MTANZANIA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani ujumbe wenye maudhui ya ubaguzi ulioandikwa kwenye bango lililobebwa na mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mawasiliano na Umma wa CCM, Daniel Chongolo, ilieleza kwamba chama hicho kimesikitishwa na ujumbe huo na kuwaomba radhi Watanzania.
“Tumesikitishwa sana na ujumbe huo uliokuwa katika bango hilo, CCM kinaomba radhi kwa ujumbe huo, kinapinga na kinakemea kabisa fikra, hisia na mitazamo yoyote yenye maudhui ya kibaguzi.
“Ujumbe huo si tu kuwa una maudhui ya kibaguzi, bali pia unaenda kinyume kabisa na falsafa na shabaha ya waasisi wa Mapinduzi hayo matukufu ya mwaka 1964 na unapingana na misingi na itikadi ya CCM inayohimiza umoja na mshikamano wa kitaifa,” alisema Chongolo katika taarifa yake.
Hatua hiyo ya CCM imekuja baada ya wananchi mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kulaani bango hilo ambalo walionya kuwa halina nia njema na mshikamano wa Taifa.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema siasa za namna hiyo hazifai na zinapaswa kulaaniwa na kila mpinga ubaguzi nchini.
“Nitashangaa sana kama wakubwa CCM hamtaomba radhi kwa siasa hizi mbaya kabisa ‘What will be the stop’,” alisema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.
Kutokana na tafrani hiyo ya ubaguzi, nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani kile walichodai chembechembe za ubaguzi wa aina yoyote visiwani humo.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Mawasialino wa chama hicho, Tumaini Makene, ilieleza kwamba Chadema kwa kusimamia misingi ya utaifa hasa haki, uadilifu, utu, umoja na uzalendo haiko tayari kuona Taifa linafikishwa huko na hata kuhatarisha maisha ya jamii nzima ya Watanzania.
“Chadema tunalaani na kupinga kwa nguvu zote mipango, mikakati, tabia na chembechembe za ubaguzi wa aina yoyote, ukiwemo huu wa kisiasa ambao sasa unaanza kusakafiwa kwa ubaguzi wa rangi.
“Kwa sababu tunaamini wanaobeba ajenda hii hawataishia hapo bali watazidi kutugawa Watanzania pia kwa ukanda, ukabila, udini kama wamekuwa wakijaribu kuchochea,” alisema Makene.
Kutokana na kauli hiyo, alisema wanamkumbusha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, kuhakikisha anawachukulia hatua wale wanaoeneza chuki na hatari ya kuvurugika kwa amani kwa ujumbe wa kibaguzi.
MTANZANIA
Mwili wa marehemu Leticia Nyerere unatarajiwa kusafirishwa kutoka Marekani kuja nchini kesho kwa ajili ya mazishi yaliyopangwa kufanyika katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
John Shibuda ambaye ni msemaji wa familia ya Musobi Mageni, alisema kuwa mwili wa marehemu Leticia utasafirishwa kutoka Marekani alipofariki dunia na baadaye utaagwa katika nyumba ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Msasani jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa.
“Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kuelekea Musoma siku ya Ijumaa kwa ajili ya mazishi na suala lililokuwa limechelewesha ni pamoja na kupatikana haraka cheti cha kifo nchini Marekani,” alisema Shibuda.
Naye Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa aliyekwenda kutoa salamu za pole nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani, aliwaasa ndugu na jamaa wa marehemu kuendelea kumwombea marehemu huku akisisitiza kuwa Leticia alikuwa ni mchapakazi wakati alipokuwa ni mbunge.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Leticia aliyewahi kuwa mbunge wake katika Bunge lililopita.
Taarifa ya Chadema iliyosainiwa na ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene ilisema: “Tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki katika wakati huu mgumu wa kuondokewa na mpendwa wao.
“Mwenyezi Mungu awatie moyo wa ujasiri na subira katika wakati huu mgumu wa majonzi ya msiba huo.”
Taarifa hiyo ya Chadema ilisema kama chama watamkumbuka Leticia kwa mchango na ushiriki wake wakati wote alipokuwa mwanachama wao huku akiwa miongoni mwa watu waliopata fursa za kuwa wabunge kupitia chama hicho.
Leticia ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu katika Bunge la 10, alifariki dunia Januari 9 mwaka huu katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo MaryLand nchini Marekani ambako alikuwa amelazwa tangu mwishoni mwa mwaka jana akitibiwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Aliolewa na mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere mwaka 1996 na kufanikiwa kupata watoto watatu ingawa baadaye walitengana na kuhamia nchini Marekani ambako alichukua uraia na kuishi kabla ya kurejea nchini ambapo mwaka 2010 aliteuliwa na Chadema kuwa mbunge wa viti maalum kwa miaka mitano.
Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema juzi kuwa mwili wa marehemu Leticia unatarajiwa kusafirishwa kutoka nchini Marekani kwa ajili ya maziko.
