Tunayo story kutokea Mahakama ya Hakiu Mkazi Kisutu ambapo Maofisa wanne wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini(TFDA) wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka moja la kusababisha hasara ya Sh.Milioni 58,390,000 kwa mamlaka hiyo.
Maofisa hao ni Raymond Wigenge, Ezekiel Mubito, Adelard Mtenga, Abdalah Juma na mshtakiwa wa kwanza Chary Ugullum ambaye hajafikishwa mahakamani.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustino Rwezile ambapo amedai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanashtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi.
Wakili Swai amedai kuwa kati ya Mei na Desemba mwaka 2016 washtakiwa hao wakiwa katika ofisi ya TFDA kwa uzembe waliisababishia hasara ya kiasi cha Sh.Milioni 58,390,000 kwa kuidhinisha posho maalumu kwa wafanyakazi ambao walishalipwa na kufanya walipwe mara mbili jambo ambalo ni kosa la kisheria.
Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa walikana shtaka hilo na upande wa Jamuhuri walidai kuwa upelelezi umekamilika na waliomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali.
Hakimu Rwezile amesema dhamana kwa washtakiwa hao ipo wazi hivyo wanatakiwa wadhamini wawili wawe na kitambulisho cha Taifa(Nida) na barua za utambulisho.Pia kati yao mmoja awasilishe fedha taslimu Sh Milioni 5.839 au hati yenye thamani ya Sh.Milioni 5.839.
Hata hivyo washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wote wamerudishwa mahabusu.Hakimu Rwezile ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 28,2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.