Siku moja baada ya kuthibitika kwamba Jack Wilshare atakaa nje ya uwanja wa takribani wiki 8 baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki kati ya England na Denmark, klabu ya Arsenal imekiandikia chama cha soka cha England (FA) kiwalipe fidia baada ya mchezaji wao kuumia akiwa anaitumikia timu ya taifa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Wilshare amevunjika mguu baada ya kuchezewa rafu na mchezaji wa Denmark Daniel Agger, na sasa kuna uwezekano hatoichezea tena Arsenal msimu huu, huku kukiwa na hatihati ya kuzikosa fainali za kombe la dunia.
Arsenal ambao wapo katika harakati za kugombea ubingwa wa England, inasemekana wametaka kulipwa kiasi cha paundi laki sita ikiwa kama fidia ya mchezaji wao kuumia akiwa anaichezea England.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger tayari amethibitisha Wilshare hatovaa jezi ya Arsenal kwa wiki 8.