MTANZANIA
Kamati ya Migogoro na Usuluhishi ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA), imepanga kuanza kusikiliza maelezo ya Serikali ya Burundi na chama tawala dhidi ya hoja za wanaharakati wa haki za binadamu na vyama vya kiraia kutaka ifutiwe uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Vikao hivyo vinatarajiwa kuanza Januari 25 hadi Februari 4, mwaka huu kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu baada ya wanaharakati hao kuwasilisha maombi mbele ya kamati hiyo ya Bunge.
Katika hoja yao, wanaharakati hao wanaliomba Bunge hilo likutane, kujadili na kutoa azimio la mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo, baada ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kutangaza kujiongezea muhula wa utawala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Migogoro na Usuluhishi, Dk. Abdullah Mwinyi, alisema tayari wameshafanya mawasiliano na Serikali ya Burundi kwa ajili ya kikao hicho.
Alisema siku ya kwanza walalamikaji ambao ni vyama vya kiraia walipata fursa ya kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalisikilizwa.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya pili ilifuatia zamu ya wadau ambao ni watu kutoka taasisi na asasi zisizo za kiserikali, walisikilizwa na kuhojiwa.
“Tulipokea barua yao na tukawashukuru kwa kukubali kufika. Lakini tumewaomba wafike Januari 25, mwaka huu kwa ajili ya kuwasikiliza, watasema watakayoyasema na tutawauliza maswali baada ya hapo tutakaa kamati yetu kupitia yote yaliyozungumzwa,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Baada ya hapo tutatayarisha ripoti tutakayoiwasilisha ndani ya Bunge ambako nako itajadiliwa na wabunge kisha kupitisha maazimio yatakayowasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao nao watawasilisha mbele ya wakuu wa nchi wanachama,” alisema.
Alisema dhamira ya kamati yake ni kuhakikisha wanamaliza kusikiliza pande zote wakati wa vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza Januari 25, mwaka huu mjini Arusha.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewatia mbaroni wahamiaji haramu 83, raia wa Ethiopia, waliokuwa wakisafirishwa na gari aina ya Scania lenye namba za usajili T478 DFE mali ya Frola Mwambenja, ambao walikuwa wakitokea Kongowe jijini Dar es Salaam kuelekea Kyela mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema jeshi hilo linamshikilia pia dereva wa gari hilo, Hans Mwakyoma (28) mkazi wa Tukuyu Mbeya na msaidizi wake Alex Adam (32) mkazi wa Mbeya mjini, kwa tuhuma za usafirishaji wa watu hao.
Kamanda Kakamba alisema gari hilo lilikamatwa na askari wa doria wa jeshi hilo saa 3.30 usiku katika Kijiji cha Mahenge, barabara kuu ya Iringa Mbeya likiwasafirisha watu hao kuelekea Kyela ambako ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
“Lilipokamatwa roli hilo, dereva alisema halina mzigo, lakini askari wetu walipolifungua walikuta watu hao wakiwa wamelaliana, baadhi yao wakiwa na hali mbaya na wengine wakiwa wagonjwa,” alisema.
Alisema baada ya kuwakamata, wahamiaji hao walipewa chakula na wale walioonekana wagonjwa wamepatiwa matibabu wakati taratibu zingine za kuwafikisha katika vyombo vya sheria zikiendelea.
“Jambo la kushangaza ni kwamba watu hao walipakiwa katika gari hilo Kongowe jijini Dar es Salaam. Kila mtu anajua Kongowe si Ethiopia kwa hiyo kuna swali la kujiuliza ni namna walivyofika Kongowe hadi wakapata huduma ya kusafirishwa kuelekea wanakoelekea,” alisema.
Alisema biashara haramu ya usafirishaji watu ni jipu kubwa linalohitaji nguvu ya pamoja katika kulitumbua kwani inahusisha mtandao wa watu wengi ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kupambana na biashara hiyo, taarifa za kiintelejensia za jeshi hilo zinaelekea kuunasa mtandao wa biashara hiyo na mkakati huo utakapofanikiwa wahusika wake watatumbuliwa majipu hadharani.
Alisema watu hao wamekuwa wakiitia gharama kubwa serikali, kwani baada ya kuwakamata imekuwa ikilazimika kuwahudumia na kuwasafirisha hadi walipotoka.
MTANZANIA
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (CHADEMA) amesema anatarajia kufufua hoja ya kujadiliwa upya kwa ripoti ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta Escrow zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza jana alisema sababu za kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua iwapo fedha hizo ni za umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi ya 10 likiwemo azimio namba moja la kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) Harbinder Singh Sethi na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi.
Kamati inaelekeza Serikali kutumia sheria za nchi, ikiwamo sheria ya Proceeds of Crime Act, kuhakikisha kuwa Singh Sethi anarejesha fedha zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati yake ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha hizo zilizua mjadala mkubwa bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka msimamo wa Serikali kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma na hivyo kuzidisha mjadala.
