Vitu vingi sana vimebadilika kwenye kikosi cha Real Madrid tangu kilipoanza kunolewa na kocha Rafa Benitez ambaye alichukua rasmi mikoba ya Mtaliano Carlo Ancelotti ambaye alifukuzwa baada ya msimu uliopita ambao ulimalizika bila ya taji lolote .
Hata hivyo moja ya mambo ambayo yamedhihirika wazi ni jinsi ambavyo Benitez anavyopenda kutoa fursa kwa wachezaji wake wote kucheza akiwatumia wachezaji zaidi ya 15 kwenye mechi za mashindano mbalimbali ambayo Madrid inashiriki kwa msimu huu .
Jumla ya wachezaji 22 kati ya 23 wa kikosi kizima cha kwanza cha Real Madrid wamepata nafasi ya kucheza angalau mechi moja nzima ya dakika 90 huku mchezaji mmoja pekee ambaye ni Kiko Catilla akiwa hajacheza mechi hata moja .
Katika kikosi kizima cha Real Msimu huu ni wachezaji wawili tu ambao wamecheza kwenye mechi zote msimu huu nao ni Cristiano Ronaldo na kipa Keylor Navas huku mchezaji Denis Sherychev akiwa amecheza dakika 19 katika mechi mbili .
Rafa Benitez amekuwa akipenda kuzungusha nafasi za kikosi chake cha kwanza akitofautiana na makocha wengine ambao wamekuwa na kawaida ya kuwa na kundi Fulani la wachezaji ambao hucheza mechi nyingi kuliko wengine .
Real Madrid ambayo juzi ilishinda mchezo wake dhidi ya Malmo kwenye ligi ya mabingwa itapambana na mahasimu wao wa jadi Atletico Madrid katika muendelezo wa ligi ya Hispania jumapili hii .