Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 19, 2017 imemtaka mshtakiwa Yusuf Ally maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli’ na wenzake watano katika kesi ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Tsh. Milioni 785.6 kuacha kuwalalamikia Mawakili wa Serikali, badala yake iwalalamikie Mawakili wao ili kesi hiyo iharakishwe.
Hayo yameelezwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Elia Athanas kudai kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo washtakiwa walilalamika kwamba kesi hiyo inachelewa.
Hakimu Simba aliwataka washtakiwa hao kuacha kuwalalamikia Mawakili wa Serikali, bali wawasumbue Mawakili wao huhu alimtaka pia Wakili wa Serikali, Athanas afuatilie kesi ili wakati ujao wajue imefikia wapi.
Baada ya kueleza hayo kesi imeahirishwa hadi October 2, 2017.
Mbali ya Yusuf Alli, washtakiwa wengine ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa ambao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Tsh. Milioni 785.6.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya January, 2014 na October 2015, wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Tsh Milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
GOOD NEWS! Kutoka Wizara ya Afya, vifaa vya Hospital kutengenezwa nchini