MTANZANIA
Utafiti mpya wa ugonjwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU), unatarajiwa kuleta faraja kwa wenzi, ambapo mmoja anaishi na virusi hivyo na mwingine akiwa hana.
Faraja hiyo inahusisha kufanya tendo la ndoa bila kutumia kinga na hivyo kupata watoto bila kusababisha maambukizo yoyote mapya baada ya unywaji wa dawa.
Ugunduzi wa dawa hiyo mseto ya kimiminika ijulikanayo kama PrEP, tayari imetumiwa na wanaume mashoga nchini Uingereza na Marekani.
Dawa hiyo huweza kuondoa hatari ya kuambukizwa hadi asilimia sifuri, itaondoa changamoto iliyokuwapo katika njia namba moja ya kujikinga na virusi, yaani kutumia kondom wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Matumizi ya kondom yalimaanisha kuwa wenzi wa aina hiyo hawawezi kupata watoto bila uwezekano wa kuhatarisha mwenzi ambaye hana VVU.
Kwa sababu hiyo, mamlaka nchini Kenya zimeanzisha mradi wa kuwasaidia wenzi kuwa na familia bila kuhatarisha afya zao.
John na mkewe Josephine, wanaoishi kaskazini mwa Nairobi ni mfano wa wenzi wa aina hiyo, ambapo Josephine anaishi na VVU wakati John hana maambukizo hayo.
Mume huyu anasema kuwa hali kama hiyo inaweza kuwa ngumu na anawajua wenzi ambao wameshatengana kwa sababu hiyo.
Kuna wenzi 260,000 nchini Kenya, ambako mmoja anaishi kwa VVU huku mwenzake akiwa hana.
Wenzi wa aina hiyo wanaojulikana kitaalamu kama serodiscordant, wanachukua asilimia 44 ya mambukizo mapya ya VVU katika taifa hilo. Pamoja na asilimia hiyo wamezaa watoto.
“Lakini nia ya kupata watoto kwa wenzi wa aina hii bado huwa na nguvu mno –utafiti mmoja wa hivi karibuni kwa wenzi wa serodiscordant umeonesha asilimia 17 ya wanawake walipata mimba.
“Kwa sasa majaribio mapya ya dawa yametoa mwanga wa matumaini na faraja kwa wenzi wa aina hii,” anasema John.
Imebainika kwamba njia mpya ya kutumia dawa za kukabiliana na VVU, ambazo kwa kawaida hupewa watu wanaoishi na virusi hivyo, inaweza kutumika kwa wenzi wa aina hiyo kujaribu kuzaa watoto wasio na VVU bila pia kumwambukiza mwezi asiye na virusi hivyo.
Dk. Nelly Mugo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Washington cha nchini Marekani kwa pamoja wanaendesha majaribio hayo.
Majaribio hayo yalihusisha wenzi 4,700, ambao mmoja ana VVU na mwingine hana maambukizo.
Katika majaribio hayo, mtu ambaye hakuambukizwa VVU alikunywa PrEP katika kipindi cha miezi 36.
“Tulibaini kwamba kuwa na dawa katika mfumo wako mwilini kulipunguza kiwango cha maambukizo kwa zaidi ya asilimia 90.
“Lakini pia iwapo mwenzi mwenye VVU pia alichukua dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs), uambukizo wa VVU ulipunguzwa hadi asilimia sifuri au karibu na sifuri,” alisema.
Katika baadhi ya jamii shinikizo la kijamii la kutaka kuwa na watoto linaweza kuwa kubwa huku familia zisizo na watoto mara nyingi zikipata shida kueleza kwanini hazijazaa.
Katika utafiti wa karibuni, wenzi walieleza kwamba walijisikia kutokuwa na la kufanya na wako katika hatari ya kupata VVU iwapo watajaribu kupata mimba.
Lakini katika mradi wa sasa, wenzi wasioambukizwa walipata faraja baada ya kubakia salama bila kuambukizwa walipofanya tendo la ndoa bila kinga, hali iliyosababisha imani kwa dawa hiyo kuwa na uwezo wa kuwalinda.
Dk. Mugo anasema: “Hisia za kawaida zilizozoeleka kwa kuzaa watoto ni pamoja na kutimiza matarajio ya wenzi husika ya ukubwa wa familia waitakayo, kupata watoto wao wenyewe wa kuwazaa na kuendeleza uhusiano imara na mara nyingi muhimu zaidi ikiwa ni kukabiliana na shinikizo la nje kutoka kwa jamii” alisema.
VVU haitibiki, kwa sababu mara inapoingia katika mwili, hujificha katika mahali ambapo ni vigumu kupafikia, na kusababisha hodhi, hali inayomanisha kwamba kamwe haiwezi kuondolewa kutoka humo hodhini.
