Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imefafanua kuwa hakuna uthibitisho kwamba mkimbizi aliyekufa kwenye kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, alikuwa akiumwa ugonjwa wa ebola.
Agosti 9 mwaka huu, Buchumi Joel akitokea katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili, hasusan kwenye fizi, macho na masikio. uzikwa chini ya uangalizi wa ofisi ya afya ya mkoa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo mpaka sasa hakuna uthibitisho kwamba mgonjwa huyo amekufa kutokana na ebola, licha ya kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.
“Ili kupata uhakika wa hilo tayari sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa uchunguzi zaidi, kujua chanzo cha ugonjwa huu,” ilisema taarifa hiyo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huo iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.
Katika hatua nyingine, wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo uliotikisa dunia katika miaka ya hivi karibuni.
Miongoni mwa tahadhari hizo ni kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, haja ndogo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya anapohisiwa kuwepo mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Mpaka sasa zaidi ya watu 11,269 wamepoteza maisha katika nchi za Guinea, Liberia na Siera Leone tangu kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa huo
MWANANCHI
Mbunge wa Sikonge, CCM, Said Nkumba ametangaza kukihama hicho na kujiunga na Chadema, kwa madai CCM ‘haina mapenzi na watu’.
Nkumba anakuwa mbunge wa sita kutoka CCM kutimkia upinzani katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja.
Wabunge waliokihama chama hicho ni Edward Lowassa (Monduli), Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi), Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya.
Lowassa ametimkia Chadema na ndiye aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho kwa mwavuli wa Ukawa, kugombea urais katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.
Nkumba alisema: “Sikushawishiwa, nimejiondoa CCM kwa uamuzi wangu na nimefanya hivi kwa kuwa sikuwa nasikilizwa kwa kile nilichokisema.
“Niliipenda CCM kwa dhati kabisa, lakini sikuona sababu ya kuendelea kubakia CCM, sisikilizwi, chama hakina mapenzi na watu, ndiyo maana tunaondoka.”
Nkumba aliyekuwa kinara wa kuipinga Ukawa ambao baada ya kutoka bungeni kwenye Bunge la Katiba, alisimama kidete na kuanzisha “Tanzania Kwanza, Mbili yatosha” alisema amejiunga na upinzani ili kujenga chama cha Chadema.
“Mimi najiamini, ninakubalika ndani ya chama, sasa nimekuja huku, nataka kuendelea mazuri ya Chadema, ninaona huku kunanifaa,” alisema Nkumba.
Akizungumzia kuwa wanaokwenda upinzani ni makapi, Nkumba alisema kuwa hata makapi bado yanakuwa na faida.
“Unajua kuwa wakati mwingine makapi ya asali labda ukamua sawasawa, lakini kwa hapa, sisi bado tuna asali, si makapi yasiyokuwa na kitu.”
Kuhusu hatma ya CCM na kuondokewa watu mbalimbali na kujiunga upinzani, Mbunge huyo alisema kuwa wakuu wa chama hicho, lazima washtuke na wasipokuwa makini, huu utakuwa mwisho wa CCM.
“Hivi wewe hushtuki, wanaona kabisa chama kikubwa lakini watu wanaondoka, wanaona kabisa mwelekeo haupo, halafu wanaendelea na yao, ni wazi kuwa wataanguka,” alisema.
MWANANCHI
Sasa ni dhahiri kuwa mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yanayofanyika leo yatamkutanisha kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tangu waziri huyo mkuu wa zamani ajiondoe CCM na kujiunga na Chadema.
Ingawa ratiba ya JK haikuwekwa wazi, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga alisema Rais atawasili wilayani Mwanga leo mchana.
“Tunatarajia Rais atawasili wilayani kwetu mchana na tunatarajia ibada itaanza saa 7:00 mchana. Shughuli za kuaga mwili hapa Usangi zitaanza saa 3:00 asubuhi katika Usharika wa Kivindu,” alisema.
Habari zaidi kutoka kwa mmoja wa wanafamilia zinasema kuwa Rais atawasili kwa helikopta. Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro leo saa 2:00 asubuhi na kwenda moja kwa moja na msafara wa magari hadi Usangi wilayani Mwanga kwa ajili ya mazishi hayo.
Vigogo wengine waliothibitisha kuhudhuria mazishi hayo ni pamoja na waziri mkuu mstaafu na baba wa Jimbo la Mwanga, Cleopa Msuya, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro na Lowassa.
