NIPASHE
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema CUF inaendelea kutafuta haki ya Wazanzibar ya kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi ili mshindi ajulikane na hatimaye kuapishwa.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika makao makuu ya CUF Mtendeni juzi, baada ya kurudi safari yake ya kuonana na rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Aliwaambia wanachama hao kuwa hakuna kurudi nyuma katika kudai haki yao kwa njia ya amani na utulivu ili matokeo yatangazwe na mshindi wa urais ajulikane.
“Niwahakikishieni vijana na wanachama wa CUF kuwa hakuna kurudi nyuma, tunaendelea kudai haki yetu na tunashukuru dunia nzima inatuunga mkono kwa hili,”alisema Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Alisema kuwa wapinzani wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mpango wao ni kutaka kuendelea kuwa katika madaraka wakijua kuwa muda wa Dk. Ali Mohammed Shein wa kukaa madarakani umekwisha, lakini wanang’ang’ania aendelee kinyume cha Katiba.
Aidha, alisema kuwa hakuna dawa yoyote ya kumaliza mgogoro ulipo Zanzibar isipokuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu ili mshindi ajulikane na kuapishwa.
“Wanaosema kuwa uchaguzi urejewe waachieni wenyewe, sisi katika CUF hakuna msamiati huo kwa sasa kurejea uchaguzi, huo ndio msimamo wetu,” alisisitiza Maalim Seif.
Alisema kuwa kwa uwezo wa Mungu haki yao wataipata na kuwataka vijana kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kutunza amani ya nchi kwa kutokubali kuchokozeka. Alisema CUF na viongozi wake hawatakubali kuwa chanzo cha kuvuruga amani ya nchi na wataendelea kuhubiri amani wakati wote.
Mvutano wa kisiasa unaoendelea Zanzibar ulisababishwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar wa rais na wawakilishi Oktoba 28, kwa madai kuwa ilibaini kuwapo kwa kasoro kadhaa kisiwani Pemba.
Hata hivyo, waangalizi wa nje na ndani wameeleza kushangazwa ha hatua ya Jecha, kwa kuwa hawakushuhudia kasoro zozote hadi walipotoa ripoti ya awali.
Aidha, asasi za nchini na mataifa kadhaa yakiwamo Uingereza, Ireland na Marekani yameshatoa taarifa ya kushangazwa na uamuzi wa Jecha na kushauri mchakato wa kutangaza matokeo uendelee.
NIPASHE
Kundi la watu wanaoaminika kuwa ni majambazi wakiwa na silaha mbalimbali kama mapanga na marungu, juzi waliteka magari katika kijiji cha Igogo,Wilaya ya Igunga huku wakiimba ‘hapa kazi tu’.
Baadhi ya madereva waliokumbwa na dhahama hiyo, walidai kuwa baada ya kusimamishwa na majambazi hao waliwashambulia kwa marungu na papa la panga huku wakiwaamrisha watoe fedha na simu za mkononi huku wakitamka kila wakati kauli mbiu iliyotumika kwenye kampeni ya hapa kazi tu.
Mmoja wa madereva hao alisimulia na kusema alikumbana na mkasa huo usiku wakati akitokea hospitali ya rufaa kupeleka wagonjwa.
“Wakati wakitushambulia kwa mapanga , majambazi hao walikuwa wakisema ‘hapa kazi tu, toeni pesa na simu'” alisema.
MWANANCHI
Mjadala kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na Jecha, umechukua sura mpya, baada ya mmoja wa watoto wa Rais wa zamani, Dk. Amani Abeid Karume, kuibuka na kufichua kile anachoamini kuwa ni sababu ya utata uliojitokeza sasa.
Mtoto huyo ni Mwanasheria, Fatma Karume, ambaye akiwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, waliuambia umma kupitia mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha televisheni jijini Dar es Salaam juzi kuwa sababu mojawapo ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni muundo wa uongozi unaomruhusu rais wa visiwa hivyo kuwa mmoja wa wajumbe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akifafanua, Fatma alisema kuwapo kwa nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Mawaziri kunaibua mgongano inapotokea mshindi wa upande mmoja akiwa ni wa kutoka chama kingine na hiyo ni sababu mojawapo wanayoamini kuwa imechangia kufutwa kwa uchaguzi na pia kukwaza ukuaji wa demokrasia visiwani humo.