Nadharia iliyo nyuma ya PrEP ni kwamba kuchukua dawa za ARVs kabla ya kuambukizwa kunamaanisha tayari zipo ndani ya mwili.
Lakini watafiti wameonesha kuwa iwapo mtu asiyeambukizwa tayari atakuwa na dawa za PrEP katika mifumo yao ya mwili wakati virusi vinapoingia katika miili yao hiyo huuawa.
Hili linamaanisha kuwa virusi huwa havina nafasi ya kujificha katika hodhi, na hivyo ni vigumu kwa mtu kuambukizwa.
“PrEP ni kitu kizuri kinachoweza kuwafaa wenzi hawa,” anasema Dk. Mugo, kwa sababu inaweza kutatua kile alichokiita ‘hali tete ya ufarakano.
“Wakati unapobaini mwenzi wako ana VVU husababisha maumivu makubwa ya kihisia,” aliongeza. “Lakini uhusiano na hisia na mapenzi vina nguvu kuliko virusi.
“Wengi wa wenzi hutaka kubakia pamoja, lakini wanashindwa kurejea katika hali ya kawaida ya uhusiano wa tendo la ndoa. PrEP ina uwezo mkubwa wa kutatua tatizo hilo,” anasema.
Jaribio hilo lilikuwa na mafanikio kwani kufikia Septemba 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza kuwa watu walio katika hatari ya kupata VVU wapatiwe PrEP kama chaguo la pili la kujikinga, kama sehemu ya uzuiaji wa maambukizo.
NIPASHE
Rungu la faini kutokana na ukiukwaji wa sheria za mazingira limeendelea kuviandama viwanda mbalimbali vya mkoa wa Morogoro.
Hivi sasa viwanda vya sukari vya Mtibwa na Ilovo kilichoko Kilombero pamoja na kile cha kutengeneza ngozi cha ACE, vimetozwa jumla ya sh. milioni 40 kwa makosa ya aina hiyo katika maeneo yao.
Uamuzi huo ulitolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoani hapa akiambatana na maofisa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
Kiwanda cha Ilovo kimetozwa faini ya sh. m,ilioni 25 baada ya kubainika kuwa na mfumo mbovu wa utunzaji taka ngumu na kushindwa kuhifadhi vyema mabaki ya mabati yanayotolewa kiwandani hapo. Mbali na faini ambayo inatakiwa kulipwa ndani ya siku saba, walitakiwa kurekebisha upungufu huo ndani ya siku 30.
Naibu waziri huyo aliutaka uongozi huo kuhakikisha upungufu 40 uliotajwa kwenye ripoti ya ukaguzi, iliyofanywa na Nemc zaidi ya miezi mitatu iliyopita, unafanyiwa marekebisho sambamba na kuutolea taarifa uwanja wa ndege ulioko ndani ya kiwanda hicho ambao hauna cheti chochote cha ukaguzi.
Kwa upande wa kiwanda cha ngozi cha ACE cha mjini Morogoro, serikali imekitoza faini ya Sh. milioni 15 kutokana na kubainika kuwa na mfumo mbovu wa utiririshaji na uhifadhi wa maji taka.
Mpina pia aliiagiza menejimenti ya kiwanda kudhibiti harufu mbaya inayolalamikiwa na wananchi, hususan walio jirani na kiwanda hicho.
Naibu Waziri Mpina alifanya ziara pia katika soko kuu la mjini Morogoro na kuagiza ujenzi mpya wa soko kuzingatia vizimba vya uhifadhi wa taka ili zisitawanyike na kuutaka uongozi wa manispaa kutofanya mlundikano wa taka katika eneo hilo kama ilivyoonekana.
Ziara hiyo ya Mpina iliyafikia pia maeneo ya kituo kikuu cha mabasi cha Msamvu, kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula cha Abood (Moproco), Kiwanda cha maturubai, Kiwanda cha nguo cha 21st Century, Kiwanda cha Magunia na mabwawa yanayopokea majitaka yatokayo viwandani.
Kutokana na maagizo ya Naibu Waziri, mtaalamu wa mazingira kutoka Ilovo, Mary Kigula, alisema watahakikisha wanatekeleza ikiwa pamoja na kupanda miti na kutoa huduma za kijamii katika maeneo yanayowazunguka.
Naye Mkuu wa Idara ya Uzingatiaji wa Sheria ya mazingira kutoka Nemc, Alfred Msokwa, alisema baraza limekuwa likitoa ushauri na maelekezo kwa uongozi wa viwanda lakini wengi wamekuwa wakipuuza.
Msokwa alisema tangu mwaka 2013 NEMC imefanya ukaguzi katika viwanda takribani vyote mkoani Morogoro na kutoa ushauri ambapo baadhi ya viwanda bado vipo katika utekelezaji wa marekebisho yake huku vingine vikipuuzia maelekezo hayo na kujikuta vikitakiwa kulipa faini kwa mujibu wa sheria.