Kwa kawaida shughuli za mazishi huwa hazichukui mwelekeo wa kisiasa na ni kawaida mahasimu kukutana, kuongea na kusalimiana, lakini tukio la leo litakuwa likifuatiliwa kutokana na matukio ya hivi karibuni ya wawili hao ambao hawakukutana “barabarani”.
Vigogo hao wanakutana, ikiwa ni siku nne tu baada ya Lowassa kumtaja hadharani Kikwete kuwa ameharibu uchumi wa nchi kwa kushindwa kusimamia mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali ambazo ni muhimu kwa wananchi.
Akimpokea mgombea urais wa CCM, John Mafuguli baada ya kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Kikwete, bila kumtaja Lowassa, alisema: “Mtoto wako akikukosoa na kuungana na maadui, unamshughulikia pamoja na maadui hao ili kumwonyesha kuwa wewe ni baba yake.”
Kutofautiana kwao kulianza mara baada ya Kamati Kuu ya CCM kumuengua Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Akiwa mwenyekiti wa CCM, Julai 11 mjini Dodoma, Kikwete aliongoza kikao cha Kamati Kuu kilichoengua jina la Lowassa, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho kutokana na kuwa na uzoefu na kukubalika kwa wanachama kulinganisha na makada wengine 38.
NIPASHE
Wakati kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu msimamo halisi wa kisiasa wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, mwenyewe ameibuka na kusema ataweka kila kitu hadharani muda wowote kuanzia sasa.
Katika siku za karibuni, Dk. Slaa amekuwa gumzo kutokana na kutoonekana katika shughuli mbalimbali za chama hicho pamoja na mikutano muhimu inayoitishwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Dk. Slaa alisema kuna mambo mengi yanayozungumzwa juu yake ambayo hayana ukweli wowote na kwamba hivi karibuni atazungumza na kuweka hadharani kila kitu.
Hata hivyo, Dk. Slaa hakusema ni mambo gani yasiyo ya kweli yanayozungumzwa juu yake na wala hakuwa tayari kuweka wazi siku atakayoweka hadharani yale aliyoyahifadhi moyoni mwake.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa atashiriki uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao, Dk. Slaa alisema hakuna ukweli wowote kuhusiana na jambo hilo na zaidi, akasisitiza kuwa pawe na subira kwani mambo yote yatajulikana siku atakapozungumza.
“Hakuna ukweli baba… sijui kwa nini watu wanapenda kutoa kauli za namna hiyo. Ukweli utajulikana tu ndani ya muda mfupi,” alisema Dk. Slaa kupitia ujumbe mfupi alioutuma kwa namba ya simu yake ya kiganjani jana.
Awali, Dk. Slaa alipigiwa simu na Nipashe simu yake ya mkononi ikawa inaita muda mrefu bila kupokelewa, lakini baadaye alipotumiwa maswali kupitia ujumbe mfupi wa maneno alijibu haraka na kukanusha taarifa zilizodai kuwa atashiriki uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu zitakazoanza Agosti 22.
Swali jingine aliloulizwa ni sababu za yeye kuwa kimya na haonekani katika shughuli za kisiasa za chama chake na Ukawa unaoundwa pia na washirika wa Chadema; Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alikaririwa akisema kuwa amewasiliana na Dk. Slaa na kwamba (Dk. Slaa) amekubali kushiriki uzinduzi wa kampeni za Ukawa kwenye jimbo la Kibamba.
Mnyika aliwaambia wanachama wa Chadema wa matawi ya kata ya Goba muda mfupi kabla ya kufanyika kura za maoni kumchagua mgombea wao wa udiwani katika eneo hilo.
“Dk. Slaa yupo mapumzikoni na nilizungumza naye kwa kirefu na aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni za chama Jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge,”Mnyika.
NIPASHE
Maduka sita yanayozunguka Soko Kuu la Morogoro, yameteketea kwa moto kutokana na hitilafu ya umeme na kuwasababishia hasara wafanyabiashara ambayo thamani yake haijajulikana.
Mashuhuda na wamiliki wa maduka hayo, walidai kuwa moto huo ulianzia kwenye duka la mmoja wao usiku wa kuamkia juzi baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Morogoro, kurejesha umeme na kusambaa kwenye maduka mengine.
Mmoja wa wafanyabiashara, Didas Mushi, alilitupia lawama Tanesco kwa kuwa chanzo cha moto huo kutokana na kukata umeme mara kwa mara na kuurejesha bila ya kutoa taarifa.
“ Chanzo kwa maduka haya kuungua ni kukatika kwa umeme wa Tanesco mara kwa mara bila kutoa taarifa na uliporudisha majira ya saa sita usiku (juzi) ulitokea mlipuko na moto kusambaa hadi kwenye maduka mengine,” alisema “ Mushi.
