MWANANCHI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtahadharisha mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa kuwa kampeni alizoanza kwa kuyatembelea makundi kadhaa zinaweza kutumiwa na maadui wa kisiasa kumdhuru.
Hata hivyo, wanasiasa wametakiwa kufuata ratiba ya kampeni kwa kuzingatia mwongozo wa Tume ya Uchaguzi (NEC) ili kulisaidia jeshi hilo kukabiliana na vitendo viovu.
Onyo hilo limetolewa ikiwa ni siku ya pili tangu Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Haji walipoanza kuwatembelea wananchi huku wakitumia usafiri wa umma.
Kwa kutumia staili hiyo, leo Lowassa akiwa na Duni Haji wametembelea maeneo ya Tandika, Tandale na Kariakoo jijini Dar.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema ziara iliyofanywa leo maeneo ya Swahili, Kariakoo zimesababisha mikusanyiko isiyo ya lazima na kusimamisha shughuli za maendeleo.
Baada ya CCM kuzindua kampeni zake mwishoni mwa juma lililopita viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, Chadema nacho kinajiandaa kufanya hivyo Agosti 29 maeneo hayohayo.
MWANANCHI
Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), kimekata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa majimbo ya Mlalo, Bumbuli, Ludewa na Peramiho yaliyotangazwa kuwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamepita bila kupingwa kwa madai kuwa waliotangaza hawana mamlaka hiyo.
Wakili wa Chadema, Peter Kibatala alisema tayari utaratibu wa kuandaa rufaa hizo umeshakamilika.
“Ninasimamia rufaa ya kesi tatu. Tunapinga wakurugenzi wa halmashauri kutangaza majimbo yao kuwa yana wagombea waliopita bila kupingwa wakati sheria haiwaruhusu kufanya hivyo.
“NEC pekee ndiyo wanaweza kusema lolote baada ya kusikiliza kilichoamuliwa na mkurugenzi,” Kibatala.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wagombea watano wa ubunge kupitia CCM wamepita bila kupingwa baada ya wawakilishi wa vyama vya upinzani kushindwa kujitokeza au kuwekewa pingamizi kutokana na makosa kadhaa ya kikanuni.
Mgombea wa Chadema Jimbo la Bumbuli, David Chanyezhea alisema baada ya kupokea barua ya kuenguliwa na mkurugenzi wa uchaguzi wilayani kwa maelezo kuwa amekosa vigezo, amekata rufaa NEC kupinga uamuzi huo.
Chanyezhea alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya jitihada za kumtaka ajiondoe kwenye kinyang’anyiro hicho na wapambe wa mgombea mwenzake wa chama kingine.
“Nimeshaandika barua ya kukata rufaa na kuituma NEC. Ninaamini haki itatendeka kwani sheria inaruhusu mtu kugombea udiwani na ubunge kwa wakati mmoja na wapo wabunge wa namna hiyo kwenye mabunge yaliyopita,” alidai mgombea huyo.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alisema kutokana na makosa hayo, ana imani kuwa NEC itakuwa makini na kutoa majibu sahihi dhidi ya rufaa hizo.
Alipoulizwa kuhusu mustakabali wa majimbo mawili yaliyosalia, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema tayari hatua zimeshachukuliwa kwa lile la Peramiho na la Nanyamba.
Mwalimu alisema hawawezi kulizungumzia Jimbo la Nanyamba kwa kuwa mgombea aliyesimamishwa alikuwa wa CUF.
HABARILEO
Watu nane wamethibitishwa kufariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine 262 wameambukizwa maradhi hayo katika mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro.
Waziri wa Afya na Usatwi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hadi kufikia jana, kwa mkoa wa Dar es Salaam, watu saba wamefariki na wengine wapatao 230 tayari wameambukizwa ugonjwa huo.
“Tangu ugonjwa huu uanze Agosti 15 mwaka huu, idadi ya wagonjwa walioripotiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 230 na vifo vya watu saba,” alisema Dk Rashid.
Dk Rashid alisema maeneo yalioathirika zaidi na ugonjwa huu kwa mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na maeneo ya Makumbusho, Kimara, Tandale, Manzese, Saranga na Magomeni.
Maeneo mengine ni Mwananyamala, Kibamba, Kigogo, Goba, Mburahati, Kinondoni na Kijitonyama kwa manispaa ya Kinondoni. Kwa upande wa manispaa ya Ilala, maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Buguruni, Majohe, Chanika, Sharifu Shamba na Tabata, wakati katika manispaa ya Temeke, maeneo yalioathirika ni Mtoni kwa Azizi Ally, Keko na Yombo Vituka.