MTANZANIA
Hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, jana ameonekana hadharani katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Jecha ambaye inaaminika alikuwa mafichoni tangu alipotangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, alionekana ameketi kwenye jukwaa kuu la viongozi, jirani na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Kuonekana kwa Jecha hadharani kumezua mijadala mitaani na hata katika mitandao ya kijamii, huku wengi wakihoji alikuwa wapi mara baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi.
Watu mbalimbali wamekuwa wakihoji kuonekana kwa Jecha hadharani jana, siku ambayo Dk. Shein alitumia maadhimisho ya Mapinduzi kutangaza kwamba uchaguzi wa marudio Zanzibar iwe isiwe utafanyika.
Oktoba 28, mwaka jana majira ya saa sita mchana kwenye Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar zilizopo Kilimani mjini Unguja, ilikuwa ndiyo siku ya mwisho kuonekana Jecha hadharani.
Siku hiyo huku akiwa chini ya ulinzi wa vijana wawili wanaoaminika kuwa ni makomandoo wa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania (JWTZ) waliovaa kiraia, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar mbele ya vyombo vichache vya habari.
Alitumia dakika mbili tu kuvitangazia vyombo hivyo vya habari juu ya adhima yake ya kuufuta uchaguzi na kutoa sababu zilizomfanya kufanya hivyo ikiwamo kuharibiwa kwa uchaguzi kisiwani Pemba.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa taarifa yake kwa vyombo hivyo, Jecha hakutaka kuulizwa maswali.
Oktoba 27, mwaka jana ikiwa ni siku moja kabla ya kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, Jecha pia hakuonekana kwenye kituo cha kutangaza matokeo kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani kwa kile kilichodaiwa alipata matatizo ya kiafya na hivyo kumwachia kazi hiyo Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa.
Siku hiyo majira ya saa kumi jioni, askari wa JWTZ walizingira kituo cha Bwawani na kuwaamuru watu waliokuwa ndani kutotoka nje na hata wale walioko nje ya kituo hicho kutosogea.
Watu waliokuwa ndani ya kituo hicho wengi wao walikuwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa waliofika kusikiliza matokeo ya uchaguzi.
MTANZANIA
NI roho mkononi. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa sasa juu ya hali ya usalama ilivyo katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo kadhaa nchini pindi mtu anapokuwa amebeba kiwango kikubwa cha fedha.
Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha katika jiji hilo yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki aina ya Boxer.
Hali hiyo inawafanya watumiaji wa huduma za benki zilizo ndani ya jengo la Mlimani City maisha yao kuwa hatarini, hasa wale wateja wanaotoa fedha nyingi kutokana na kukumbwa na matukio ya kuuawa na kuporwa fedha.
Jengo hilo lenye matawi ya benki sita, limekuwa likikumbwa na matukio ya mauaji kwa wateja wanaotoa fedha nyingi na majambazi.
Matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea kwa wateja hao, majambazi wamekuwa wakitumia pikipiki aina ya Boxer ambayo ina uwezo mkubwa wa kukimbia.
Miongoni mwa matukio ya kusikitisha yakihusisha moja ya benki zilizopo Mlimani City ni lile lililotokea juzi ambapo mtu mmoja aliuawa na taarifa zake kuzagaa kwenye mitandao ya jamii.
Inaelezwa kuwa mtu huyo aliuawa na majambazi wakati akitoka kwenye moja ya benki ndani ya jingo hilo kuchukua kiasi cha Sh milioni 10 na kuanza safari ya kuelekea eneo la Tegeta Salasala ambako alikuwa akifanya shughuli za ujenzi wa nyumba yake.
Taarifa iliyosambaa mitandaoni inasema kwamba tukio hilo lilitokea jirani na mtoa taarifa hiyo aliyeamua kuwatahadharisha wananchi wengine kutochukua fedha nyingi katika benki zilizo eneo hilo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema kwamba mtu huyo alipotoa fedha hizo, majambazi walianza kumfuata kwa nyuma, wakampita na kumzuia kwa mbele.
“Majambazi walipomzuia kwa mbele walimtaka atoe milioni 10 aliyochukua benki, baada ya kutoa hiyo fedha ndipo walimpiga risasi,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kwamba katika matukio hayo yanayotokea mfululizo, hivi karibuni maeneo ya Bamaga jirani na Hongera Bar, mtu mmoja na mkewe walivamiwa na majambazi walipokuwa wanatoka kuchukua fedha kiasi cha Sh milioni 13 katika benki mojawapo iliyopo Mlimani City.
Baada ya watu hao kuchukua fedha, majambazi yaliwafuata kuanzia hapo Mlimani City hadi Bamaga na kuwataka wawape fedha.
Inaelezwa kwamba jambo lililosaidia, mtu huyo alikuwa amezitenganisha fedha hizo na kuwapa laki 5, lakini walipatwa na hasira na kumhoji kuhusu fedha nyingine alikokuwa amezipeleka hali iliyofanya wampige risasi begani.
