Leo July 10, 2018 Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi ya Viongozi 9 wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe amegoma kujitoa katika kesi hiyo.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mashauri amesema hawezi kujitoa katika kesi hiyo kwa sababu hoja zilizotolewa na washtakiwa akiwemo Mbowe hazina uhalisia wala mashiko.
Katika uamuzi huo, Hakimu Mashauri amesema amesikiliza hoja za washtakiwa kwamba ajitoe katika kesi hiyo ambapo ameona hoja nzito ni 5.
Miongoni mwa hoja hizo ni kwamba masharti ya dhamana ya washtakiwa kuripoti kituo cha Polisi Kati (Central) kila Ijumaa ni adhabu tosha kwa upande wao.
“Kimsingi hoja hiyo haina mashiko kwa sababu washtakiwa wana mawakili, hivyo wangeweza kukata rufaa wakati walipopewa masharti hayo,”.
Kuhusu hoja ya kesi hiyo kusikilizwa haraka haraka, amesema hatua hiyo inatokana na upelelezi kukamilika hivyo lazima ianze kusikilizwa.
Pia kuhusu kutoa muda mfupi kwa Mbowe pindi alipofiwa na Kaka yake, Hakimu Mashauri amesema hiyo sio hoja kwa sababu mahakama iliahirisha kesi yake pindi alipoumwa na hata alipofiwa napo mahakama ilifanya hivyo.
Pia hoja ya Hakimu kupendelea upande mmoja wa mashtaka, amesema kuwa hiyo ni hoja ya ajabu sana kwani amekuwa akiingilia kati hoja za Wakili wa utetezi, Peter Kibatala ili kumsahihisha pindi anapokosea.
Kuhusu kutoheshimu vibali vya bunge kwa sababu ya kuumwa kwa mbunge wa Tarime Vijijini, Esther Bulaya, Hakimu Mashauri amesema mahakama ilivipokea vibali hivyo na haikufanya chochote zaidi ya kuahirisha kesi.
Hakimu Mashauri amesema kuwa sababu nyingine ilitokewa na mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa kwamba yeye ni mtaalamu wa Philosophy hivyo akimuangalia Hakimu anaona anapendelea upande mmoja.
“Nipo katika benchi la mahakama kwa miaka 22 sijawahi kukutana na hoja za kujitoa zisizo za msingi, hivyo hoja hiyo haina mashiko, wewe ni mtaalamu Philosophy mimi mtaalamu wa sheria hivyo sijaona sababu za kujitoa katika kesi hii,”amesema.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi July 18,2018.
Mbali na Mbowe, Matiko na Msigwa washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Pia wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda na Esther Bulaya.
Inadaiwa kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo February 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.
Wanadaiwa kuwa Februari 16,mwaka huu katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washitakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.
Inadaiwa kitendo cha kugoma kulisababisha hofu iliyochangia kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.