Ijumaa, September 29, 2017 Upande wa utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufuta kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi na mwenzake kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza amri ya kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa.
Katika kesi hiyo, mbali na Sethi mshtakiwa mwingine ni James Burchard Rugemarila ambao wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi ikiwemo kutakatisha fedha
na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kutokana na hatua hiyo, Mahakama imeamuru mshtakiwa Sethi akatibiwe katika Hospitali ya Muhimbili ndani ya siku 14 na endapo itashindikana Mkuu wa Gereza la Segerea ambalo Sethi yupo, ataitwa mbele ya Mahakamani kuhojiwa kwa kushindwa kutekeleza amri hiyo.
Hatua hiyo inatokana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kumueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Baada ya kutolewa maelezo hayo, Wakili wa Sethi, Joseph Makandege aliiambia Mahakama kuwa kumekuwepo na mfululizo wa amri za Mahakama zikiagiza mteja wake apatiwe matibabu na uchunguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
>>>”Hadi leo asubuhi tumebaini hajapelekwa katika Muhimbili kama amri za Mahakama zilivyoagiza. Hivyo, ni rai yetu kwamba kitendo hicho cha kutokuteleza amri za Mahakama ni ukaidi.”
Kutokana na hatua hiyo, Wakili Makandege alidai kuwa kwa vile upande wa mashtaka umekaidi amri za Mahakama, wanaomba Mahakama itoe adhabu inayostahili.
>>>”Hivyo naiomba Mahakama iitupilie mbali hati ya mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa, ili mshtakiwa wa kwanza Sethi aweze kupata wataalam wa matibabu yake katika Hospitali ikiwamo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.”
Aidha, Makandege amedai kuwa mashtaka yaliyopo ni ya hila, ambayo lengo lake ni kuupa upande wa mashtaka fursa ya kuwaadhibu washtakiwa hasa mshtakiwa wa kwanza Sethi kabla hawajahukumiwa.
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa TAKUKURU, Leonard Swai alidai kuwa tatizo limejitokeza katika utekelezaji wa amri za Mahakama akisema kuwa Magereza wamekuwa wakiwatibu wafungwa na mahabusu hata pasipokuwa na amri ya Mahakama na kusema kilichojitokeza ni utaratibu wa kumpeleka Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
>>>”Tumejitahidi kuwasiliana na Magereza wapo katika hatua za mwisho, tunaomba muda wa ziada ili tuiwezeshe Magereza kukamilisha utaratibu wa kumpeleka Sethi Muhimbili. Hatujakataa tunaomba muda.”
Hakimu Shaidi alisema pamoja na amri za Mahakama kuwa hazijatekelezwa, kupitia Swai kukiri kuwa hazijatekelezwa na ni lazima amri za Mahakama zifuatwe.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi October 13, 2017 na kwamba hadi siku hiyo Sethi awe amekwishapata matibabu na iwapo atakuwa hajapata Mkuu wa Gereza alilopo afike Mahakamani kujieleza.
“Hatuogopi mtu, hawa wote tutawachukulia hatua” – Waziri Mpango
EXCLUSIVE! Mbunge NYALANDU aongelea kumsaidia TUNDU LISSU