Hali hiyo ilimfanya mke wake awaongeze laki moja, na wakafanikiwa kubaki na kiasi kingine cha fedha walizokuwa wamezificha kwenye mlango wa nyuma.
Taarifa nyingine inaelezea kwamba mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Joshua alivamiwa na majambazi baada ya kuchukua fedha kiasi cha milioni 4 kwenye benki mojawapo ya Mlimani City.
Inaelezwa kwamba baada ya mama huyo kufika eneo la Kwa Kakobe, majambazi walimpita na kumsimamisha baada ya kujifanya kuwa wanamjua na aliposimama walimlazimisha kutoa kiasi hicho cha fedha alichokitoa benki na akawapa kunusuru maisha yake.
Kwa sasa benki zilizopo Mlimani City zinaonekana kuwa eneo hatari la kutolea fedha nyingi kutokana na taarifa kwamba upo uwezekano wa kuwapo kwa wafanyakazi wa baadhi ya benki hizo kushirikiana na majambazi.
Tukio jingine lilitokea mwaka jana na kushuhudiwa na gazeti hili, ambapo mtu mmoja alipigwa risasi mbili majira ya saa 6 mchana na kuporwa fedha akiwa katika gari maeneo ya Sinza Kijiweni karibu na Baa ya Deluxe.
Dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo lililoshambuliwa namba T 236 DDT aliyefahamika kwa jina moja la Abasi, alisema fedha ambazo majambazi hao walichukua zilitolewa benki moja ya eneo la Mlimani City.
“Baada ya kuingia na kuegesha gari hapa jirani na hopitali hii ya watoto, alikuja mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi akiwa ameshuka kwenye pikipiki aina ya Boxer na alipofika alisogelea gari letu na kufunua koti lake alilokuwa amebeba bunduki ya SMG,” alisema.
Alisema mtu huyo alimwelekezea silaha mtu aliyekuwa nyuma ya gari na kumwamuru kutoa fedha, lakini akaambiwa hakukuwa na fedha ndani ya gari.
“Baada ya kuona anabisha alimpiga risasi ya kwanza, akageuza SMG kwangu nikakimbia, akafyatua lakini hakunipata ndipo nikasikia risasi nyingine ikipigwa.
“Baada ya muda kulikuwa kimya na niliporudi tena nikakuta majambazi wakiwa wameshaondoka na mkoba wa fedha ‘briefcase’ na kutokomea nao hali iliyofanya wananchi kusogea na kumsaaidia mzee ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi,” alisema Abasi.
MTANZANIA ilipomuuliza dereva huyo kiasi cha fedha kilichoibiwa alisema majambazi hao waliondoka na kiasi kidogo cha fedha na si zote Sh milioni 10.
Tukio jingine lililotokea mwaka jana lilihusisha majambazi kumpora mama mmoja kiasi cha shilingi milioni 10 na kutokomea kusikojulikana.
“Alipotoka benki, majambazi hayo yalimfuata na kuligonga gari lake na ndipo dada huyo aliposimama ili aangalie nani kagonga gari yake ambapo jambazi mmoja alishuka na kumpiga risasi ya kifuani na kutokomea na kiasi hicho cha pesa,” alisema shuhuda wa tukio hilo.
Tukio jingine lilitokea eneo hilo Agosti 22, mwaka juzi likimuhusu Edson Cheyo mmiliki wa Kampuni ya Sowers African iliyopo jirani na Mlimani City aliyeporwa Sh milioni 18.
Cheyo alipigwa risasi ya kifuani na begani na majambazi waliomvamia wakiwa wamepanda pikipiki na walichukua fedha zote na mwenyewe kufariki dunia akiwa anapelekwa hospitali ya Mwananyamala.
Tukio jingine la mauaji ni lile la Sista Brigita Mbanga, mkazi wa Makoka pamoja na dereva Mack Patrick ambao waliuawa eneo la Ubungo Kibangu wakati wakitoka kuchukua fedha Mlimani City.
Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.
Hata hivyo, imekuwa ikidaiwa kuwa baadhi ya benki nchini zimekuwa zikidaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na kufa wakitoka kuchukua pesa.
“Haiwezekani hata mtu anapovamiwa na majambazi kabla ya kuuawa au kujeruhiwa huambiwa tupe miliooni 10 ambazo ndiyo zilizochukuliwa benki. Je, jambazi amejuaje kama wewe una kiasi hicho cha fedha?” alisema mmoja wananchi anayefanya shughuli zake Mlimani City.
Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Salum Mashati, alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha akitoka benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20, wanajuaje kuwa una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki uhalifu huu.”
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki lililopo Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe, alikanusha madai hayo na kusema hawana ushirikiano na majambazi hao wanaofanya uhalifu katika maeneo hayo.