NIPASHE
Kashfa ya benki ya Stanbic Tanzania iliyotokana na mkopo wa Sh. trilioni 1.3 ambao Serikali ya Tanzania ilikopa benki ya Standard ya Uingereza, imeingia kwenye sura mpya baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuitoza benki hiyo faini ya Sh. bilioni tatu kutokana na kuvunja taratibu za kibenki.
Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka jana, Mahakama ya London, Uingereza ilibaini ufisadi kwenye mchakato wa mkopo huo ambao serikali ya Tanzania ilikopa benki ya Standard ya Uingereza kupitia mshirika wake Stanbic Tanzania.
Katika hukumu yake, mahakama hiyo iliamuru Serikali ya Tanzania ilipwe dola za Marekani milioni saba (Sh. bilioni 15), ikiwani ni asilimia moja ya riba iliyoongezwa na tozo ya Sh. bilioni moja.
Katika mkopo huo, serikali ilitakiwa kulipa asilimia 1.4, lakini benki ya Stanbic Tanzania, ikaingiza kinyamela kampuni ya Kitanzania ya EGMA kama mtu wa kati pamoja na kuongeza asilimia moja ya mkopo huo kisi cha dola za Marekani milioni sita.
Fedha hizo zinadaiwa kuingizwa kwenye akanti ya EGMA na baada ya siku chache kutolewa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, alisema kwa kuzingatia upungufu wa miamala iliyohusisha kampuni ya EGMA na Stanbic Tanzania, BoT imeiandikia barua benki ya Stanbic ya kusudio la kuitoza faini ya Sh. bilioni 3.
Alisema faini hiyo imetozwa kutokana na kifungu namba 67 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Alisema sheria hiyo inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kitaisha Januari 30, mwaka huu.
Alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi huo, Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
Kuhusu kampuni ya EGMA, Dk. Mpango alisema uchunguzi bado unaendelea kufanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na utakapokamilika taarifa itawekwa wazi.
“Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia sheria,” alisema.
Dk. Mpango alisema Julai, 2013 BoT iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo, huku baadhi ya wafanyakazi wake kuacha kazi na wengine kuondolewa kazini wakiwamo viongozi waandamizi wa benki hivyo, hivyo kuagiza kufanyika kwa ukaguzi maalum.
Alisema ukaguzi huo ulibaini kuwapo kwa miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya EGMA iliyohusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo huo.
Alisema malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume cha taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic.
Dk. Mpango alisema taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic na BoT iliagiza Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Alisema pia Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Kupambana na Utakatishaji Fedha ( FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka na Stanbic walitekeleza na kutoa taarifa FIU.
Alisema Septemba 29, mwaka jana, BoT ilipokea barua kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Kughushi na Rushwa ya nchini Uingereza (SFO), ikiiomba BoT ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya benki ya Standard ambayo ni mshirika wa Stanbic Tanzania.
Dk. Mpango alisema katika kesi hiyo benki ya Standard ilikubali makosa na ilitozwa faini ya dola za Marekani milioni 32.20, ambazo kiasi cha dola milioni 7 zinalipwa kwa serikali ya Tanzania, dola milioni 6 zikiwa ni fidia na dola milioni moja zikiwa kama ni riba.
“Faini waliyopewa Stanbic kwa benki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema.
Dk. Mpango alionya kuwa, hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Nipashe lilimtafuta msemaji wa benki ya Stanbic, Annette Nkini, kuelezea hatua ya BoT kuindikia barua ya kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa kuna wakubwa wake ambao wanapaswa kulizungumzia.
NIPASHE
Wakati mazungumzo ya kutafuta muafaka wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana yakiendelea kufanyika , Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wake, Abdallah Bulembo, imejipanga kupiga kambi visiwani Zanzibar kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.
Chama hicho kimeridhia kurudiwa kwa uchaguzi huo, huku chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF ambacho mgombea wake ni Seif Shariff Hamad kikikataa kurudiwa kwa uchaguzi huo na kutaka atangazwe mshindi kwa kuzingatia uchaguzi mkuu uliopita ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa madai ya kufanyika udanganyifu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Abdallah Bulembo, alisema baraza hilo limeridhia jumuiya hiyo kuhamia Zanzibar kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa marudio.
“Tutahamia Zanzibar tutakapotangaziwa ni tarehe ngapi imepangwa uchaguzi huo kufanyika,” alisema Bulembo.
Aidha, alisema kikao hicho cha baraza kuu pia kilimpongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
Kuhusu kujaza nafasi za watu waliohamia vyama vya upinzani, Bulembo alisema baraza limeteua watu kujaza nafasi za walioondoka CCM kwenda vyama vya hivyo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana wakiwa wajumbe wa baraza hilo.