Mfanyabiashara wa nguo, Masanja Okwima, alisema kuungua kwa maduka hayo kumewasababishia hasara ya zaidi ya Sh. milioni 10 na kuitaka Tanesco kulipa gharama hizo kwakuwa wao ndio chanzo cha moto huo.
Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Morogoro , Marcio Semfukwe, alithibitisha moto huo kusababishwa na hitilafu ya umeme ambayo huenda imesababishwa na mmoja wa wafanyabiashara hao kuunganisha nishati hiyo bila kibali cha shirika hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusisitiza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi.
NIPASHE
Wafanyakazi wa Kampuni ya China Major Bridge Engineering Co. ltd wamegoma kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigamboni, wakiushinikiza uongozi kuwalipa madai yao.
Miongoni mwa mambo wanayodai ni malipo ya mshahara wa kima cha chini cha Sh. 325,000 kilichotangazwa na serikali pamoja na kuwapatia mikabata ya kazi.
Khamis Mpili, alisema tangu mradi wa ujenzi huo uanze kuna wafanyakazi hawajapatiwa mikataba ya kazi, hali inayosababisha kukosa haki zao za msingi zikiwamo malipo ya likizo, nyongeza ya mishahara, na kuingiziwa fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
“Kuna wafanyakazi wana mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu hawana mikataba ya kazi, tunataka uongozi utupatie stahiki zetu tuendelee na kazi,” alisema Mpili.
Aidha, alisema wanafanya kazi kwa saa 84 badala ya saa 45 bila kupewa likizo na kwamba baadhi ya wafanyakazi walipata ulemavu cha kushangaza wameachwa bila kupatiwa matibabu kufuatana na sheria za ajira zinavyoelekeza.
Alisema viongozi wa NSSF walikwenda eneo la ujenzi na kuwaandikisha wafanyakazi wachache katika fomu za usajili huku wengine wakikosa fomu hizo.
Alidai kuwa waliowateua kuwapigania haki zao walifukuzwa kazi na uongozi.
Izua Sosthenes, alisema Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka , alifika ofisi za makandarasi hao, lakini hakuonana na wafanyakazi wamueleze matatizo yao.
Alisema, siku nyingi zimepita tangu, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alipokwenda kukagua ujenzi wa daraja hilo.
Mhandisi wa kampuni hiyo, Liu Tao, alisema kampuni yao iliingia mkataba na serikali mwaka 2012 kabla ya sheria ya mshahara wa kima cha chini haijabadilishwa.
Alisema watafanya juu chini kuhakikisha wanaanza kuwalipa baadhi ya wafanyakazi madai yao na kuahidi wengine watamaliziwa haraka iwezekanavyo.
Aliongeza kuwa baada ya kuwalipa, ujenzi utaendelea na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Mwanasheria wa Wizara ya Kazi na Ajira, Omari Sama, alisema walichokigundua ni uelewa mdogo wa matakwa ya sheria za kazi kati ya mwajiri na waajiriwa, hivyo walichofanya kutoa elimu kwa pande zote mbili.
Meneja Mradi huo kutoka NSSF, Karim Mattaka, alisema mgomo walioufanya wafanyakazi wa kampuni ni batili kwa kuwa wamekwenda kinyume cha sheria cha kufanya migomo zinavyoeleza.
NIPASHE
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), imepitisha majina ya wagombea ubunge wa majimbo pamoja na viti maalumu, huku baadhi ya wabunge wakongwe wakijikuta wakitupwa nje.
Katika kikao hicho kilichoanza juzi na kumalizika jana mjini hapa, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, waliokatwa ni Mbunge wa Babati Mjini anayemaliza muda wake, Kisyeri Chambiri na mwenzake wa Babati Vijijini, Virajilal Jituson.
Wengine walioangukiwa na rungu la Kamati Kuu ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu ambaye alishinda katika kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali, Rita Mlaki na Mbunge wa Sikonge anayemaliza muda wake, Said Nkumba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kilisema kuwa hatua ya kufikiwa kwa uamuzi huo ni kutokana na wagombea hao kuhusishwa na tuhuma za rushwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, pamoja na baadhi yao kushinda na hata kukatiwa rufaa, lakini bado walionekana kuwa na makosa ya wazi ikiwamo ya kuhonga wajumbe kwa kuwashawishi ili wachaguliwe katika nafasi hiyo.
Katika mchakato huo, Jituson wa Babati Vijijini alipata kura 8,523 kati ya 32,073 zilizopigwa na aliyemfuatia alikuwa Daniel Sillo aliyepata kura 6, 222.