“Si kweli kwamba benki zinashirikiana na majambazi kufanya uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers) hawaruhusiwi kuingia na simu wanapohudumia wateja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alipotakiwa kuelezea namna polisi ilivyojizatiti kudhibiti matukio hayo yanayotokea katika benki hizo, alisema hakuna tukio hata moja ambalo limewahi kutolewa taarifa polisi.
“Hivi kweli inawezekanaje tangu kumeanza kutolewa taarifa hizo hakuna taarifa iliyowahi kutolewa polisi na mengi ya matukio ambayo yemekuwa yakiripotiwa yakifanyiwa ufuatiliaji yanakutwa ni uzushi, kwani hakuna tukio linalotokea hapa Dar es Salaam na wahusika walimalize kwa kukaa kimya,” alisema Kamanda Wambura.
Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka, huenda wananchi wakapatwa na hofu ya kuweka fedha zao benki kwa kuogopa kuporwa na kupigwa risasi wakienda kuzichukua.
Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro, alikiri kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wa benki wenye mtandao na majambazi, huku akisema jeshi lake limeweka mikakati kuhakikisha mtandao huo unasambaratishwa mara moja.
“Ni kweli kwamba baadhi ya mabenki, si yote, yameajiri baadhi ya wafanyakazi, si wote wenye mtandao na majambazi. Kwahiyo hata wao ni majambazi tu.
“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kukamata pikipiki zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka makachero nje na ndani ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikipiki na magari. Nina uhakika tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.
MTANZANIA
Wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba mkoani Dodoma wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuwafuta kazi watendaji wa Serikali ambao wameuza nyumba za Serikali kinyume cha sheria.
Wafanyabiashara hao walisema wamekuwa wakifanya biashara katika soko hilo kwa muda mrefu, lakini hivi sasa wanashangaa kuelezwa kuwa wanatakiwa kuhama kwani jengo hilo limeuzwa kwa mtu binafsi.
Walidai jengo hilo lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Afya kwa muda mrefu, lakini wanashangazwa na hatua ya Serikali kuliuza kwa mtu binafsi badala ya kutoa nafasi kwa wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara zao.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Huseni Michuzi, alisema kwa muda mrefu wapo katika eneo hilo, lakini wanashangaa Serikali kuwataka kuhama wakidai eneo hilo si halali kwao.
“Hili ni soko, hapa tunafukuzwa tupo zaidi ya watu 15, tunaambiwa hili eneo kauziwa mtu binafsi, sasa tunajiuliza mtu binafsi anaweza kuuziwa mali ya Serikali? Tunamwomba Waziri Lukuvi awafute kazi wote waliohusika na dili hili kwani wametumia madaraka yao vibaya,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo, Athumani Makole, alisema alipokea malalamiko ya wafanyabiashara 15 wakitakiwa kuhama katika eneo hilo ambalo linadaiwa ni mali halali ya Solomoni Munuo.
“Lile eneo lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya maonyesho ya Nanenane, baadae ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilitupa maelekezo kuwa ni eneo la walemavu sasa tunashangaa Munuo kudai ni eneo lake,’’ alisema.
Kwa upande wa aliyeuziwa jengo hilo, Munuo, alisema eneo hilo ni mali yake aliyokabidhiwa kihalali na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kushirikiana na manispaa baada ya kuona jengo hilo halitumiki.
Akifafanuzi kuhusu suala hilo, Ofisa Masoko wa Manispaa ya Dodoma, Steven Maufi, alisema kutokana na vielelezo vilivyo eneo hilo ni mali ya Munuo hivyo ana haki ya kuwaondoa watu waliokuwa mbele ya nyumba yake.
“Hilo ni eneo halali la Munuo ndiyo maana tukaamua kuwaondoa wafanyabiashara walio mbele yake, lakini pia wamekuwa wakisababisha uchafu kutokana na kumwaga chini takataka,’’ alisema.
NIPASHE
Wakati, Rais John Magufuli, akifikisha siku ya 70 ofisini leo tangu kuapishwa kwake Novemba tano mwaka jana, gazeti hili limebaini kuwa mpaka sasa amepanda ndege mara moja tu na kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam mara mbili tu.
Taarifa hizo ambazo zilithibitishwa na mmoja wa wasaidizi wa Rais Magufuli, zinaeleza kwamba, jana ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda ndege tangu aingie madarakani.
Katika safari yake ya jana, Rais Magufuli alitumia ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandaoni (Distance calculator), umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Zanzibar ni kilomita 73.43.
Muda wa kutoka Dar es Salaam kwa ndege kwenda Zanzibar, kikokotozi hicho kinaonyesha ni dakika 14 mpaka dakika 20 kutegemea na ukubwa wa ndege na mwende kasi inayotumia.
Jana Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliokuwapo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuuungana na Rais Ali Mohamed Shein katika kusherehekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi.