“Mkoa wa Kagera mjumbe wa baraza kuu alihamia Chadema, mkoa wa Pwani alihamia CUF, mkoa wa Njombe alihamia ACT-Wazalendo, kwahiyo nafasi zile tumepitisha majina matatu matatu ili yarudi kwenye mikoa kujaza hizo nafasi,” alisema.
Bulembo pia alisema amemteua, Shehe Hamis Hamdani, kuwa mjumbe wa baraza hilo kutoka Pemba na katika nafasi ya mjumbe wa kamati ya utekelezaji taifa baraza limemchagua Jaffari Mwenyemba ambaye ni Meya wa Manispaa ya Dodoma na Godfrey Mheluka kuwa Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Bara.
Bulembo alisema mwaka huu wiki ya wazazi itafanyika mkoani Morogoro na kwamba sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM zitakazofanyika mkoani Singida, jumuiya hiyo itapiga kambi huko kufanya kazi za chama.
Kuhusu elimu, Bulembo alisema Baraza limeagiza watu wote wanaohusika na ubadhirifu katika shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo wapelekwe mahakamani.
Alisema kuna shule zimefanyiwa ukaguzi na kubainika kuwapo na ubadhirifu wa fedha nyingi na watumishi wote waliohusika watapelekwa mahakamani.
NIPASHE
Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kimejiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio unaotarajiwa kufanyika Machi, mwaka huu visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Ayubu Kimangale, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema wao kama chama cha siasa lengo lao ni kukuza chama kupitia chaguzi kama hizo, hivyo ni lazima washiriki kwa hali na mali.
Kimangale alisema wamejiandaa kusimamisha wagombea katika ngazi za urais, uwakilishi katika kila nafasi.
Aidha, baraza hilo la wadhamini limeteua viongozi wa muda baada ya wale waliokuwapo kusimamishwa kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za kushindwa kuwajibika zinazowakabili.
Kimangale alisema uongozi huo wa muda utafanya kazi kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo chama kitafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wapya.
Alisema viongozi waliosimamishwa ambao hawatakutwa na hatia wataruhusiwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa walioteuliwa kushika nafasi hizo kwa muda ni Jumapili Kaliki, nafasi ya Mwenyekiti, Khamisi Kombo, Makamu Mwenyekiti, Zamila Mrisho, Katibu Mkuu na Mvita Mangupili, Naibu Katibu Mkuu.
NIPASHE
Viongozi wa kampuni ya Victoria Media inayomiliki gazeti la Mawio wameelezea kusikitishwa kwao na uamuzi wa serikali wa kulifuta gazeti hilo huku wakidai kushangazwa na uamuzi huo mzito uliotangazwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ambaye pia ndiye aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Mawio lililokuwa likitoka kila wiki, Simon Mkina, alisema wameshItushwa na uamuzi wa kufutwa kwa gazeti hilo na kwamba, pamoja na hatua hiyo kali dhidi yao, kinachowashangaza ni ukweli kuwa hadi sasa hawajapata taarifa yoyote rasmi ya serikali kuwaarifu jambo hilo ili wajue ni hatua gani wachukue.
“Sisi (Mawio) ndiyo waathirika wakubwa wa taarifa hii. Kinachotushangaza ni kuwa hadi sasa hatujapata barua yoyote ya serikali kuhusiana na jambo hili. Nasi tumemsikia tu Waziri (Nape) akitangaza kutufuta na kwakweli tumeshtushwa sana. Tutakaa na kuamua ni hatua gani tuchukue kutokana na uamuzi huu,” alisema Mkina wakati akizungumza na Nipashe jana.
Kadhalika, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa kampuni hiyo, Yusuf Abood, alisema hadi jana uongozi wa kampuni ya yao (Victoria Media) ulikuwa haujapata barua yoyote ya kufutwa kwa gazeti hilo bali wanasikia kupitia katika mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.
Alisema serikali inapaswa kutoa sababu zilizosababisha kufutwa kwa gazeti hilo kwa maandishi kwani kuna adhabu za kulifuta gazeti na adhabu za kulifungia gazeti.
Alisema kulifuta gazeti la Mawio kutakuwa kumeminya haki ya wananchi ya kupata habari na pia kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa.
Akieleza zaidi, alisema uongozi wa kampuni ya Victoria Media ulikuwa ukipokea barua kila baada ya wiki mbili kutoka serikalini iliyokuwa inawataka kujieleza au kutoa maelezo kuhusu habari fulani na hivyo, hadi kufutwa kwa gazeti hilo, uongozi wao bado haujafahamu ni habari gani iliyosababisha gazeti lao kufutwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema Serikali imelazimika kulifuta gazeti la Mawio kutoka katika orodha ya magazeti yaliyopo nchini kutokana na kukithiri kwake katika kutoa habari zisizozingatia miiko ya uandishi wa habari licha ya kuwahi kuonywa mara kadhaa katika kipindi cha takribani miaka nane.
Alisema amri ya kulifuta gazeti hilo imetolewa katika tangazo la Serikali namba 55 la Januari, mwaka huu, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229, kifungu cha 25(1).
