HABARILEO
Wakati joto la uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu likizidi kupanda, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeviagiza vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kisheria, kutoendesha kampeni zao katika nyumba za ibada.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alipozungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi ya Tume hiyo mjini hapa.
Alivitaka vyama hivyo kuzingatia maadili kama ilivyokubaliwa na vyama vyote 22 na ambayo viongozi wake waliridhia na kusaini mbele ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mbali na nyumba za ibada, NEC pia imeviagiza vyama hivyo vya siasa, kutoendesha kampeni zao katika taasisi za umma kama vile vyuo vikuu.
Kwitega alisema NEC ni chombo huru, ambacho hakifungamani na chama chochote cha siasa na kwamba jukumu lake ni kusimamia kwa uadilifu wa hali ya juu masuala ya Sheria za Uchaguzi nchini.
Mbali na nyumba za ibada na taasisi za Serikali, pia alivitaka vyama vya siasa kuepuka kutumia lugha za matusi kejeli na kashfa wakati wa kampeni, huku akivihimiza kunadi sera zake mbele ya wananchi pamoja na yale ambayo chama husika kimetekeleza ama kinatarajia kutekeleza.
Alisema NEC itasimamia maadili ambayo yamekubaliwa na vyama vyote vya kisiasa vyenye usajili wa kudumu. Aidha, Kwitega alivitaka vyama vya siasa kutowatumia viongozi wa madhehebu ya dini, kuendesha kampeni zao katika madhehebu yao.
Alisema kwamba maeneo ya ibada ni kwa ajili ya kuabudu, sio kuendesha kampeni za kisiasa. Pazia la kampeni kwa vyama vyote, zinazotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili, linatarajiwa kufunguliwa Agosti 22.
HABARILEO
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya afya, wanatarajia kuendesha kampeni ya uhamasishaji wa uzazi wa mpango kwa jamii katika maeneo ya mabaa na vilabu vya pombe mkoani Kigoma.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la World Lung Foundation, Victoria Marijani alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari wakati wa kikao cha wadau kujadili njia mbalimbali za kuwa na mpango wa pamoja na kuendesha kampeni za uzazi wa mpango mkoani Kigoma.
Alisema mkakati huo, unalenga kufikia malengo ya kitaifa ya asilimia 60 ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ili kuongeza uelewa kwa wananchi ambao wakati mwingine hawafikiwi katika kampeni zinazofanyika.
Hata hivyo, Meneja huyo wa World Lung Foundation, alisema umekuwa na mafanikio kiasi katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango tangu kuanza kwa kampeni zinazoendeshwa na shirika hilo na watu wameanza kujitokeza katika kutumia njia hizo za uzazi wa mpango.
Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dk Leonard Subi alisema bado kuna uelewa wa chini kwa wananchi wa mkoa huo katika kujua elimu ya afya ya uzazi na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ambapo kwa sasa asilimia 14 ya wananchi wa mkoa huo ndiyo wanaotumia njia hizo.
Sambamba na hilo, Dk Subi alisema dini, mila na desturi pia ni kikwazo kwa wananchi katika kutumia njia za uzazi, ambapo wananchi wengi wanaamini kwamba kila mtoto anakuja na riziki yake aliyoandikiwa na Mungu.
Alisema kufanyika kwa mkutano huo wa pamoja wa wadau wanaotoa huduma za afya katika sekta hiyo, kutasaidia kuzifanya kampeni hizo kuwa na mafanikio na kuongezeka kwa uelewa kwa wananchi katika kutumia njia za uzazi wa mpango.
Dk Wilfred Mongo kutoka shirika la EngenderHealth, alisema kuwa bado hakuna wataalamu wa kutosha wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango na kwamba kilichopo sasa ni watu wengi kutoa habari kuhusu jambo hilo kuliko kutoa elimu.
