Mapema jana September 12, 2017 ziliripotiwa taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa kwa risasi kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba na watu wasiojulikana wakati akiingia getini nyumbani kwake tukio ambalo limeamsha hisia za watu wengi na kupaza sauti zao kukemea huku wakilitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua zaidi.
Kufuatia tukio hilo Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’ limetoa tamko kulaani kitendo hicho ambacho kinafanana na alichofanyiwa Mbunge wake Tundu Lissu ambaye yupo Nairobi Kenya akitibiwa.
Katika taarifa yao CHADEMA imesema:
Tumepokea Taarifa za kuvamiwa kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba na kupigwa risasi, kwa mshituko mkubwa na hasa kutokana na ukweli kuwa tukio hili limetokea Katika kipindi hiki ambacho sisi CHADEMA na watanzania wote tukiwa kwenye Taharuki na huzuni kubwa iliyosababishwa na jaribio la kutaka kumuua Mhe. Tundu Lissu Akiwa Dodoma wiki iliyopita.
Tunalaani kwa nguvu zote uhalifu huo na tunaungana na Familia ya Meja Jenerali Mritaba na watanzania wote kumuombea aweze kupona na kurejea Katika majukumu yake ya kujenga taifa.
Aidha tunavitaka vyombo vya dola kuchunguza na Kuwatia hatiani wale wote waliohusika na uvamizi huo ili kuhakikisha kuwa usalama wa raia na Mali zao hauko shakani.
Imetolewa leo Jumatano Septemba 13, 2017 na;
John Mrema -Mkurugenzi wa Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje.
Zitto Kabwe kuhusu kushambuliwa kwa risasi Tundu Lissu