BEKI wa Simba, Joseph Owino amewatupia lawama viungo wa kati wa timu hiyo akidai kuwa wanajisahau na kuzikimbia nafasi zao huku wakiingilia majukumu ya viungo wa pembeni, lakini Donald Mosoti naye amenena.
“Kiukweli mabeki wa kati tunapata wakati mgumu, viungo wa kati wanasogea pembeni hivyo yale mashambulizi ya timu pinzani ambayo walitakiwa kuyatuliza wao inabidi sisi mabeki wa kati ndiyo tuyatulize,” alisema.
“Kwa kweli hilo ndilo linalotugharimu na kufanya tufungwe, hivyo sioni haja ya viungo wote kucheza pembeni wakati mabeki wetu wa kati ndiyo wanatakiwa kupanda kushambulia.
“Viungo wanatakiwa kuwa makini na kuziba nafasi zao inavyotakiwa, tukicheza hivyo ni lazima matokeo mazuri yatakuja na nashukuru kocha ameona tatizo hilo ndiyo maana kila mara anawakumbusha wachezaji uwanjani.”
Viungo wa kati wa Simba ambao wamekuwa wakitumika zaidi na Kocha Zdravko Logarusic ni Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdulhalim Humud na Amri Kiemba.
Juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Owino alikiongoza kikosi cha Simba alipokuwa nahodha na timu hiyo ikapata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting.
Simba imeruhusu mabao matano katika michezo yake miwili iliyopita. Mosoti amefafanua hilo na kusema kuwa safu yao ya ulinzi imetetereka kwa sasa kutokana na kubadilishwa mara kwa mara kwa mabeki wa pembeni, jambo linalowapa kazi ngumu mabeki wa kati.
Kwa siku za karibuni, Logarusic alibadilisha mabeki wa pembeni na kumtumia, Henry Joseph katika nafasi ya beki wa kushoto badala ya Issa Rashid ‘Baba ubaya’ huku beki ya kulia akimtoa Haruna Shamte na kumtumia William Lucian ‘Galas’.
Hata hivyo juzi Jumapili, Logarusic alimpanga Baba Ubaya kushoto na kulia alicheza Shamte.
“Mabeki siku zote ni lazima wazoeane ili waweze kucheza kwa usawa ila kwa sasa kumekuwa na mabadiliko kadhaa ya beki wa pembeni ambayo kwa kiasi fulani yanachangia kutetereka kwa safu yetu ya ulinzi,” alisema Mosoti ambaye ni raia wa Kenya.
SOURCE: MWANASPOTI