Wengine waliokuwapo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa, safari iliyomtoa Rais Magufuli kutoka Magogoni, Ikulu jijini Dar es Salaam hadi Zanzibar ni ya pili tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 baada ya kushinda kwa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mbali na safari hiyo, safari nyingine ni ile aliyotumia usafiri wa barabara kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kufungua Bunge la 11 na kupendekeza jina la Waziri Mkuu.
Katika safari hiyo ya Dodoma ambako ndipo makao makuu ya nchi na kuliko na Ikulu ya pili kwa ukubwa ya Chamwino ukitoa ile ya Magogoni, Rais Magufuli baada ya kuzindua Bunge Novemba 20, 2015 alikaa kwa siku kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha umbali, kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ni kilomita 583.64 ambazo kwa gari linalotembea wastani wa mwendo kasi wa kilomita 112 kwa saa, litatumia saa tano na dakika 12 kumaliza safari hiyo.
Wakati leo akifikisha siku ya 70 ofisini, Rais Magufuli hajawahi kusafiri nje ya nchi na mara kadhaa amekuwa akitimiza ahadi yake ya kuhakikisha kuwa mabalozi wa Tanzania katika nje ya nchi wanaliwakilisha taifa kwenye baadhi ya mikutano ili kuondokana na gharama zinazoepukika.
“Lazima tukubaliane kuwa katika kubana matumizi kuna faida na hasara zake, ndiyo maana hata kutosafiri kwake kutakuwa na faida nyingi lakini kunaweza kuwa na hasara kidogo. Ila lazima tu tukubaliane ukitaka kwenda mbiguni lazima kwanza ufe, vivyo hivyo ukitaka kubana matumizi kutakuwa na hasara zake,” alisema mmoja wa wasaidizi wa kiongozi huyo.
Wakati akizindua Bunge, Rais Magufuli alisema safari za nje zimeligharimu taifa Sh. bilioni 356.3, ambazo kati yake Sh. bilioni 183.1 zilikuwa kwa ajili ya tiketi za ndege, Sh. bilioni 68.6 ziligharamikia mafunzo na Sh. bilioni 104.5 zilikuwa za posho.
Rais Magufuli ambaye amebana safari za nje za watumishi wa umma, aliliambia Bunge kwamba, fedha hizo zingeweza kujenga kilometa 400 za barabara ya lami.
Licha ya safari hizo za kikazi, Rais Magufuli pia alisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Msoga, mkoani Pwani kwenye msiba wa dada wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Mpaka sasa, licha ya watumishi wengi wa serikali kuomba kusafiri nje ya nchi na kunyimwa kibali, serikali imewasimamisha kazi watumishi wanne wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kwa kwenda nje ya nchi bila kibali maalumu cha Ikulu.
Itakumbukwa pia kuwa, mpango wa Rais Magufuli wa kubana matumizi, ulifanya utaratibu wa kusherehe siku ya Uhuru ibadilishwe na watu kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi badala ya kwenda uwanja wa taifa kuangalia gwaride na halaiki ambayo huwa inagharimu mabilioni.
Kutokana na kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Sh. bilioni nne zilizookolewa na kuelekezwa kwenye utanuzi wa barabara ya Bagamoyo eneo la Mwenge mpaka Morocco ambako kazi hiyo inaendelea kwa sasa.
Mpango huo wa kubana matumizi ya serikali, pia ulifanya sherehe ya kufungua Bunge ifutwe na fedha zake kuelekezwa kununua vitanda vya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hatua ya Rais Magufuli kutosafiri mara kwa mara huku pia serikali yake ikidhibiti safari za nje kwa viongozi na watumishi wote wa serikali imekuwa ikiwavutia watu wengi nchini na kwingineko nje ya Tanzania, akiwamo mgombea urais wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye.
Katika moja ya mikutano yake ya kampeni akiwa kwenye wilaya ya Agago, nchini humo, Besigye alisema akiingia Ikulu atafuata nyayo za Rais Magufuli kwa kupiga marufuku safari holela za nje ya nchi na kuongeza kuwa ataiuza ndege anayoitumia mpinzani wake, Rais Yoweri Museveni, aina ya Gulfstream V Jet.
Licha ya rekodi ya Rais Magufuli ya kutosafiri kwenda Ulaya na nchi nyingine za nje ya Tanzania hata mara moja tangu aingie madarakani kuwavutia wengi, baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe wamedai kuwa hali hiyo ni balaa kubwa la kiuchumi kwa wasaidizi wa Rais ambao wengi wangetamani asafiri zaidi kama ilivyo kwa wakuu wengine wengi wa nchi za Kiafrika waingiapo madarakani.
Kutokana na rekodi ya safari za Magufuli, ni wazi kuwa hadi sasa, wasaidizi wa Rais huyo wa awamu ya tano watakuwa wamehusika katika safari za kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma na Unguja visiwani Zanzibar alikokuwa jana.
