Leo January 2, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kusikiliza ushahidi wa kesi ya Utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa (TFF) Jamal Malinzi na wenzake kwa siku tatu mfululizo.
Hayo yameelezwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kesi hiyo kuitishwa leo kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi hiyo iliyofikia shahidi wa 10, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi January 16, 17 na 21, 2019 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Malinzi na wenzake waliwatakiwa kheri ya mwaka mpya, ndugu, jamaa na rafiki waliofika katika kesi yao.
Washitakiwa wengine ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wakikabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.
Miongoni mwa mashitaka hayo ni inadaiwa, June 5, 2017 maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Malinzi na Selestine walighushi nyaraka ya maazimio ya kamati tendaji ya June 5, 2017 kwa lengo la kuonesha kuwa kamati hiyo ya TFF imelenga kubadili mtia saini wa shirikisho hilo katika akaunti za benki kutoka Edgar Masoud kwenda kwa Mwanga.