Katika mkoa wa Morogoro, Dk Rashid alisema ugonjwa huo ulianza mkoani hapo Agosti 17 mwaka huu na hadi kufikia Agosti 24, mtu mmoja amefariki dunia na wengine 32 wameambukizwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Rufaro Chatora amepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali lakini amesema haina budi kuchukua hatua zaidi ili kudhibiti maambukizi yasiongezeke.
HABARILEO
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana alikuwa mstari wa mbele kunogesha kampeni za mgombea wa urais wa CCM, Dk John Magufuli, akisisitiza ni chaguo sahihi kwa Watanzania na kwamba hata upatikanaji wake ulikuwa sahihi kwa asilimia 100 na kwamba, yeye aliyekuwa mjumbe wa vikao hivyo ni shuhuda wa hilo.
Kutokana na ukweli huo, amesema hana kinyongo, ndiyo maana yuko mstari wa mbele kumnadi aweze kuwa Rais wa Tano wa Tanzania baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Katika Uwanja wa Nelson Mandela, Pinda alisema kuna baadhi wamesusa na hivyo haya yeye alipokosekana katika uzinduzi wa kampeni za Urais za CCM jijini Dar es Salaam, kuna waliompigia simu na kuhoji kwa nini hakuwepo.
“Mimi ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Kamati ya Maadili, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu. Nimeona nisiache kuja huku, maana Waswahili hawaachi kusema, unaona hata Waziri Mku kamsusia mwenzake, maana alikuwa naye katika kinyang’anyiro…Mimi ni muumini wa chama changu, kilichofanyika mpaka tukampata Magufuli nataka niwaambie ni halali asilimia 100,” alisema.
Alifafanua kuwa walichokuwa wakitafuta CCM ni kumpata mtu ambaye kwa wale waliokuwa katika kamati na vikao hivyo, wamekubaliana kuwa anaweza kuwavusha bila matatizo.
“Mimi nilikuwepo na nilikuja mkanidhamini na niliwaambia tulikuwa 42, ikaja 38 nikasema atabaki mmoja. Tumeletewa Magufuli, si mwingine si Pinda. Chama hapo kama ni kupiga, basi kimelenga shabaha. “Huyu baba ni mwadilifu na mchapakazi sana, ana huruma sana lakini kwa mambo yenye uongo, wakwepa kodi, wezi ni mkali sana…
Nilitaka kuja kuwathibitishia kuwa mimi nimeungana naye kwa asilimia mia,” alisema. “Juzi mtu mmoja alinipigia akasema mbona katika uzinduzi hukuwepo, nikamjibu kwa hiyo?” nikahoji. Akaongeza: “Tumepewa heshima ameanzia huku Katavi na Rukwa, namngoja huku.
Sisi barabara tumepata, mkoa wa Katavi tumepata wilaya na kata za kutosha, sasa zawadi ni kumpa kura”. Wapanda daladala Alisema anashangaa imekuwaje watu waanze kupanda daladala sasa kwenda Chanika na kwingineko Dar es Salaam na kuhoji; “Siku zote alikuwa wapi.
Anangoja moto umewaka ndio anapanda?” Magufuli Akizungumza katika mkutano huo, Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli alianza kwa kusalimia kwa karibu lugha kumi na kusema ataunda serikali ya mawaziri wachache, lakini kazi atakazowapa anahisi baadhi watakimbia.
Aliahidi kuhakikisha wafanyabiashara wadogo hawabugudhiwi, wakiwemo bodaboda na mamalishe na kuhakikisha wafanyabiashara wakubwa wanalipa kodi ili ihudumie wananchi.
NIPASHE
Aliyekuwa Waziri na Mambo ya Ndani na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, jijini Mwanza, Lawrence Masha, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na shitaka la kutoa lugha ya matusi dhidi ya maofisa wa Jeshi la Polisi na kisha kupelekwa selo katika gereza la Segerea.
Masha ambaye ni wakili wa kujitegemea alikamatwa juzi na kulala selo katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alifikishwa mahakamani hapo jana saa 4:20 asubuhi akiwa amevaa fulana la rangi nyeusi, suruali ya jinsi ya rangi ya bluu mpauko na sendozi za rangi nyeusi.
Alifikishwa mahakamani hapo na msafara wa magari saba ya jeshi hilo likiwamo la maji ya kuwasha akiwa pamoja na washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi mbalimbali.
Saa 8:40 asubuhi alisomewa shitaka moja linalomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema.
Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Wankyo Simon alidai kuwa, Agosti 24, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Oysterbay, mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alitoa lugha ya matusi dhidi ya Inspekta Msaidizi wa Polisi Juma Mshana na wenzake kituoni hapo.
Alidai Masha aliwatolea lugha ya matusi maofisa hao wa polisi, akinukuu maneno hayo: ‘Polisi ni washenzi, waonevu hamna shukrani, huruma wala dini’ na kusababisha uvunjifu wa amani.
