Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Prince William Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo Prince William ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, na amemshukuru Rais Magufuli kwa kupata nafasi ya kuzungumza nae.
Prince William amezungumzia juhudi anazozifanya katika uhifadhi wa wanyamapori na amemuomba Rais Magufuli kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ujangili hasa wa Tembo.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemkaribisha Prince William kuja hapa Tanzania wakati wowote, na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza ikiwemo kushirikiana nae kuhifadhi wanyamapori.
“Naomba ufikishe salamu zangu kwa Malkia Elizabeth II, mwambie Watanzania tunaipenda Uingereza na tutaendeleza na kuuimarisha zaidi ushirikiano wetu mzuri kwa manufaa yetu sote” -Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na ujangili hasa wa Tembo ambapo kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba anatarajia Prince William ataunga mkono ili kukomesha kabisa ujangili katika hifadhi zote za wanyamapori hapa nchini.
Prince William aliyeingia hapa nchini jana atakuwepo kwa siku 4 hadi tarehe 29 Septemba, 2018.
MWANZO MWISHO: Shuhudia shangwe za Wanaukara Mv. Nyerere ilivyotolewa majini