Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga Haruna Niyonzima aka Fabregas amesema baada ya kuwanyoosha timu ngumu ya Mbeya City na kuvunja rekodi yao ya kutokufungwa katika ligi kuu ya Vodacom, sasa kifuatacho ni kulamba ‘Ice Cream’ za Bakheresa kwa kuvunja rekodi ya klabu ya Azam ya kutofungwa kwenye ligi.
Azam FC ambayo mpaka sasa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo katika ligi kuu ya Vodacom, inashika usukani mwa ligi ikiwa na pointi 36.
Mbeya City na Azam ndizo timu pekee zilizokuwa hazijapoteza mechi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Lakini timu hiyo ya Mbeya iliharibiwa rekodi yake Jumapili baada ya kuchapwa na Yanga bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti Mwanaspoti, Niyonzima alisema anaamini watafanikiwa kuifunga na Azam kutokana na morali na malengo waliyojiwekea wachezaji katika kuhakikisha wanautetea ubingwa wao.
“Tumeanza na Mbeya City kwanza ambao wenyewe hawajafungwa tangu kuanza kwa Ligi Kuu, sasa bado Azam FC nao hawajafungwa katika msimu huu,” alisema.
“Siyo Azam FC tunaotakiwa kuwafunga peke yake, tumepanga kutoa vipigo kwa kila timu tutakayocheza nayo mechi zijazo.”
Yanga itacheza na Komorozine ya Comoro jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.