Mshitakiwa Masha alikana shitaka hilo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na haukuwa na pingamizi la dhamana dhidi ya mshtakiwa.
Baada ya kusikiliza mashitaka hayo, Hakimu Lema alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi zinazotambulika ambao watatakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja kila mmoja.
Baada ya hakimu kuweka wazi dhamana kwa mshitakiwa, upande wa Jamhuri uliomba muda wa kuhakiki nyaraka za wadhamini wawili waliojitokeza kumdhamini, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, mwaka huu.
Hata hivyo, ilipofika saa 9:40 alasiri Masha aliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi makali wa polisi na kupelekwa katika mahabusu ya Gereza la Segerea kutokana na muda wa mahakama kufanyakazi kumalizika huku taratibu za dhamana zikiwa hazijakamilika.
NIPASHE
Serikali imesema zaidi ya Sh. bilioni 230 zimepotea katika kipindi cha mwaka uliopita kutokana na ajali za barabarani nchi nzima.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga alisema kiasi cha Sh. bilioni 230 zilipotea katika ajali zilizotokea kipindi hicho licha ya baadhi ya ajali hizo zingeweza kuepukika.
Katika semina hiyo ya kuwaelimisha madereva juu ya makosa ya kibinadamu yanavyochangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani, Konisaga alisema uzembe, ulevi, uchakavu wa barabara, ubovu wa magari ni miongoni mwa sababu hizo.
“Katika kipindi cha mwaka jana pekee Sh. bilioni 230 zilipotea kutokana na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani ambazo nyingi zimesababishwa na makosa ya binadamu,” alisema.
Awali akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa Usalama Barabarani na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA), Geofrey Silanda, alisema tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini zinaonyesha asilimia 75 za ajali za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu.
“Lakini pia asilimia 50 ya makosa hayo ya barabarani yanayohusiana na mambo ya kibinadamu yanafanywa na madereva,” Silanda.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Mkoani Mwanza (Uwamata), Shabani Wandiba, aliitupia lawama serikali kuwa ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa kusababisha ajali za barabarani kutokana na kupanga muda wa magari kusafiri bila ya kuangalia umbali.
“Ratiba inapangwa bila kuangalia umbali, mwendo kulingana na alama za barabarani, mfano mwendo wa kilomita 80, 50, 20 kwa saa pamoja na muda wa chakula yote hayo ni miongoni mwa vyanzo vya ajali,” Wandiba.
NIPASHE
Walimu zaidi ya 2,000 mkoani Mwanza wanaidai serikali malimbikizo ya mishahara pamoja na gharama za upandishwaji madaraja.
Aidha, baadhi ya walimu wanaidai serikali fedha za likizo na matibabu na wengine wakisubiri kupandishwa madaraja.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) mkoani Mwanza, Sibora Kisheri, alisema wanaungana na Rais wa chama hicho taifa, Gratian Mkoba (pichani), kuitaka serikali kuwalipa madeni yao kabla ya Septemba mwaka huu.
Hata hivyo, Kisheria hakutaja kiasi cha fedha ambacho walimu wanaidai serikali mkoani humo.
Alisema wanaunga mkono kauli ya Mkoba ya kuitaka serikali kulipwa madeni yao kabla ya Septemba, mwaka huu pamoja na kwamba Rais Jakaya Kikwete alishaahidi kuwalipa wakati mkutano mkuu wa CWT uliofanyika mkoani Arusha.
“Mwanza tupo tayari kupokea maelekezo yoyote ya CWT makao makuu na kuyaunga mkono, tunataka haki yetu ilipwe kwa wakati maana walimu tunaathirika na tunafanya kazi katika mazingira magumu,” alisema Kisheri.
Naye Katibu wa CWT Mkoa wa Mwanza, Said Mselem, aliiomba serikali wakati wa kupanga bajeti, walimu wawe wanahusishwa ili inapopitishwa waelewe kilichopitishwa.
alisema wakati wa kupitisha bajeti wamekuwa hawahusishwi hivyo kuwawia vigumu kujua kipi kilichopitishwa ili utekelezaji usipofanyika waweze kufuatilia jambo ambalo hata katika sheria zao zinaeleza hivyo.
Mselem alisema CWT mkoa wa Mwanza hawatakubali kuona mwalimu yeyote mkoani humo anahamishwa na kupelekwa eneo jingine bila kulipwa gharama za uhamisho.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha, Dk. John Magufuli kugombea urais kupitia chama hicho kwa kumuamini kuwa atasimamia vizuri rasilimali za nchi ikiwamo gesi na madini kwa manufaa ya taifa na Watanzania.
