Asilimia 45 ya wanaume wanajijua kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU na asilimia 55 hawajijui huku wanawake waliokuwa wanajijua kuwa wanamaambukizi ni asilimia 56 na 44 bado hawako tayari.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuzindua rasmi kampeni ya kitaifa ya upimaji virusi vya Ukimwi VVU iliyopewa jina la ‘Furaha Yangu’ yenye lengo la kuhamasisha huduma za kupima VVU na kuanza ARV mapema hasa kwa wanaume.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dr. Angela Ramadhan wakati akizungumzia Kampeni ya kuhamasisha mkakati wa serikali wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema kwa wale watakaokutwa na maambukizi.
“Asilimia 45 ya wanaume wanajijua kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU na asilimia 55 hawajijui huku wanawake waliokuwa wanajijua kuwa wanamaambukizi ni asilimia 56 na 44 bado hawako tayari” amesema Dr. Angela
“Katika dira ya kuwa na taifa bila Ukimwi, Tanzania imeridhia malengo ya UNAIDS ya 90-90-90 ambapo asilimia 90 ya watu wote wanaoishi na VVU kutambua hali zao za VVU, asilimia 90 ya wenye maambukizi kuanza dawa na asilimia 90 ya walioanza dawa kupunguza kiwango cha VVU mwilini,” Dr. Angela.
Dr. Angela amesema kuwa Kuanza ARV mapema kutapunguza wingi wa VVU mwilini na kuimarisha kinga kwa wagonjwa,hivyo kampeni hii kwa wanaume itakuwa chachu ya kujua afya zao na wengi kuwa tayari kwa kuimarisha afya na kupunguza hatari ya kuambukiza wenza wao.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI TACAIDS, Dr. Leornad Maboko, alisema uzinduzi wa kampeni hiyo utakuwa na siku tano za kutoa huduma za afya bila malipo, ikiwemo upimaji wa VVU na magonjwa sugu.