“Rais yeyote anaposafiri ni lazima aambatane na timu ya watu kadhaa wa karibu yake. Kama Rais anasafiri mara kwa mara, ni wazi kwamba hawa pia hunufaika kwa safari hizi ambazo huambatana na posho nzuri za safari. Hata hivyo, kwa hawa (wasaidizi) wa Rais Magufuli hali iko tofauti… Rais amesafiri mara chache na hivyo wao pia watakuwa wameguswa na ratiba hiyo kwa kusafiri mara chache,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana kuhusiana na safari za Rais.
NIPASHE
Baadhi ya vyuo vikuu nchini viko hatarini kufutwa baada ya serikali kuamua kuvipitia ili kujiridhisha kama vina sifa stahiki.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliliambia gazeti hili kwamba uamuzi huo unakuja baada ya kubaini kwamba licha ya vyuo vingi kuwa na ithibati, bado baadhi havina sifa ya kuwa vyuo vikuu.
Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), takriban vyuo vikuu 60 ithibati na vinahesabika kuwa ni vyuo vikuu kamili.
“Hatutaki vyuo ambavyo vipo vipo tu. Tutavikagua upya kuangalia kama vinakidhi vigezo na hata uhalali wa ithibati vilivyopewa,” alisema Prof. Ndalichako.
Aliongeza kuwa vyuo vitakavyothibitika kuwa havifai vitafungwa bila kusita kwa kuwa serikali haitaki Watanzania wafanyiwe majaribio katika elimu. Alisema ni bora ijulikane wazi kuwa hakuna chuo kikuu kuliko kumpeleka mwanafunzi mahali halafu akatoka mtupu.
“Kuwa na vyuo vingi ambavyo havina sifa, kunachangia kuwa na vijana wengi mtaani ambao hawana ajira, jambo ambalo linawaongezea hasira,” alisema Ndalichako.
Prof. Ndalichako alisema serikali itaangalia pia taratibu zinazotumiwa kutoa ithibati kwa sababu kumekuwa na kilio kikubwa kwa umma, wengi wakilalamika kuwa wanafunzi wanamaliza vyuo vikuu wakiwa hawana na uwezo hafifu.
“Kila mtu analalamika, lakini tumechukua hatua gani? Je, tumekaa chini na kuangalia vigezo na kuona ili mtu awe na chuo anatakiwa kuwa na sifa gani? Anatakiwa awe na watu wa aina gani?.
“haiwezekani mtu mwenye shahada moja amfundishe mwanafunzi wa shahada ya kwanza. Wa kumfundisha huyu anatakiwa angalau awe na shahada ya uzamili, ingawa nayo haitoshi… inatakiwa angalau asilimia 50 ya walimu wa kila chuo kikuu wawe na Ph.D (shahada ya uzamivu),” alisema.
Profesa Ndalichako pia alisema kuna vyuo ambavyo mtu akienda kufundisha hata kwa saa moja tu, anaingizwa kwenye orodha ya walimu waajiriwa.
“Tunaposema walimu, tunamaanisha wale ambao wameajiriwa na chuo. Tunaposema tunaangalia ubora wa elimu, itabidi tuangalie utoaji wa ithibati na kujiridhisha kwamba mambo ambayo tunasema yanatakiwa yawepo ili chuo kiitwe chuo kweli yawepo.
‘Kuna wengine wanafanya chuo kama sehemu ya maonyesho. Siku ile unaenda kukagua unakuta maabara na vitu vingine, kumbe vyote vimeazimwa,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia ubora wa elimu ya juu lazima ziwe na mfumo wa kukagua na kufuatilia mara kwa mara na si kuangalia tu wanafunzi wakiwa vyuoni, bali hata baada ya kumaliza na kwenda kwenye soko la ajira ili kusikia waajiri wanawazungumziaje.
Alisema ili kufikia lengo la Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati, kama ambavyo serikali ya awamu ya tano inatamani, lazima viwango vya elimu viangaliwe upya.
Nipashe ilipotaka kujua sababu za Profesa Ndalichako kutorudi Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (Necta) baada ya kumaliza likizo ya mwaka mmoja bila malipo, alisema ni kwa sababu aliamua kujiendeleza kielimu.
“Necta nilikaa miaka tisa, niliona mambo mengi niliyotamani kufanya nimefanya, hivyo nikaona pia kitaaluma watu niliowaacha chuo kikuu (Dar es Salaam) wakiwa walimu wenzangu ni maprofesa. Nikaoana na mimi nijiendeleze kitaaluma,” alisema.
Ili kupata daraja la uprofesa, wanataaluma ambaye amefikia hatua ya mhadhiri mwandamizi, anapaswa kufanya utafiti wa kitaaluma na ushauri elekezi. Utafiti wake huo unatakiwa kuchapishwa kwenye majarida ya kitaaluma kitaifa na kimataifa.
Kutokana na kiu yake hiyo serikali ilimkubalia na baada ya likizo, alirudi chuo kikuu baada ya kuomba na wakamkubalia.