HABARILEO
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) upande wa Zanzibar, umesema unaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete kwamba CCM imejiandaa kushinda na kushika dola kwa sababu inao uzoefu wa kuongoza nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya UVCCM eneo la Gymkanna mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alisema hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti huyo wa CCM wakati wa kuwapokea wagombea wa chama hicho kuchukua fomu kutoka Tume ya Uchaguzi NEC katika ofisi ndogo za CCM Lumumba, imewavunja moyo wapinzani kwa kiasi kikubwa.
Shaka alisema CCM haibabaishwi na uamuzi wa kuhama kwa waliokuwa viongozi wake mbalimbali kwani tangu mwaka 1957 wakati wa harakati za kudai uhuru viongozi wa vyama vya TANU na ASP walikuwa wakihama vyama hivyo na kwenda upinzani.
“Tunaipongeza hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amewaambia ukweli wapinzani kwamba CCM imejiandaa kushinda katika uchaguzi mkuu kwa sababu inao viongozi safi wenye uwezo wa kuongoza dola,” alisema.
Aidha Shaka alitumia nafasi hiyo kusema kwamba UVCCM ipo imara huku ikiwaunga mkono wagombea wa CCM wa nafasi mbali mbali ikiwemo ya urais wa muungano.
Alisema umoja wa vijana katika mchakato wa wagombea wa nafasi ya urais wa muungano haukuwa na mgombea unayemuunga mkono, isipokuwa wanachama wenyewe walikuwa huru kutafuta mgombea wanayeona anafaa.
“Mchakato wa kuwania nafasi ya urais wa muungano umemalizika na sasa tunaye mgombea John Magufuli na mgombea mwenza Samia Suluhu. Hao ndiyo wagombea tunaowaunga mkono UVCCM katika harakati za kuwania urais wa muungano,” alisema.
Alisema mgombea aliyepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM, John Magufuli pamoja na mgombea mwenza Samia Suluhu ni viongozi wenye uwezo mkubwa wa kuongoza nchi ambao walipata kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi
MWANANCHI
Wakati vyombo vya juu vya baadhi ya vyama vya siasa vikiwa vimeanza hatua za mwisho za kupitisha wagombea wa ubunge na udiwani tayari kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, hadi juzi wabunge 51 walikuwa wameanguka kwenye kura za maoni za ndani ya vyama vyao.
Idadi hiyo ni takriban asilimia 14 ya wabunge 357 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, inayojumuisha waliochaguliwa na wananchi na wa viti maalumu, ambao waliamua kwenda kupambana majimboni.
Miongoni mwa walioanguka ni mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambao walikuwa wakitetea viti vyao majimboni.
Kati ya wabunge hao walioanguka, wawili wanatoka Chadema, wanne CUF na wengine 45 waliosalia wanatoka CCM.
Matumaini pekee yaliyosalia kwa wabunge hao ambao baadhi yao wamekata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni, ni huruma za vikao hivyo ambavyo vinaweza kubadili matokeo ya baadhi ya majimbo, hasa ambayo taratibu zilikiukwa na ushahidi wa kuwapo matumizi ya rushwa.
Wakati wabunge walioanguka Chadema wanasubiri kwa hamu kikao cha Kamati Kuu kilichoanza juzi kupitia majina hayo, wa CCM wanasubiri mfululizo wa vikao vinavyoanza leo hadi Agosti 13, wakati mchakato kupitisha wagombea wa NCCR-Mageuzi bado.
Kwa wabunge wa CUF, hakuna matumaini kutokana na vikao vya juu vya chama hicho kukamilisha kazi yake hivi karibuni.
Mbali na walioanguka, wabunge waliopita katika kura za maoni lakini vyama vyao vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), nao watalazimika kusubiri hadi vyombo hivyo vya mchujo vitakapomaliza kazi, kujua kama wamepita.
Hiyo inatokana na makubaliano ndani ya umoja huo ya kusimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.
