Leo June 14, 2018 Maafisa wa mahakama wamemuarifu shemeji wa Mfalme Felipe VI wa Uhispania kwamba anapaswa kuanza kifungo chake cha miaka mitano na miezi 10 jela, katika kipindi cha siku tano sijazo, baada ya kupatikana na hatia ya makosa kadhaa ya uhalifu likiwemo la udanganyifu na kukiuka ulipaji kodi.
Televisheni ya Umma TVE ilionyesha picha za Inaki Urdangarin akiwasili kwa gari katika mahakama ya Palma de Mallorca leo baada ya kutua kwa ndege kutoka Geneva, anakoishi na mkewe Binti wa Ufalme Cristina.
Mahakama ilimkuta na hatia mwaka jana ya ubadhirifu wa euro milioni 7, na kutumia nafasi yake kama shemeji wa Mfalme, ili kujipatia kandarasi za serikali kuhusiana na masuala ya michezo.
Mkewe Cristina naye ametozwa faini kwa kosa la kujinufaisha kutokana na uhalifu wa mumewe.