Alisema ni dhahiri hali huwa ngumu kwa baraza la mawaziri linaloundwa na watu wa itikadi ya chama kimoja kuchanganyika na mwingine mwenye itikadi tofauti, hasa katika mazingira ya kuwa na usiri katika baadhi ya mambo na kwamba, hilo huchangia kusuasua kwa maendeleo ya kidemokrasia visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, ili kuondokana na mgogoro kama uliopo sasa, Fatma alisema ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini na kwingineko barani Afrika kuzingatia sheria na katiba zilizopo.
Awali, ilisisitizwa na wanasheria hao kuwa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Zec peke yake, haukuzingatia sheria na katiba na ndiyo maana sasa kumeibuka mgogoro wa kikatiba kwani kifungu kinachotumika kuhalalisha hoja ya kuendelea kubaki madarakani kwa Dk. Shein kimekuwa kikitafsiriwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa.
Akielezea zaidi, Awadh alisema hakuna kifungu chochote kinachomruhusu Jecha kufuta uchaguzi na ndiyo maana hadi sasa hakuna mtu aliyethubutu kutaja kwa uwazi ni sheria ipi imempa nguvu mwenyekiti huyo wa Zec kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
NIPASHE
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, ametoa msamaha kwa wafungwa 4,160 ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuaga na kumpisha mrithi wake, Rais Dk. John Magufuli.
Kati ya wafungwa hao, 864 wameachiwa huru na 3,293 kupunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu iliyobaki ya kifungo chao.
Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ilieleza kuwa, Kikwete alitumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ni mategemeo ya serikali kwamba wafungwa watakaochiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.
Pia ilieleza kuwa msamaha huo utawahusu wafungwa wenye magonjwa kama upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi), kifua kikuu na saratani ambao wako katika hali mbaya kwa kuthibitishwa na jopo la madaktari chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Ilisema msamaha huo utawahusu wafungwa wenye umri wa kuanzia miaka70 na kuendelea.
Kundi lingine la msamaha litawahusu wafungwa wa kike waliongia gerezani wakiwa na ujauzito pamoja na wanawake waliongia gerezani na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Kadhalika, msahama huo utawahusu wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili uliothibitishwa pia na jopo la waganga.
Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wenye makosa makubwa kama waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani, waliojihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulenya, waliohukumiwa kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.
Wengine wasionufaika na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na silaha, risasi au milipuko isiyo halali, kunajisi, kubaka, kulawiti, kuwapa mimba wanafunzi, makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo na wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii.
Wengine ni waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais na bado wangali wakiendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki, wanaotumika vifungo kwa makosa ya kutoroka wakiwa chini ya ulinzi, wanaotumika vifungo kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha serikalini, wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za serikali na ujangili, waliohukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya mashambulizi na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.
MWANANCHI
Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walikuwa miongoni mwa makada wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao hawakuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais John Magufuli.
Ni kawaida kwa mawaziri wakuu wa zamani kuwa sehemu ya wageni rasmi kwenye sherehe hiyo ya kihistoria, lakini jana wawili hao, ambao walitangazaa kuihama CCM mwezi Julai na kuhamia kambi ya upinzani, hawakuwamo kwenye jukwaa la wageni rasmi.
Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema vyama vinavyounda Ukawa havitahudhuria sherehe hizo kwa kuwa vinapinga jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa na kuwataka wananchi wapenda mabadiliko na wapenda haki, viongozi na wabunge wa chama hicho kutohudhuria shughuli hiyo.
Ukawa ilimsimamisha Lowassa kugombea urais na kwa mara kwanza mgombea wa upinzani alipata kura milioni 6.07, ambazo ni karibu ya mara tatu ya kura alizopata Dk Willibrod Slaa mwaka 2010.
Hata hivyo, viongozi wa Ukawa walipinga matokeo yaliyokuwa yakitangazwa, wakisema ni tofauti na yale yaliyokusanywa na mawakala wao na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha utangazaji.
Lowassa, ambaye alikuwa akipeperusha bendera ya Chadema, alikuwa akiungwa mkono na NLD, NCCRMageuzi na CUF ambavyo vinaunda Ukawa.
Lowassa alihamia Chadema baada ya CCM kutompitisha kuwa mgombea wa urais, baadaye kundi la makada kutoka CCM lilimfuata, akiwamo Sumaye, Dk Makongoro Mahanga, aliyekuwa Waziri wa Kazi na Ajira, na Kingunge NgombareMwiru, mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani.
Mbowe alisema juzi kuwa sababu kubwa ya Ukawa kususia sherehe hizo ni kutaka kuonyesha nchi na dunia nzima kuwa hawakubaliani na mchakato wa uchaguzi, hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mwenyekiti wa NEC akishayatangaza, hakuna mahali pa kuyapinga.