“Hali imekuwa tete kwa baadhi ya wabunge, hasa wa Babati Mjini na Vijiji ambao wote wameondolewa katika uteuzi na Kamati Kuu, unajua Chambiri ana tuhuma za rushwa na ripoti ya Takukuru ilisaidia sana kummaliza katika vikao hivi vya uteuzi.
“Ila mwenzake wa vijijini, Jituson yeye alilalamikiwa na wagombea wenzake na hata kumuhusisha na tuhuma za rushwa hali ambayo pia vilipatikana baadhi ya vielelezo dhidi yake.
“Ila kwa Rita Mlaki ni wazi hapa unaweza kusema kama kuna uonevu wa wazi kwani alishinda kura za maoni kupitia UWT kundi la NGO’s, lakini CC ikatumia hoja ya uwiano bara na Zanzibar.
“Badala yake wamemwondoa yeye aliyeshinda na kuteuliwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Hadija Abood ambaye yeye katika kundi hili sasa amepangwa na Mchungaji Getrude Lwakatare, hoja hii ya uzanzibari imetumika katika kundi hili tu haikugusa kundi la wafanyakazi wala walemavu,” alisema mtoa habari huyo ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake.
Katika kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi mwaka huu, Chambiri alishinda dhidi ya makada wengine saba wa chama hicho ambao walipinga matokeo hayo.
Katika mchakato huo wa kura za maoni, Chambiri alipachikwa jina la ‘ATM inayotembea’ kutokana na madai ya kugawa fedha kwa wapiga kura, madai ambayo hata hivyo aliyakanusha mara kwa mara.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Chambiri alikamatwa mchana na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) akiwa ndani ya ofisi za CCM Wilaya ya Babati Mjini.
Habari zaidi kutoka ofisi za Takukuru zinaeleza kuwa hatua ya kumtia mbaroni mbunge huyo ilitokana na kutafutwa kwake kwa zaidi ya siku tano baada ya kudaiwa kushiriki vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni.
Inadaiwa Chambiri alinusurika kukamatwa na maofisa wa taasisi hiyo katika Kijiji cha Kiongozi ambapo wapambe wake wawili walikamatwa wakiwashawishi wapiga kura kwa kuwapa fedha na kukutwa na kitita cha Sh milioni 12.5.
HABARILEO
Jitihada za Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo na ufugaji nchini, zimepata msukumo mpya kufuatia uamuzi wa kujengwa kwa maabara ya kisasa kabisa ya matumizi ya teknolojia ya vinasaba ya kuboresha mbegu za mimba za ng’ombe inayojulikana kama embryo transfer.
Maabara hiyo ya kisasa itajengwa katika eneo la Ranchi ya Mzeli, mkoani Tanga na kampuni ya nyumbani ya Overland Livestock Multiplication Unit and Embryo Transfer kwa kutumia teknolojia kutoka nchi ya New Zealand kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa ya Rachi (NARCO).
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Feisal Edha akifuatana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, mtaalamu kutoka New Zealand na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya NARCO alimwambia Rais Kikwete mwanzoni mwa wiki hii mjini Dodoma kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo, ambayo itakuwa ya pili ya aina yake katika Afrika Mashariki.
Maabara hiyo inawezesha ng’ombe bora ambaye ni mama bandia kupokea mbegu bora kutoka kwa ng’ombe bora mfadhili na kumlea hadi kutoa ndama wa kisasa kabisa ambao wanazaliwa kwa wingi na baadaye wanaweza kuuzwa kwa wananchi.
Edha alimwambia Rais Kikwete kuwa kwa kawaida ng’ombe huzaa ndama 13 katika maisha yake ya wastani wa miaka 13 hadi 16, lakini chini ya teknolojia hiyo, ng’ombe anaweza kutoa mayai kiasi cha 126 kwa mwaka ambayo yanaweza kupandikizwa katika teknolojia hiyo kwa wakati mmoja baada ya ng’ombe hao huingizwa katika joto.
Rais Kikwete alioneshwa kufurahishwa kwake na hatua hiyo, akisisitiza kuwa amekuwa akielekeza kuhusu umuhimu wa kuleta mageuzi katika mifugo ya Tanzania kwa miaka yote ya uongozi wake. “Nimewapenda na kuwaamini sana watu wetu wa mifugo, lakini hakuna jambo la maana wamefanya katika muda wote.
Nakushukuru Bwana Feisal kwa uamuzi wako huu na nataka kukuhakikishia kuwa kama watu wetu wanakuzungusha, wewe endelea tu na mimi niko yatari kukusaidia,” alisema Rais Kikwete.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos