Vigogo sita wa Shirika la Umeme (Tanesco) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa 202 ya uhujumu uchumi wa kuisababishia Tanesco hasara ya Sh.Bilioni 2.7.
Vigogo hao ni Mhasibu Mwandamizi, Emilian Mlowe, Bashiru Ngella, Barnabas Massaly, Assistant Office Automation, Shakila Ngela, Senior Finance Manager, Mkawa Maira na Credit control accountant, Yared Jonas.
Washtakiwa hao walisomewa makosa yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.
Katika kesi hiyo namba 70/2017 wakili Kishenyi amedai washtakiwa wanakabiliwa na makosa 202 ambapo aliyasoma makosa hayo kwa ufupi. Miongoni mwa makosa hayo inadaiwa washtakiwa walililaghai shirika la Tanesco kupitia mfumo wa kompyuta.
Inadaiwa walitenda kosa hilo January 7, 2014 na January 31, 2015 ambapo waliingia kwenye mfumo wa kompyuta wa TANSMS 33 na kujipatia Tsh.Bil.2,746,485,545.63 ambazo walionyesha zimelipwa na wakala wa Tanesco wakati wakijua ni uongo.
Pia wanadaiwa wameisababisha hasara Tanesco ya Sh.Bilioni 2.7 ambapo inadaiwa walitenda kosa hilo
July 2014 na March 31, 2017. Makosa mengine ni ya wizi ambayo inadaiwa walitenda katika tarehe tofauti katika shirika hilo.
Baada ya kusomewa makosa hayo, Hakimu Nongwa alisema washtakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka.
Pia amesema kuhusu suala la dhamana, washtakiwa waende kuomba Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’. Kesi imeahirishwa hadi November 21,2017.
Ulipitwa na hii? Ni kesi ya Rais wa Simba na Makamu wake leo