“Watawala wamechezea haki ya Watanzania ya kupiga kura. Kura zimehesabiwa kama karatasi za kawaida tu. Matokeo ya wagombea wetu yamehujumiwa waziwazi. “Safari hii hujuma hazikuwa kificho.
Kila mtu amejionea matokeo yaliyokuwa yanatangazwa na Jaji Lubuva si yale ambayo yalikuwa yamebandikwa vituoni,” alisema Mbowe juzi.
Ukawa pia ililalamikia kile walichoita “mchezo mchafu” waliofanyiwa wagombea wao wa ubunge katika majimbo mbalimbali, ikieleza kuwa walitangazwa washindi ambao hawastahili.
Hata hivyo, juzi jioni Naibu Katibu Mkuu wa CUFBara, Magdalena Sakaya aliwaeleza wanahabari kuwa hawakuwa wamepata mwaliko wowote wa kuhudhuria sherehe hizo.
Katika hotuba yake fupi ya shukrani, Dk Magufuli aliwashukuru wagombea wenzake wa urais, akisema wamempa changamoto kubwa na amejifunza mengi kutoka kwao na kuwataka wapinzani washirikiane katika kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo
MWANANCHI
Kila mzazi anapokaribia kupata mtoto, moja ya mambo muhimu ambayo hufikiria juu ya jina la kumpatia baada ya kujifungua na mtoto kuishi duniani.
Wazazi wengi huchukua muda kufikiria ni jina gani zuri la kumpa mtoto wao. Kuna wakati baadhi ya wazazi hufikia hatua ya kuvutana kuhusu jina tu.
Kuvutana huko kunatokana na umuhimu wa jina kwa sababu inaaminika kila jina lina maana yake na tabia zake zitaakisiwa nalo.
Kuna majina ambayo hupendwa sana kutokana na dhana kwamba watu wanaopewa majina hayo huwa na tabia nzuri, upeo mkubwa, uvumilivu na wengine bahati.
Je, ikitokea unabahatika kupata mtoto wa kike uliyemtafuta kwa muda mrefu, utampa jina gani? Huenda jina Janeth likawa miongoni mwa matatu au 10 utakayoorodhesha ili kuchagua moja la kumpa binti yako.
Kama halitakuwapo basi fanya mpango wa kuliweka kwa sababu jina hilo ndiyo habari ya mjini kwa sasa.
Kwa nini jina la Janeth ni habari ya mjini? Siku Dk John Magufuli alipopitishwa na CCM kuwania nafasi ya urais, baadhi ya watu walidai ikiwa angepata nafasi hiyo Afrika Mashariki ingeongeza idadi ya wake wa marais wenye majina ya Janeth.
Imekuwa hivyo, mke wa Rais Magufuli aliyeapishwa jana anaitwa Janeth. Mke wa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni anaitwa Janet Museveni, na mke wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame anaitwa Jeanette.
Licha ya kwamba jina la mke wa Kagame linaandikwa tofauti na mengine, lakini matamshi ya majina hayo ni sawa.
Kwa mujibu wa kamusi ya Encyclopaedia jina la Jeannette, asili yake ni Ufaransa ndiyo maana linaandikwa tofauti na Janeth ambalo asili yake ni Scotland.
Kama hujui wakati jina Janeth hupewa mtoto wa kike kinyume cha jina hilo ambao hupewa mtoto wa kiume ni John.
Kwa hiyo majina ya Janeth na John Magufuli yameshabihiana vilivyo. Kutokana na utuki huo majina ya wake za marais hao sasa yamekuwa habari ya mjini.
Kuna baadhi ya watu wanatamani kuwapa majina watoto wao kwani huenda wakawa ‘ma First Lady’ watarajiwa.
Gumzo kwa sasa au watu wengi wanahoji iwapo marais hao watakutana wakiwa na wake zao, likataitwa jina hilo, itakuwaje?
Maana ya jina Janeth Kwa mujibu wa kamusi ya tafsiri ya majina, jina Janeth (Kiebrania) ambalo asili yake ni Uingereza linamaanisha Mungu ni mwenye neema.
Sifa za wanawake wenye jina hilo zimedadavuliwa zaidi na tovuti ya ‘sevenreflections’. Tovuti hiyo inawaelezea wanawake wenye jina hilo kuwa ni waaminifu, wema, wenye vipaji na wavumbuzi wa mambo.
Wanawake wenye majina hayo ni jasiri, wavumilivu, wabunifu, wadadisi, wanafahamu nini wanataka, siyo tegemezi na viongozi wazuri.
