Leo October 23, 2018 Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi (Darasa la saba) kwa mwaka 2018 ambapo inaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 4.96.
Akitangaza matokeo hayo Katibu Myendaji wa NECTA Dkt. Charles Msonde amesema kuwa ongezeko hilo ni kutoka asilimia 72.76 kwa mwaka jana hadi kufikia 77.725 kwa mwaka huu ambapo jumla ya Watahiniwa 733,103 kati ya 943,318 wamefaulu mtihani huo.
Msonde amesema kuwa kati ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo, wasichana walikuwa 383,830 idadi ambayo ni sawa na asilimia 77.12 na wavulana 350,273 (78.38)
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo ya Maarifa ya Jamii, Kiingereza, Sayansi na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.03 na 11.92 wakati somo la Kiswahili ukishuka kwa asilimia 1.44 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2017.