Akizungumza jijini Arusha juzi wakati akifungua mkutano wa nne kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-Tamisemi), Bodi ya Mfuko wa Barabara na wadau wa barabara, Rais Kikwete alisema ana amini endapo Magufuli atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania wa Kati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, atasimamia vizuri rasilimali hizo kutokana na kuwa msomi mzuri na kuwa na uchungu wa maendeleo ya taifa lake na watu wake.
“Huyu Magufuli siwezi kujilinganisha naye, mwenzangu ana PhD ya kusomea na ameifanyia utafiti kwenye ganda la korosho jinsi ya kutumia mafuta yake kunufaisha nchi kwenye maendeleo ya taifa, ila mimi nina PhD ya heshima, hatuwezikuwa sawa, hivyo nina imani naye sana,” alisema.
Rais Kikwete alisema CCM imemchagua kwa makusudi Dk. Magufuli kwa ajili ya kuhakikisha nchi inaneemeka na rasilimali ya gesi ambayo hadi sasa uwekezaji wake umegharimu dola za Marekani bilioni 20 hadi 30 mpaka kuanza uvunaji wake.
“Naomba tusifanye mchezo na rasilimali hii, ndiyo sababu mimi nimehakikisha tunakuwa na sheria nzuri ya kusimamia vizuri rasilimali hii isije ikatupeleka kubaya, japo baadhi ya watu walisema naharakisha ya nini, ila najua kuna nchi walipata mafuta ila watu wakubwa wakakopa kwa kujivunia mafuta hayo na matokeo yake hadi sasa wanalipa madeni na nchi, mimi sikutaka hayo,” alisema.
Alisema ni vizuri rasilimali kama hizo zikawekewa utaratibu wa kuzilinda kabla ya kuanza uvunaji wake na kwamba baada ya miaka michache ana amini Tanzania itakuwa nchi tajiri kwa kuuza gesi nje kwenye masoko makubwa.
Rais Kikwete alisema Dk. Magufuli kutokana na usomi na uchapakazi wake, kila wizara aliyowekwa aliongoza vizuri na kupatikana mafanikio makubwa, hivyo akiwa Rais atafanya mambo mengi makubwa zaidi kwa manufaa ya taifa na wananchi wote.
MTANZANIA
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema ikiwa atachaguliwa kuongoza Serikali ya awamu ya tano atahakikisha anapambana na watendaji wala rushwa serikalini.
Amesema watendaji hao ndiyo wamekuwa wakikwamisha juhudi za Serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi hali inayosababisha malalamiko ya wananchi.
Kauli hiyo aliitoa jana kwa nyakati tofauti alipohutubia wananchi katika mikutano ya kampeni katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Dk. Magufuli pia aliahidi kufuta utaratibu wa wakulima kukopwa mazao yao na serikali.
Alisema utaratibu huo umekuwa hauleti tija kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakirudi nyuma kwa maendeleo badala ya kusonga mbele.
“Hakuna jambo linaloniudhi kama wakulima kukopwa mazao yao, ninajua mikoa ya Katavi hasa Majimoto na Nkasi ni wakulima wazuri wa mahindi na mpunga ila nimekuwa siridhiki na namna watu wanavyokopwa mazao yao.
Mgombea huyo wa urais aliwaahidi wananchi kuwa ikiwa atafanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu wa tano, kuanzia Februari mwaka kesho elimu ya msingi hadi sekondari itakuwa bure kwa watoto wote.
“Fedha zipo lakini kuna wala rushwa wachache ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali, mimi ninasema nichagueni nikapambane na watendaji wabovu ambao hawafai kwa sasa.
“Ninajua wazi kero kubwa ni barabara na ninachopenda kuwaambia wakandarasi waliposikia nimeteuliwa kuwania urais hivi sasa wote wamerudi kazini licha ya wengine hawaidai serikali, na ni lazima barabara ya Nkasi-Mpanda ikamilike kwa wakati.
Dk. Magufuli alisema ingawa Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa changamoto zimebaki na akaahidi kuzikamilisha kwa wakati.
“Ninashangazwa sana leo tuna kero ya maji sasa inafanyika wiki ya maji wakati maji yenyewe hayapo, wiki ya Ukimwi dawa hakuna, wiki ya maziwa lakini viwanda na maziwa hakuna, kwangu ninataka kurekebisha hili kwa vitendo,” alisema.
Alisema moja ya ahadi yake kupitia ilani ni kuhakikisha ujenzi wa zahanati na huduma ya umeme kwa kila kijiji katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake.
“Ilikuwa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere (Julius), mzee Mwinyi, Mkapa, Rais Kikwete na awamu ya tano ninawaomba mnikabidhi mimi kwanini zamu yangu kuwatumikia Watanzania,” alisema.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos