Mgogoro uliokuwepo baina ya Yanga dhidi ya shirikisho la soka la Uganda (FUFA) kuhusu washambuliaji wao Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza waliotakiwa kwenda kuichezea timu yao ya Taifa maarufu kama The Cranes umemalizika.
Uganda inacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Zambia kesho Jumatano mjini Lusaka, Zambia. Yanga imeiomba Fufa ibaki na wachezaji hao ili iweze kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Machi 9 mwaka huu mjini Cairo.
Yanga leo Jumanne inaingia kambini kujiandaa na mechi hiyo ambayo katika mchezo wa awali ilishinda bao 1-0, lililofungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Moses Katabaro, alisema: “Tumezungumza na kumalizana na viongozi wa Fufa, Okwi na Kiiza hawataenda.”
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Kazi yangu ilikuwa ni kuwaunganisha Yanga na Fufa, nafikiri hakuna tatizo na wameelewana.”
Awali Yanga iliomba kwa TFF na kukubaliwa kubaki na wachezaji wake walioitwa Taifa Stars kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Namibia itakayochezwa kesho Jumatano jijini Windhoek, Namibia.
Wachezaji hao ni Deo Munishi ‘Dida’, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Athuman Idd ‘Chuji’ na David Luhende.
SOURCE: MWANASPOTI