Nape alisema mojawapo ya habari zilizosababisha gazeti hilo kufungiwa ni pamoja na ile iliyokuwa na kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar” pamoja na ile ya “Seif Rais Zanzibar, maandalizi ya kumtangaza yaiva.”
Alisema hatu hiyo inalizuia gazeti hilo kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306.
“Serikali kwa masikitiko makubwa imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo usioridhisha na kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na pia kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi,” alisema Nape.
Alieleza kuwa serikali haikukurupuka kulifuta gazeti hilo, kwani Msajili wa Magazeti amekuwa akifanya juhudi kubwa na za muda mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari 2016, kwa kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala bila ya mafanikio.
Alisema Msajili wa Magazeti aliwahi kufanya mawasiliano na Mhariri wa gazeti hilo mara nane lakini mhariri wa gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa.
HABARILEO
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa kushirikiana na Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Usalama wa Taifa wamekamata madini yenye thamani ya jumla ya Sh milioni 11.2 ambayo yalikuwa yakitoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Aidha serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imesema inatoa motisha kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa kwa Kamishna wa Madini ama Wakala za utoroshaji/magendo na biashara haramu ya madini zitakazowezesha ukamataji wa madini.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TMAA, Yisambi Shiwa alisema raia mmoja wa kigeni na Mtanzania, walikamatwa wakiwa na madini hayo bila kuwa na kibali chochote cha usafirishaji kama ambavyo Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza.
“Raia huyu wa kigeni ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi kwani tayari ameshafunguliwa kesi mahakamani, alikuwa anasafiri kwenda mji wa Bangkok Thailand na alikamatwa akiwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo almasi, aquamarine, sapphire, green tourmaline, quartz na rhodolite,” alisema Shiwa.
Shiwa alisema tukio lingine, Mtanzania ambaye alikuwa anasafiri kwenda Ujerumani alikamatwa akiwa na madini na kufikishwa katika vyombo vya dola. Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari 13 mwaka huu, kumekuwepo na matukio 14 ya utoroshaji madini.
Alisema madini yenye thamani ya Sh bilioni 3.2 yalikamatwa na wakaguzi wa Wakala kupitia Madawati ya Ukaguzi yaliyopo katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam (JNIA), Kilimanjaro (KIA) na Mwanza ambapo yote yalitaifishwa na Serikali.
MWANANCHI
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema operesheni inayoendelea ya kukamata wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume na sheria, haiwalengi raia wa Kenya kama inavyodhaniwa.
Agizo la kuwaondoa raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria lilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipotembelea makao makuu ya Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Waziri Masauni alisema kumekuwapo na ongezeko la wageni nchini wanaoishi kwa vibali vya kufanya kazi za kitaalamu au wawekezaji, lakini wanafanya biashara zisizo na tija na wengine kufanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya na hivyo kuagiza waanze kusakwa na kurejeshwa kwao.
Utekelezaji wa agizo hilo ulichukuliwa kuwa unawalenga raia wa Kenya, ambayo ina vitega uchumi vingi na ambayo raia wake wana muingiliano mkubwa na Watanzania.
Lakini Waziri Kitwanga alisema fikra hizo ni tofauti na nia ya Serikali na kwamba operesheni hiyo itakuwa endelevu. Alisema mpaka kufikia Ijumaa ya wiki iliyopita, raia 409 wa kigeni walikuwa wamekamatwa, na wengi ni kutoka nchi za India na China. “Tunataka raia wa kigeni anayeingia nchini afuate utaratibu,” alisema Waziri huyo.
“Wapo wanaosema kuwa tunawalenga zaidi Wakenya, lakini kati ya raia hao 409 waliokamatwa, Wakenya ni wanane tu.” Alisema raia kutoka Kenya wanaoishi nchini ni zaidi ya 6,000 na wote wana vibali, isipokuwa hao wanane ambao pia walibainika kujihusisha na uhalifu.
“Nchi za Afrika Mashariki zina makubaliano maalum ndiyo maana hakuna usumbufu kwa raia wa nchi za ukanda huo zaidi ya hao Wakenya tu,” alisema.
Mwaka jana kulikuwa na matukio kadhaa yaliyohusishwa na harakati za kigaidi. Vituo viwili vya polisi vya Mkuranga na Sitakishari vilivamiwa na watu waliopora silaha, wakati watu takriban 10 walikamatwa mkoani Morogoro wakiwa na vifaa ambavyo polisi walisema hutumiwa na watu hao.
Pia polisi walihitaji msaada wa askari wa Jeshi la Wananchi kupambana na vijana waliokuwa kwenye mapango ya Amboni Tanga, huku vituo watoto kadhaa wakibainika kufundishwa mafunzo ya kigaidi kwenye nyumba za mkoani Kilimanjaro.