“Nisingerudi hata huu uprofesa nisingeupata. Kwa hiyo kila jambo lina sababu yake na hata nisingeteuliwa (kuwa Waziri) ningejiendeleza kwa sababu sasa hivi mimi ni Associate Profesa (Profesa Mshiriki), lakini nisingeteuliwa kulikuwa na miradi mingine ya utafiti ambayo nimeanza kuitafuta.
“Nilishapata ruzuku kutoka taasisi moja ya Canada na kupata ruzuku ya dola za Marekani 248, 000 (Sh. milioni 530) kwa ajili ya utafiti niliokuwa nifanye Tanzania na Uganda kuangalia walimu wanavyofanya upimaji wwa wanafunzi na humo ndani ningepata machapisho pia,” alisema.
Aliongeza kuwa mwezi wa 12 kuna ruzuku nyingine ambayo ni ya Uingereza, kwenye taasisi iitwayo ESRC aliomba ili afanye utafiti kwenye eneo hilo hilo la upimaji ambalo ndilo eneo lake la kitaaluma.
“Utafiti huu nilikuwa nifanye kwenye shule zilizo kwenye watu wengi ambazo kwa kawaida mahitaji ni meingi kuliko uhalisia. Kwa mfano, uwiano wa mwalimu na wanafunzi haulingani na vitu vingine na nilishapata pauni 697,000 (Sh. bilioni 2.17), kati yake pauni 193,000 (Sh. milioni 599.85) ingekuja kwangu na nyingine kwenye vyuo vya nje ambavyo tungeshirikiana,” alisema.
Alisema licha ya kuwa eneo hilo halipo kwenye wizara yake moja kwa moja, ameanza mazungumzo na mwenzake wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambapo pamoja na mambo mengine, wataangalia madeni ya walimu na namna ya kuyalipa.
MWANANCHI
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete akiambatana na mkewe Salma, jana walimtembelea Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili.
Kikwete ambaye alifika hospitalini hapo saa 11 jioni, alianza kuwasalimia baadhi ya wagonjwa waliolazwa na baadaye kuingia wodi aliyolazwa Sumaye.
Baada ya kuingia katika chumba hicho, Kikwete alikaa kwenye kochi pamoja na Sumaye kisha kumpa pole na kumtania Sumaye aliyekuwa na mkewe Esther kuwa amenenepa japokuwa anaumwa.
Sumaye alisema ana siku ya tano hospitalini hapo na kuelezea furaha yake kwa ujio huo wa Kikwete. “Japokuwa nilikuwa katika hali mbaya ila sasa hivi naendelea vizuri. Pia, nakupongeza mheshimiwa (Kikwete) kwa kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Sumaye.
Mbali na Kikwete, Waziri Mkuu, Kassim majaliwa na mkewe nao walimtembelea kiongozi huyo jana. Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kila siku hali ya Sumaye inaimarika. Juzi, Rais Magufuli alimtembelea Sumaye na kumpa pole huku akimuombea apone haraka
MWANANCHI
Wakati Serikali na wadau mbalimbali wa watetezi wa haki za wanawake na watoto wakihimiza elimu kwa mtoto wa kike, mama mmoja mkoani hapa anatuhumiwa kutaka kumuozesha mtoto wake mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) baada ya kupokea mahari ya Sh600,000 na ng’ombe wanne.
Tukio hilo lilitokea leo katika Mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma. Mama huyo anadaiwa kutaka kumfungisha ndoa binti huyo kwa kijana mmoja anayeishi mtaani hapo.
Hata hivyo, mpango huo wa ndoa ulitibuliwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Nashoni Chinywa ambaye baada ya kupata taarifa aliamua kuwaita polisi wauzuie.
Akizungumzia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Mdala Mazengo alisema aliamua kumuozesha binti yake baada ya kumtaarifu kuwa amepata mchumba. Naye mtoto huyo alidai kukutana na kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 mtaani hapo na kumuahidi kufunga naye ndoa.
Hata hivyo, baadhi ya majirani walidai kuwa mama huyo ambaye ni mjane, ana tabia ya kuwaozesha watoto wake wa kike wakiwa na umri mdogo.
Chinywa alisema baada ya mahojiano, mama huyo alikiri kufanya kosa hilo baada ya kuchoshwa na tabia za watoto hao kwani hata dada yake alibebeshwa mimba akiwa nyumbani.
Hata hivyo, alisema kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa baada ya Kamati ya Serikali ya Mtaa kukutana na Kamati ya Maendeleo ya Jamii kujua ni hatua gani zichukuliwe dhidi ya mama huyo.
“Alikataa shule, sasa yeye mwenyewe aliniambia amepata mchumba na mimi niliamua kumuozesha kwa kuwa wao wenyewe wamependana,” alisema Mdala Mazengo na kuongeza: “Walishatoa barua ya posa na kesho ndiyo tulikuwa tunapanga mahari ya kulipa, wao walikuwa wanataka kunipa mahari kidogo, sasa wakati tunabishana ndipo mwenyekiti na maaskari wakafika hapa nyumbani na kutukamata.” Walidai kuna mtoto mwingine alimuozesha akiwa na miaka 14.
