Leo Kiungo wa ulinzi kutoka timu ya Yanga Athuman Idd Athuman maarufu kama ‘Chuji amerejeshwa kundini kuungana na wachezaji wenzake baada ya kuwa amesimamishwa na uongozi kutona na kitendo cha utovu wa nidhamu aliouonyesha mwishoni mwa mwaka jana.
Chuji alisimamishwa na uongozi na Yanga baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kuamua kuondoka vyumbani kuelekea nyumbani kabla ya mchezo kumalizika kitu ambacho alikiri ni makosa mbele ya uongozi.
Uongozi wa Yanga ulifikia hatua ya kumpa barua ya kumsimamisha Chuji ambaye alikiri kufanya kosa hilo na kisha kuandika barua ya kuomba msamaha na kuahidi kutorudia tena kitendo hicho au kufanya kitendo kingine chochote cha utovu wa nidhamu.
Baada ya kuandika barua kwa uongozi kuomba msamaha, Chuji alipewa onyo kali na uongozi na kupewa kipindi cha matazamio ambapo kwa kipindi cha mwezi mmoja ameonekana kubadilika na kurejea katika nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.
Chuji ataungana na kikosi cha Young Africans kesho tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu pamoja na mashindinao ya Klabu Bingwa Afrika ambayo yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki ijayo kwa Yanga kuanza na timu ya Komoronize ya Visiwa vya Comoro.