Waziri Kitwanga alisema katika kuhakikisha mipaka na bandari inalindwa ipasavyo, wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wapo katika majadiliano ya kuanza kuweka polisi kulinda bandari, badala ya kampuni binafsi.
“Tunajadili idadi ya askari tutakaowatumia, tutawaweka sehemu gani, pia iwapo wavae sare au wawe kiraia,” alisema.
“Watanzania watambue kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anaishi kwa usalama na utulivu. Kila Mtanzania anaweza kutafuta haki yake lakini akumbuke kuwa upande mwingine kuna wajibu anaotakiwa kuufanya. Haki na wajibu viende sambamba.” Kuvamiwa vituo vya polisi Waziri Kitwanga pia alizungumzia tishio la vitendo vya ugaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, akisema matukio ya kuvamiwa kwa vituo vya polisi, yana harufu ya ugaidi. “Ugaidi haujakomaa Tanzania, na magaidi hawajawa na nguvu. Wanachofanya ni kuvamia kituo cha polisi, kuchukua silaha na kuzitumia kufanya uhalifu kupata fedha ili kuendesha maisha yao. Kuna dalili kubwa kwamba huu ni ugaidi,” alisema.
Alisema licha ya Serikali kuwakamata, wapo wanaoendelea kuingia nchini na ili kumaliza suala hilo ni lazima uwekwe mpango wa muda mrefu.
“Kwa sasa tunaendelea kujadiliana kuhusu mpango wa kutambua raia wetu na wanafunzi katika shule mbalimbali. Lazima tujue wangapi wameacha shule na wamekwenda wapi.
Ugaidi ukikomaa katika nchi unakuwa tatizo kubwa,” alisema. “Magaidi hawatengenezwi nchini, wanatoka hapa wanakwenda Somalia wanafundishwa na kisha wanarudi kufanya ugaidi.
Lazima tutambue raia waliotoka Tanzania walikwenda nchi gani na kwa sababu gani. Bado tunajadiliana tuone tutaliendesha vipi jambo hili.” Kitwanga alisema ili polisi iweze kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima iwe na mfumo imara kuanzia makao makuu hadi ngazi ya chini ya ulinzi shirikishi.
Alisema moja ya changamoto alizokumbana nazo baada ya kuteuliwa kuwa waziri ni dosari katika mfumo wa utendaji kazi.
Alisema nchi ina polisi 45,000 na kati yao wanaoishi kambini ni 10,000 tu na kwamba kuishi uraiani kunashusha nidhamu. “Hii ni changamoto kwa sababu ukitaka kuwakusanya wote hutaweza maana wengi wanaishi uraiani.
Kwa viwango vya kimataifa, askari mmoja anapaswa kulinda watu 350. Kwa Afrika askari mmoja analinda kati ya watu 500 hadi 700 lakini kwa Tanzania analinda watu 1,000 hadi 1,200,” alisema
MWANANCHI
Wakati katibu mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akitangaza kujiondoa chama hicho, aliacha maswali ya kutathmini ujio wa Edward Lowassa kama utakuwa mzigo au mali kwa vyama vya upinzani, na sasa wilaya za Ilala na Kinondoni zimekamilisha majibu.
Ushindi wa kwanza wa vyama vya upinzani katika nafasi ya umeya za manispaa hizo mbili umeonyesha nguvu ya waziri huyo mkuu wa zamani aliyotoka nayo chama tawala.
Ushindi huo ambao unavifanya vyama vya Chadema na CUF kuelekea kutwaa umeya wa Jiji la Dar es Salaam, pamoja na mwingine kwenye majiji ya Mbeya na Arusha umedhihirisha nguvu ya Lowassa, ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vingine vitatu, CUF, NLD na NCCR Mageuzi vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). “Lowassa ameiteka Dar,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kwenye mahojiano na gazeti la Mwananchi kabla ya madiwani wa CUF na Chadema kushinda viti vya umeya wa Ilala na Kinondoni mwishoni mwa wiki.
“Tangu upinzani uingie nchini haujawahi kuishika Dar.” Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, alisema Lowassa ameweza kuvipa vyama hivyo nafasi ya kuongoza halmashauri jambo ambalo linathibitisha kuwa alikuwa ni mali na si mzigo kwao.
Katika uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Kinondoni, diwani wa Ubungo, Boniface Jackob alishinda kwa kupata kura 38, huku Jumanne Mbulu wa CUF akitwaa unaibu meya.
Kwenye Manispaa ya Ilala, Charles Kayeko (Chadema) alishinda umeya na Omari Kumbilamoto wa CUF alitwaa unaibu. Ushindi huo ni wa kwanza kwa vyama vya upinzani jijini Dar es Salaam tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Mbali na ushindi huo, Ukawa imefanikiwa kutwaa viti kadhaa kwenye halmashauri ambazo zilikuwa mikononi mwa CCM hivyo kuongeza wigo wao kwenye uongozi. Mkoani Kilimanjaro, Chadema imeshika halmashauri sita kati ya saba ambazo ni Moshi Mjini, Hai, Rombo, Moshi Vijijini na Siha wakati mkoani Mbeya, Chadema imechukua halmashauri ya jiji hilo, pamoja na ile ya mji wa Tunduma.