Kwa mujibu wa makubaliano ya vyama hivyo vinne; Chadema, CUF, NLD na NCCR – Mageuzi- kinachooonekana kina nguvu kwenye jimbo fulani ndicho mgombea wake ataachiwa kupeperusha bendera ya umoja huo, jambo ambalo vyama hivyo vilisema vimekamilisha kazi ya mgawanyo kwa asilimia 95.
Wakati Chadema, CUF, NCCR na NLD wakisubiri utekelezwa wa makubaliano hayo, wabunge wa CCM watakuwa njiapanda baada ya chama hicho kueleza kuwa hakitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kupingana na maoni ya wanachama kwa kutengua matokeo ya kura za maoni.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jamidu Katima alisema kuanguka kwa wabunge hao kunatokana na wengi wao kutoonekana majimboni baada ya kupewa dhamana ya kuongoza wananchi.
“Kama kiongozi umepewa dhamana, lakini huonekani jimboni basi ni dhahiri wananchi watakukataa. Wakikuona unachukua fomu watakushangaa lakini ujue watakukataa kwa sababu huwatatulii kero zao kama ulivyoahidi awali.”
Profesa Katima alisema kwa sasa Watanzania wameamka, hivyo ni vigumu kudanganyika na kwamba kama kiongozi hatumii vyema dhamana aliyopewa, wananchi watamuacha apumzike kwa amani.
Maoni kama hayo yalitolewa na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo ambaye alisema zipo sababu chekwa za baadhi ya mawaziri kushindwa kwenye kura za maoni, mojawapo ikiwa ni makundi na kushindwa kutimiza ahadi.
Dk Makulilo alisema ni rahisi kwa wananchi kuacha kumchagua kiongozi baada ya kuona hajatimiza kile alichoahidi hivyo wakaona wajaribu kiongozi mwingine pengine atawatatulia kero zao.
Kuhusu kuanguka kwa wanasiasa nguli wa CCM, mhadhiri huyo alisema sababu nyingine ni siasa za makundi ambako kundi moja tu linaweza kufanya juhudi ili mwingine ashindwe.
“Sasa hivi tunazungumzia mtu kuanguka katika chama chake, kwa hiyo siasa za makundi ndani ya chama hicho inaweza kusababisha kuanguka katika kura za maoni,” alisema.
Sababu nyingine aliyoitaja Dk Makulilo ni wimbi la vijana na kuwa inawezekana wananchi wanahamia kwa wanasiasa vijana zaidi baada ya kuona wengine amekaa madarakani kwa muda mrefu.
MWANANCHI
Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuzungumza na gazeti hili na kusema yupo salama, mke wake, Josephine Mushumbusi amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri kiongozi huyo wa Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.
Tetesi hizo zilivuma kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya Dk Slaa kutoonekana katika vikao muhimu vya Chadema na Ukawa, kuwa Mushumbusi hakupendezwa na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania urais chini ya mwavuli wa Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe mpeperusha bendera.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi amezikanusha, aliamua alimfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia asishiriki shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini akija akakuambia ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji Mushumbusi akianza kutoa maelezo yake na kuendelea:
“Wakati wa vikao nilikuwa namwona (Dk Slaa) anachelewa kurudi kila siku, siku moja akaja akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa na la kusema, nikachukua shuka nikajifunika.”
Katika mahojiano yake ya kwanza na Mwananchi baada ya kuzagaa kwa tetesi hizo, Mushumbusi pia alikana kumfungia Dk Slaa ndani ya nyumba, akisema wakati maneno hayo yalipokuwa yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na wala hakujua kinachoendelea.
“Mwenyewe najiuliza nini kinaendelea, siwezi kufanya kitu kama hicho. Nyumba yangu ina milango miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena mwanamume, hata watoto siwezi kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi kuyafanya kwa mwanamume. Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.
Alisema viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanafika nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye… “Kama ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”
Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia.
Akifafanua tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu Chadema, Mushumbusi alisema kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni msaidizi tu ambaye hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.
