KLABU ya Etoile du Sahel ya Tunisia imewasilisha barua ya kurasa tatu Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ikimtaka mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi awalipe Dola 1.3 milioni za Kimarekani ambazo ni zaidi ya Sh 2 bilioni za Tanzania kama fidia.
Etoile kwenye barua hiyo ambayo Mwanaspoti ina nakala yake, imewasilishwa Fifa na klabu hiyo inataka ilipwe fedha hizo za fidia baada ya mchezaji huyo kuvunja mkataba wake na klabu hiyo kinyume na sheria za Fifa na wakaenda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa mchezaji huyo kuna watu walimrubuni.
Gharama hizo ni pamoja na fidia za uhamisho, mshahara wa Juni mwaka jana, mshahara wa kuanzia Julai mwaka jana hadi Juni 2016, posho zake za kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2016, gharama za malazi, gharama za tiketi ya ndege, gharama za usafiri wa gari, mshahara wa miezi mitano aliolipwa, pamoja na gharama za kiinua mgongo baada ya kumaliza mkataba na Etoile.
Barua hiyo ambayo Katibu Mkuu wa Etoile, Adel Ghith aliipeleka Fifa kama utetezi wao kwenye kesi dhidi ya Simba na Okwi, pia aliitoa kwa Simba ikionyesha kuwa Okwi anatakiwa kuilipa Etoile zaidi ya billioni mbili za Kitanzania.
Ghith alisema: “Ni tabia mbaya iliyofanywa na Okwi ambayo haiwezi kuvumilika na hivyo ninaomba Fifa mtupe muongozo kwani mchezaji huyo amevunja mkataba bila kufuata utaratibu na kwa njia isiyokubalika kisheria, tena tunaomba fidia ya gharama kama ifuatavyo.
“Fidia ya gharama za usajili Dola 247, 142 (sawa na Sh 393.6 milioni ),mshahara wa Mei hadi Juni 2013 ambao ni Dola 10,000 (sawa na Sh 15.9 milioni),mshahara wa Julai 2013 hadi Juni 2016 ambazo ni Dola 180,000 (Sawa na Tsh 293 milioni) na posho Dola 480,000 (sawa na Sh 764.5 milioni) kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2016.
“Gharama nyingine ni kodi ya miezi 38 ambayo ni Dola 19,000 (sawa na Sh 30.2 milioni), tiketi za ndege za Dola 12,000 (sawa na Sh 19.1 milioni), usafiri wa ndani (gari) Dola 26,600 (sawa na Sh 42.3 milioni), mshahara uliolipwa kwa miezi mitano ya awali Dola 50,000 (sawa na Sh 79.6 milioni), pamoja na kiinua mgongo ambacho angepewa baada ya kumaliza mkataba na Etoile cha Dola 300,000 (sawa na Sh 477.8 milioni),” alieleza.
Barua hiyo ya Etoile imeambatanishwa na nakala sita za muhimu ambazo ni mkataba wa Okwi na Etoile, maelezo ya Fufa (Shirikisho la Soka Uganda), nakala ya ratiba za mazoezi na michezo ya klabu, nakala iliyotafsiriwa kwa Kiingereza yenye ratiba za mazoezi na michezo ya klabu hiyo, barua ya mchezaji ya kujiunga na klabu pamoja na Leseni ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji.
Ghith alieleza kwenye barua hiyo kuwa: “Tulifurahi kuona Okwi akifanya kazi yake vizuri, alifanya hivyo mwanzoni kabla ya kubadilika lakini alikuwa akishiriki shughuli zote za timu ikiwemo hata kukichezea kikosi cha U-23 cha klabu hiyo.
“Alikuwa akilipwa mshahara wake kwa kipindi chote alipokuwa na timu na hivyo alikuwa akilipwa kwa mujibu wa taratibu za Fifa na zile za Shirikisho la Soka Tunisia,” alisema Ghith kwenye barua hiyo.
Ghith katika barua hiyo pia alisema: “Ghafla mwezi Mei Okwi alibadilika na hata kushindwa kuhudhuria na kujiunga na timu. Alianza kukosa mazoezi lakini bado tulipeleka jina lake kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho Afrika lakini baadaye aliondolewa.
“Baada ya kuwa hivyo, alipoacha kucheza kuna malipo alikuwa akilipwa kama mchezaji wetu lakini kuna mengine tulisitisha na tukamwambia kuwa hatutaweza kumlipa kutokana na sheria za Shirikisho la Soka la Tunisia kwamba mchezaji atalipwa baadhi ya malipo pale tu anaposhiriki mchezo
“Tulipokea barua ya Fufa kumualika Okwi kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Brazil 2014 dhidi ya Liberia na Angola, michezo ambayo iliandikwa kwenye barua kuwa ingeanza tarehe 8-15 Juni 2013 lakini tuligundua kuwa Mei 20, 2013 Okwi tayari alikuwa Uganda bila ruksa maalumu wala makubaliano yoyote na klabu.
“Lakini pia tuliwasiliana na shirikisho letu la Tunisia pamoja na Fufa lakini mchezaji (Okwi) hakutaka kuwasiliana na sisi ili kumaliza matatizo.
“Tarehe 12 Julai mwaka jana, tuliwasiliana na Fufa na mchezaji ili tuje kumaliza matatizo na pia kumwonyesha utaratibu pamoja na jinsi mkataba wake ulivyo lakini hakutaka kusikia lolote,” alisema Ghith kwenye barua hiyo.
Ghith alimalizia kwa kusema: “Tunadhani alishawishiwa na akaamua kuvunja mkataba kwa njia isiyo sahihi na hivyo kutokana na matukio yote hayo ndiyo maana tulichelewa kumlipa mshahara wake lakini pia tulimpa tu kumpendelea kwani hakustahili kulipwa.”
SOURCE: MWANASPOTI/MWANANCHI