Ikiwa ni siku tatu tu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutembelea bandari ya Dar es salaam na kukagua makontena 20 yenye shehena ya mchanga wa madini kutoka migodi mbalimbali iliyopo Kanda ya Ziwa.
Leo March 25 2017 Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imebaini makontena mengine 262 yenye mchanga wa dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya MOFED (zamani ZAMCARGO) iliyopo Kurasini jijini Dar es salaam yakisubiri taratibu za kiforodha kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia kitengo cha makontena kinachoendeshwa na kampuni binfasi ya TICTS.
Rais Magufuli alifika bandarini siku hiyo kukagua utekelezaji wa agizo lake la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye madini kutoka migodini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema makontena hayo yaliyokuwa katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kiforodha yamebainika leo tarehe 25 Machi, 2017 katika msako mkali unaoendeshwa na Mamlaka yake.
Mhandisi Kakoko amesema makontena yote hayo yalikuwa na lakiri (seals) za Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), na yalikuwa yanashughulikiwa na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Freight Forwarders Tanzania Limited iliyopo Dar es salaam.
Mhandisi Kakoko amesema jumla ya makontena 256 yalikuwa katika bandari kavu ya MOFED, wakati makontena mengine sita yalikuwa tayari yameshaingizwa bandarini tayari kwa kusafirishwa.
Ametoa wito kwa makampuni yote ya madini yenye shehena za mchanga yajitokeze yenyewe na kuonesha mizigo yao popote ilipo nchini kabla haijabainika katika msako kabambe unaondeshwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchi nzima.
Ulipitwa na hii? ya Rais Magufuli kusema ‘Unaweza kumchukia mtu lakini usiichukie Tanzania’, Bonyeza play hapa chini kuitazama