Hata hivyo, alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa kufanya hivyo anao lakini yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya mumewe.
“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu), ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.
Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali.
Bila kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda propaganda hizo ili abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi kutokea.
“Nilisema nitampenda kama alivyo, sitajali chochote wala akiwa katika hali gani au chama gani. Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile atakachofanya kifanikiwe,” alisema.
Mbali na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema alikwishajitoa kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala yake ameamua kufanya biashara ya kuuza mkaa.
MWANANCHI
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amekiri mbele ya Baraza la Maadili kupokea Sh1.6 bilioni kutoka Kampuni ya VIP Enginering and Marketing Limited, zikiwa ni malipo ya kutoa ushauri.
Pia, alihoji kama kuna tatizo kutumia taaluma yake ya sheria kuzishauri kampuni binafsi na kujipatia fedha.
Chenge ambaye alitoa utetezi wake jana saa 7:30 mchana, alisema hakulipwa fedha hizo kwa sababu ni kiongozi wa umma, bali kwa kutoa ushauri.
Alisema aliingia mkataba na kampuni hiyo wa kutoa ushauri wa kisheria dhidi ya Kampuni ya Mechmer ambazo ni kampuni binafsi zilizokuwa na mgogoro.
“Nawashangaa mnalalamika Chenge kulipwa na Kampuni ya VIP au wamewafuata na kulalamika kwamba hayakuwa malipo halali,” alihoji.
Alisema hakuna kufungu cha sheria kinachomzuia kutoa ushauri wa kisheria kwa kampuni binafsi.
Kuhusu malalamiko kwamba akiwa Mwanasheria wa Serikali aliishauri kuingia mkataba wa kuuziana umeme kati ya Kampuni ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Chenge alisema anawashangaa wanasheria wa sekretarieti kwa malalamiko hayo.
“Sikuishauri Serikali kuingia mkataba na IPTL bali ofisi yangu ndiyo iliyotoa ushauri kisheria. Nakubaliana na walalamikaji kwamba mwaka 1995 nilikuwa mwanasheria wa Serikali, lakini sikubaliani na madai yao.”
Alisema Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali ilitoa ushauri huo kwa sababu ndiyo jukumu lake.
“Wanasheria ni lazima wafahamu kwamba ile ni taasisi na siyo mtu kama Chenge,” alisema.
Alisema ofisi yake ilitoa ushauri wa mikataba mitatu ya IPTL na Serikali kwa lengo la kuongeza umeme hasa kutokana na ukame uliolikumba Taifa.
“Naomba baraza lako liyapuuze kwa dharua zote na kuyatupilia mbali malalamiko ya sekretarieti kwa sababu hayawezi kukusaidia kutoa uamuzi ulio sahihi,” alisema.
Kuhusu kutumia taarifa alizozipata akiwa mwanasheria wa Serikali na kuzitumia kwa masilahi binafsi, Chenge alisema: “Naomba wachanganue taarifa hizo ni zipi kwa sababu huwezi kumlalamikia mtu kwa jumla lakini kwenye malalamiko husemi.
Shahidi wa mlalamikaji, Waziri Kipacha alisema Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na IPTL.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi limesema limeshakamata bunduki 16 kati ya 21 zilizoporwa kwenye Kituo cha Stakishari.
Bunduki hizo ziliporwa Julai 12 wakati watu wanaoaminika kuwa ni majambazi walipovamia kituo hicho cha polisi, Ukonga – Dar es Salaam na kuua askari wanne na watu wengine watatu.
Jana, Naibu Kamishna wa Kanda ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari kuwa zaidi ya majambazi 10 wameshakamatwa na polisi wanaendelea kuwahoji kuhusu tukio hilo.
“Silaha zilizokuwa zimebaki ni tano, 16 zimeshakamatwa na hizo tano ndizo tunafanya bidii ya kuzipata. Niwahakikishieni kuwa zitapatikana,” Sirro.
