na wakataka Kamati Kuu imeze. Kilichofanyika si jambo dogo tu…Mzee Abeid Aman Karume alisema nchi hii ni yetu wote na mimi nasema maana yake tunaowapa madaraka wasifike mahali wakafikiria nchi hii ni yao wao, yale madaraka ni dhamana tu; na kwenye chama ni hivyo hivyo, CCM ni mali ya wanachama wote,” alisema.
Kingunge alisema chama hicho kilitoa fomu kwa wanachama ambao waliingia gharama kuzunguka mikoa mbalimbali kusaka wadhamini lakini katika hali ya kushangaza, kitengo cha maadili kiliwapuuza na kufanya maamuzi batili.
Alisema kwa utaratibu wa chama, CC ilitakiwa kuwasilikiliza wagombea wote 38 waliorudisha fomu, kuwajadili na kutoka na mapendekezo ya majina matano kupeleka Nec; utaratibu ambao ulikiukwa.
Alisema vikao vya vyombo mbalimbali ndani ya chama vimewekwa ili kutenda haki kwa wanachama wote hivyo ni muhimu kuviheshimu kwa nia ya kuleta usawa na kwamba kilichotokea Dodoma ni dharau kwa wagombea waliochukua fomu na wanachama wote wa CCM.
“Bahati mbaya katika nchi yetu wananchi ni wavumilivu mno kiasi kwamba tumefanya wakubwa zetu tunaowapa madaraka wanajua wanaweza kufanya chochote kwa sababu hakutakuwa na chochote. Sasa mimi nasema hakutakuwa na chochote sawa, lakini hata kusema?. Kwa hiyo mimi nasema kwa niaba ya wengi walio kimya,” alisema.
Kingunge aliongeza kuwa: “Na mpaka hapo kwenye CC yaliyofanyika si sahihi na kwa kweli ni batili. Upande mmoja Kamati Kuu kunyang’anywa kazi yake na kitengo lakini upande mwingine haki ya asili ya kusikilizwa, watu hawawezi kuhukumiwa tu bila kusikilizwa. Kamati Kuu inatakiwa iandae orodha fupi ya hao walioomba lakini baada ya kuwasikiliza.”
Hata hivyo, alisema Nec ina mamlaka ya kuhoji mapendekezo ya CC, kuyakubali, kukataa baadhi au yote; lakini katika hali ya kushangaza, haikufanyika hivyo.
Alisema mjadala kwenye Nec ulivyokuwa hata wazee wastaafu ndani ya CCM ambao ni marais wastaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume, walipotoshwa na hivyo michango yao iliminya haki za baadhi ya wagombea.
Hata hivyo, alisema pamoja na upotoshaji uliofanywa na kikundi cha viongozi wachache, msimamo wa Nec ulikuwa dhahiri kwamba wajumbe walimtaka mgombea aliyekuwa na nguvu kuliko wengine, Edward Lowassa.
Bila kuwataja viongozi wakuu wa chama hicho na serikali ambao walifinyanga majina ya wagombea watano na kuyawasilisha CC, Kingunge alisema viongozi hao walifanya jitihada na nguvu kubwa kuvunja kanuni na taratibu ili kuhakikisha wanamnyima haki Lowassa.
Alisema tangu mwaka 2008 baada ya kashfa ya Richmond, Lowassa amekuwa akiandamwa kuwa ni fisadi lakini ni ‘hadithi’ ambayo imekosa mashiko kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilichunguza na kuthibitisha kuwa hakukuwa na vitendo vyovyote vya rushwa.
JAMBOLEO
Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje atafikishwa mahakamani na chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza wakati wowote akituhumiwa kuwaibia wananchi wa jimbo hilo milioni 75 za mfuko wa jimboni humo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu mkuu wa CCM Mkoa Miraji Matuturu wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika soko la Igogo, Nyamagana.
Alisema CCM itaweka wakili ili Mbunge huyo awaeleze wananchi zilipo milioni 75 alizochangisha kwa ajili ya kusaidia kuboresha mfuko wa elimu jimboni kwake, lakini akazitumia kwa mafufaa na maslahi yake na familia yake.
Alidai Wenje alianzisha mfuko wa elimu ambapo Rais Kikwete alichangia milioni 10, Zitto na wageni wengine walichangia milioni 8 na Raila Odinga alichangia dola za Marekani 6,000.
Unahitaji chochote nachokipata kikufikie? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.