Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa ya vifo vya watu 14 waliopoteza maisha baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la kubebea mchanga katika eneo la Dundani Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Ajali hii imetokea leo June 25, 2018 saa 10:40 Alfajiri wakati basi dogo lililowabeba wanafamilia, ndugu na jamaa waliokuwa wakielekea Msata kuhudhuria sherehe za kumaliza mafunzo ya kijeshi kwa mtoto wao, kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa linatoka DSM kwenda Dundani kuchukua mchanga.
“Naomba unifikishie pole nyingi kwa wanafamilia wote waliopatwa na msiba, waambie naungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majozi ya kuondokewa na wapendwa wao, na sote tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi” amesema Rais Magufuli katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.
Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wa 4 wa ajali hiyo wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu yao ya kila siku.