Janeth Magufuli Kitaaluma ni mwalimu. Alikuwa anafundisha Shule ya Msingi Mbuyuni masomo ya Jiografia, Historia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Lakini ameacha kutokana na wadhifa huo mpya aliopata mumewe. Hata hivyo, hakuwa maarufu wakati alipokuwa anafundisha shuleni hapo licha ya kuwa mke wa waziri mchapakazi na sasa rais.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela anamzungumzia kama mwalimu mchapakazi na anayefahamu majukumu yake, mwenye upendo, mnyeyekevu na asiye na makuu, sifa ambazo zinaendana na jina lake.
Janet Museveni Licha ya kuwa Mke wa Rais Museveni tangu mwaka 1986 mumewe alipoingia madarakani, pia ni mwanasiasa, na ni Waziri wa Karamoja.
Jeannette Kagame Alipata wadhifa wa mke wa rais tangu mwaka 2000, Kagame alipoingia madarakani hadi sasa akiwa pia mwanaharakati, mwanzilishi wa taasisi ya Imbuto inayosaidia katika shughuli za maendeleo katika sekta ya afya, elimu na uchumi.
Mwanamke mwingine maarufu duniani mwenye jina hilo ni Janeth Jagan, aliyekuwa Rais wa Guyana kati ya mwaka 1997 na 1999.
MWANANCHI
Rais John Magufuli amesema ana deni kubwa kwa Watanzania baada ya wananchi kuonyesha imani kwake, huku akiwaambia wapinzani kuwa uchaguzi umekwisha na yeye ndiye Rais.
Katika hotuba yake ya kushukuru ya takriban dakika 10 baada ya kuapishwa, Dk Magufuli alisema ana kazi kubwa ya kuendeleza Taifa baada ya wananchi kuonyesha imani kwake huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii kutekeleza ahadi alizotoa kwenye kampeni.
“Nina deni kubwa la kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania,” alisema Dk Magufuli mbele ya maelfu ya watu waliojitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru kushuhudia tukio hilo la kihistoria la kumsimika Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
“Ninatambua kwa dhati kwamba tuna jukumu kubwa la kuwafanyia kazi Watanzania. Tunawaomba wote katika dini mbalimbali tumtangulize Mungu na kutuombea ili tutekeleza tuliyo yaahidi.”
Katika hotuba hiyo, Dk Magufuli, aliyegombea urais kwa tiketi ya CCM, hakuvibeza vyama vya upinzani na badala yake akavitaka kushirikiana naye kuendeleza Taifa.
“Na kwa ndugu zangu wa vyama vya upinzani ambao kwa bahati nzuri wengi wako hapa. Tutafanya kazi kwa ajili ya kuliendeleza Taifa, uchaguzi umekwisha.
Rais ni John Pombe Joseph Magufuli, hapa kazi tu,” alisema Rais Dk Magufuli huku akishangiliwa. “Nchi yetu daima ni kubwa kuliko vyama vyetu, mapenzi yetu na matakwa yetu.
Uchaguzi Mkuu umekwisha, sote tushikamane kama watu wa taifa moja kuijenga nchi na kusonga mbele. Ndiyo maana nimekuwa nikisema ‘hapa kazi tu’, lakini tutangulize amani na kumtanguliza Mungu.
” Pia alikuwa na ujumbe kwa wagombea walioshindana naye kuwania urais. “Ninyi mlikuwa washindani wenzangu, siyo wapinzani wangu maana sote tulikuwa na lengo la kujenga nchi moja,’’ alisema Dk Magufuli. “Ninawashukuru kwa changamoto mlizotupa.
Nimejifunza mengi kutoka kwenu. Lakini nimejifunza mengi mema ambayo tutayafanyia kazi ili kujenga Tanzania bora. Nawashukuru pia wananchi kwa kunichagua.”
Alisema kutunukiwa kwake ni ushindi kwa Tanzania kwa kuwa yeye ndiye ameshinda. Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Chato, pia aliwapongeza wabunge wateule, akiwaahidi kushirikiana nao.
“Tumepokea dhamana hii kwa unyenyekevu mkubwa sana. Tunatambua wajibu na deni kubwa la kutekeleza ahadi tulizotoa kwa Watanzania. Tutafanya kazi kwa juhudi na maarifa yetu yote kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
“Ninataka niwahakikishie, nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote kwa kumtanguliza Mungu mbele ili yale tuliyoyaahidi tuyatimize bila kubagua vyama vyetu, dini zetu wala makabila yetu. Sasa ni kazi tu.”