HABARILEO
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bilele ya Mjini Bukoba, mkoani Kagera, Siasa Phocus amevuliwa madaraka kwa madai ya kuendelea na msimamo wa kutaka wazazi wenye watoto shuleni hapo, waendelee kutoa michango kinyume na agizo la serikali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila aliliambia gazeti hili jana mjini hapa kwamba mwalimu huyo alishapewa utaratibu wa kuzingatia sera ya utoaji elimu msingi bure, lakini alikaidi.
“Kwa mamlaka niliyonayo, nachukua hatua hii kwa kumvua mamlaka mkuu wa shule Bilele kutokana na kushindwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali…,” alisema Mnambila.
Alisema mwalimu huyo aliendelea na msimamo wa kuwaambia baadhi ya wazazi waliofika kuuliza utaratibu wa michango, kwamba hana taarifa na miongozo ya serikali, akiwasisitiza kila mzazi kutimiza mahitaji yaliyopo kwenye fomu ya mwanafunzi.
“Mwalimu huyo aliendelea kutoa fomu kwa kila mwanafunzi iliyoainisha kila mahitaji kama ilivyokuwa hapo awali (miaka ya nyuma) huku akitaka michango ya madawati, karatasi za kuchapia mitihani na mlolongo wa gharama nyingine nyingi,”alisema Katibu Tawala.
Michango mingine ambayo wanafunzi wa sekondari wamekuwa wakitozwa kila mwaka ni ya fyekeo, ndoo, jembe, uji, chakula cha mchana na uzio.
Katibu tawala alionya walimu wakuu na wakuu wa shule, kuzingatia na kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bure, kama ilivyo kwenye taratibu za miongozo iliyotolewa kwao katika idara ya elimu.
Fedha zafika mikoani
Wakati huo huo, mikoa mbalimbali imethibitisha kupokea fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure. Jumla ya Sh bilioni 18.77 zimetolewa na serikali kwa ajili ya shule zote za umma nchini.
Miongoni mwa mikoa iliyothibitisha kwa waandishi wa habari kupokea fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza elimu msingi bila malipo ni pamoja na Kagera, Morogo, Rukwa na Mwanza.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Aloyce Kamamba alisema wamepatiwa jumla ya Sh 810,157,000 ambazo zimeshaelekezwa kwenye akaunti za shule zilizoko mkoani humo, ambapo za msingi ni 888 na sekondari 190. Kati ya hizo, 17 ni sekondari za bweni. Kiasi hicho kimetolewa na serikali kwa ajili ya kugharimia huduma mbalimbali ikiwemo chakula.
Mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa, Magalula Said Magalula alisema wamepokea Sh milioni 336 ambapo Sh 143,859,000 zimepelekwa kwenye shule za msingi 360 na kiasi kilichobaki, kimepelekwa shule 105 za sekondari. Kwa mujibu wa Magalula, fedha hizo ni kwa ajili ya mwezi huu kwani kila mwezi serikali itakuwa ikitoa fedha kwa ajili ya mpango huo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri shule yake kupokea Sh milioni 1.4 kwa ajili ya Januari mwaka huu. Katika Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo anayeshughulikia elimu, Wariambora Nkya, alithibitisha kupokea Sh milioni 724.7 kwa ajili ya shule 846 za msingi na 179 za sekondari za bweni na kutwa.
Mkoa mwingine uliothibitisha kupokea fedha hizo ni Mwanza wenye shule za sekondari 197, ambazo zimepewa Sh 642,648,000 kwa ajili ya fidia ya ada za kutwa na bweni na chakula kwa shule za bweni. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema upande wa Shule za Msingi, zipo 850 ambazo zimepokea Sh milioni 356,728,000.
Alisema hadi Desemba 30 mwaka jana, shule zote zilishawekewa fedha kwenye akaunti zake.
Walimu wakuu, wakuu wa shule, bodi wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo na wakati huo huo kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha elimu msingi inatolewa bure.
Licha ya wakuu wa mikoa na idara ya elimu kuhadharisha juu ya hilo, pia Wizara ya Fedha na Mipango hivi karibuni, ilionya wakuu wa shule za msingi na Sekondari watakaotumia ovyo fedha hizo zilizotolewa na serikali kutoa elimu bure, ikisema atakayebainika kuzitumia isivyo, atashughulikiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango iliwataka walimu katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, waweke wazi fedha walizopokea kutoka serikalini wananchi wafahamu alichopewa na matumizi yake.
Bodi za shule zimepewa kazi ya kuhakikisha zinasimamia matumizi na kutoa taarifa. Pia wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wamepewa wajibu wa kusimamia fedha hizo Sh bilioni 14.7, ambazo kati yake, Sh bilioni tatu zimepelekwa katika vyombo vya usimamizi wa mitihani.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.