Mkoani Arusha na Manyara, Chadema na Ukawa zimechukua Halmashauri ya Jiji la Arusha, Monduli, Karatu, Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi na Babati Mjini, wakati mkoani Kagera Ukawa imechukua Manispaa ya Bukoba na mji mdogo wa Kayanga.
Mkoani Mtwara, CUF na Ukawa zimechukua halmashauri ya Tandahimba, Mtwara Mjini na Newala Mjini huku mkoani Lindi ikichukua Kilwa. Mkoani Mara, Chadema kupitia Ukawa inaongoza halmashauri ya Serengeti, Tarime Vijijini na Tarime Mjini.
Mkoani Morogoro, Ukawa imechukua halmashauri ya Kilombero na Ifakara huku mkoani Iringa ikichukua ile ya Iringa Mjini. Kwa mujibu wa Lissu ongezeko la halmashauri kuwa chini ya wapinzani limechangiwa na waziri huyo mkuu wa zamani aliyejiuzulu mwaka 2008.
Alipoulizwa kuhusu nguvu hiyo ya Lowassa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema mbunge huyo wa zamani wa Monduli ameleta chachu ya kupata madiwani na wabunge wengi ingawa muungano wa Ukawa nao umesaidia. “Ukawa ndiyo kiini cha mafanikio, lakini chachu kubwa ni Lowassa kujiunga na Chadema kwa kuwa alikuwa na wafuasi wengi,” alisema Profesa Mpangala. Alisema hata kusingekuwa na Ukawa wala Lowassa kujiunga na Chadema, Chadema imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka kwa kuongeza idadi ya wawakilishi katika uchaguzi.
MWANANCHI
Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Jude Ruwa’ichi amewataka wenye dhamana nchini, kufanya uamuzi mgumu kwa ustawi wa Tanzania, akionya kuwa iwapo Zanzibar kutawaka, Bara haitakuwa salama.
Askofu Ruwa’ichi ameyasema hayo wakati hali ya kisiasa Zanzibar ikiwa kwenye mgogoro baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais wa visiwa hivyo, wawakilishi na madiwani, uamuzi ambao unapingwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, huku mazungumzo ya amani yakionekana kupoteza mwelekeo.
Akizungumaa wakati wa hafla ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Mkoa wa Mtwara, Titus Mdoe mkoani hapa, Askofu Ruwa’ichi aliwataka wananchi waendelee kuombea amani, lakini wenye dhamana lazima wachukue uamuzi mgumu. “Tuzidi kuomba amani itawale na hali inayoendelea Zanzibar tuangalie isitufikishe hatua ya kutugawa,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
“Zanzibar pakiwaka na Bara hapatakuwa shwari. Tumwombe Mungu atuepushe na mafarakano yote yanayoweza kuharibu amani yetu. “Wenye dhamana wafanye maamuzi magumu kwa ustawi wa jamii.” Kukwama kwa hali ya kisiasa Zanzibar kulifanya wagombea wa urais kutoka vyama vyenye ushindani mkubwa, Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na Dk Ali Mohamed Shein (CCM) kuanza mazungumzo pamoja na marais wa zamani wa visiwa hivyo na Jakaya Kikwete, lakini hadi sasa hakuna muafaka uliopatikana na badala yake kila upande unatoa kauli inayopingwa na mwingine.
Wakati Dk Shein anawataka Wazanzibari kuanza kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi kama yalivyoahidiwa na ZEC, Maalim Seif anataka mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 atangazwe na vyama hivyo vikutane kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia, Maalim Seif, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwenye serikali ya SUK inayomaliza muda wake, ameshamwandikia barua kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kumuomba atumie ushawishi wake kutatua mgogoro huo mapema. hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama aliyekuwa mgeni rasmi. Lakini Mhagama hakugusia suala hilo, badala yake alisema Taifa halina maadili kuanzia ngazi ya viongozi hadi wananchi, kulitaka kanisa kuwajenga wananchi kiimani na kimaadili na kuwa Serikali itasimamia sheria na misingi ya maadili.
Alisema vitendo vya rushwa na mauaji ya albino yanapaswa kukemewa na kila mmoja. “Tumaini la Serikali liko kwako Mdoe.
Viongozi wa dini mtatusaidia kulea Watanzania kwa kufuata misingi ya dini huku sisi viongozi wa Serikali tukiwalea kwa kufuata sheria na taratibu za kisheria,” alisema. “Tabia za kifisadi, ujambazi, kishirikina na rushwa zimeendelea kutawala nchini. Niwahakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kupambana na hayo yote,” alisema Mhagama.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.