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na marais wote wastaafu pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, isipokuwa Edward Lowassa, aliyeshika wadhifa huo kwa miaka miwili (2005 08), na Frederick Sumaye, ambaye alishika wadhifa huo kwa kipindi chote cha miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Tatu.
Wawili hao waliihama CCM mwezi Julai, Lowassa akijiunga na Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais, na Sumaye akijiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi bila ya kutaja chama.
Dk Magufuli aliwashukuru marais hao kwa kuchangia safari yake ya kuelekea Ikulu kwa vipindi tofauti na hatimaye kumpa nafasi ya kugombea urais.
Alimshukuru Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwa kumuongoza na busara zake, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa kumuibua kwa kumpa unaibu Waziri wa Ujenzi akiwa na umri wa miaka 35, na Jakaya Kikwete kwa kumuamini zaidi na kumpa uwaziri ambao alisema anaamini ndiyo leo umempa urais.
“Mimi ni nani hata wanione na kunipa nafasi hii,” alisema Dk Magufuli ambaye muda mwingi wa hotuba yake alizungumza kwa unyenyekevu.
JAMBOLEO
Saa chache baada ya kuapishwa kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli amemteua George Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amesema Rais Magufuli atamwapisha mwanasheria Masaju kesho asubuhi ili kuanza majukumu yake mara moja kwa mujibu wa sheria.
Aidha Balozi Sefue amesema kuwa, Rais Magufuli ameitisha rasmi kikao cha kwanza cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitakachoketi Novemba 17, mwaka huu.
Katibu Mkuu kiongozi amesema Rais Magufuli atarajiwa kupendekeza jina la Waziri Mkuu ambalo litawasilishwa katika bunge hilo jipya Novemba 19 ili lipigiwe kura.
HABARILEO
Rais Dk John Magufuli jana baada ya kuapishwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam alipokewa kwa shangwe na vifijo na wafanyakazi wa Ikulu eneo la Magogoni majira ya saa 7.30 mchana.
Wafanyakazi hao walijipanga kuanzia geti la kuingilia Ikulu upande wa Bahari ya Hindi ambako alishuka nje ya geti hilo na kuanza kutembea kwenye zulia jekundu lililotandazwa kuanzia geti hadi mlango wa kuingia ndani.
Magufuli alikuwa ameongozana na mke wake, Janeth na walikuwa wakiwapungia mikono wafanyakazi hao waliokuwa wakimuimbia nyimbo mbalimbali za kumkaribisha.
Alipowasili ndani ya Ikulu, alielekea moja kwa moja hadi ofisini na kuanza kazi jana hiyo hiyo kabla ya kujumuika na wageni kwa ajili ya chakula cha mchana.
Saa 9.30 alasiri aliungana na wageni mbalimbali kwa ajili ya chakula cha mchana ambacho kilihudhuriwa na marais mbalimbali akiwamo Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Wengine ni Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, lakini Rais wa Rwanda, Paul Kagame hakuwapo katika hafla hiyo huku nchi nyingine nyingi zikiwa zimewakilishwa na wawakilishi wao.
Baada ya chakula cha mchana, Dk Magufuli alipiga picha kwa awamu na viongozi mbalimbali wa nchi hizo na viongozi wengine mbalimbali ambao walikuwa wamehudhuria kuapishwa kwake. Alipiga picha ya pamoja na Rais Kenyatta na mpinzani wake wa kisiasa nchini Kenya, Raila Odinga ambaye ni rafiki wa siku nyingi wa Rais Dk Magufuli.
TANZANIA DAIMA
Muhubiri wa kimataifa nabii maarufu duniani Temipote Balogun maarufu kama TB Joshua ameacha maswali baada ya kushindwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa awamu ya tano Dk.John Magufuli.
TB Joshua aliwasili nchini November 03 kwa ndege binafsi na kupokewa na Dk.MAGUFULI pamoja na Mbunge mteule Mwigulu Nchemba katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere,Dar es salaam.
Baada ya kuwasili alifanya mazungumzo ya faragha na Dk.MAGUFULI pamoja na rais mstaafu Jakaya Kikwete kisha kufanya mazungumzo zaidi ya saa tatu na Edward Lowassa.
Ujio wa nabii huyo ulionekana kama amekuja kwa ajili ya kuapishwa kwa Dk.Magufuli lakini huku baadhi ya wananchi wakifurahishwa na ujio wake na kuamini ni fursa pekee ya kukutana naye na kufanya maombi akiwa hapa nchini.
Baadhi ya watu walisema waliamua kwenda uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kumuona nabii huyo lakini haikuwa hivyo na hawakufahamu kwa nini hakuhudhuria sherehe hizo.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyeza hapa >>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.