Alisema watuhumiwa waliovamia kituo hicho walikuwa zaidi ya 15 na walitumia mbinu mpya ambayo Polisi hawakuitegemea.
Wakati huohuo; Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya ofisa wa Polisi, Elibariki Palangyo yaliyotokea nyumbani kwake Yombo Kilakala, usiku wa Agosti.
Katika tukio jingine, polisi inawashikilia watu wanne wakituhumiwa kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh30 milioni juzi, saa 1.30 usiku huko Tandale kwa Mtogole.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetumia zaidi ya Sh. bilioni 218 kwa uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa Biometric Votes Registration (BVR) pamoja na ununuzi wa mashine na vifaa vya BVR kits.
Mkurugenzi wa Nec, Kailima Ramadhani, alisema Sh. bilioni 133 zilitumika kununua mashine za BVR 8,000 zilizotumika kuandikisha wapiga kura.
Alisema Sh. bilioni 85 zilitumika katika uandikishaji kikiwamo kulipa posho waandikishaji, opereta, kutengeneza kadi, karatasi, wino na vifaa muhimu vilivyohitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo 99.5.
Alisema, lengo lilikuwa kuandikisha wapigakura 23, 913,184 na hadi uandikishaji unakamilika Agosti Jumanne iliyopita, wapigakura 23,782,558 wameandikishwa.
Kailima alisema maandalizi ya msingi yamekamilika, ikiwamo kuwapata wazabuni wa kusambaza vifaa hivyo ambao watajulikana baada ya Agosti 21, mwaka huu.
“Maandalizi yote yamekamilika, hatuwezi kuchapisha karatasi kwa sasa tunasubiri taarifa za wagombea wakaopitishwa kutoma kwenye vyama vya siasa, kwa maana ya chama, jina, picha, eneo na nafasi anayogombea…tunaweza kuweka majina halafu wakiwekewa pingamizi tutatakiwa kuchapisha tena,” alisema.
Kuhusu malalamiko yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, Kailima alisema hakuna ukweli wowote wa kuhama kwa tiki iliyowekwa na mpigakura kwenda kwa mgombea ambaye hakumchagua.
Alisema kuna kamati mbalimbali zenye wajumbe kutoka ndani ya vyama ambao hushiriki hatua zote na kwamba hakuna atayekubali kuona chama chake kinahujumiwa.
Aidha, alirejelea kauli ya Nec kuwa watu watapiga kura katika maeneo waliyojiandikishia na ambao watapigia maeneo mengine watakuwa na fursa ya kuchagua Rais pekee.
NIPASHE
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), hawajalipwa mishahara ya miezi mitatu kati ya miezi sita waliyokuwa wakiidai mamlaka hiyo.
Wafanyakazi hao hawajalipwa mishahara ya Januari, Juni na Julai, mwaka huu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Patrick Nyakeke, alisema baadhi ya wafanyakazi hawajalipwa mishahara ya kuanzia Januari hadi Mei, mwaka huu
“Wafanyakazi zaidi ya 1,500 bado hawajapewa mishahara ya miezi ya Januari, Juni na Julai huku wengine wakiwa wanaudai uongozi wa Tazara mishahara ya miezi mitano pamoja na malimbikizo mengine,” Nyakeke.
Aidha, alisema mishahara ya Januari na Juni, mwaka huu, utalipwa na Menejimenti ya Tazara na wa Julai mwaka huu, unatarajiwa kulipwa kupitia Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya 2015/16 iliyotengwa na serikali.
Hata hivyo, alisema baada ya wafanyakazi kuuhoji uongozi wa mamlaka hiyo kuhusu suala hilo, walielezwa kuwa watalipwa mishahara na malimbikizo ya fedha za likizo kupitia makusanyo ya Tazara ya Januari hadi Julai, mwaka huu.
Nyakeke alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imetenga Sh. bilioni 30 ili kuhakikisha wafanyakazi wanaondokana na adha ya kusotea mishahara.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos