Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya uchochezi inayomkabili na Viongozi wengine wa Chama hicho kwa sababu anaumwa.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali Patrick Mwita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Mwita ameeleza kuwa washtakiwa wote wapo Mahakamani isipokuwa Mbowe ambaye amepewa taarifa na Magereza kwamba anaumwa.
“Tunaomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine tukisubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa,” Wakili Mwita
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi January 31, 2019 kwa ajili ya kutajwa.
Mbowe na Matiko wanasota mahabusu baada ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana yao November 23, 2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana.
Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa CHADEMA Zanzibar, Salum Mwalimu.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya February Mosi na 16, mwaka huu maeneo ya DSM.
TUKIO LA UGAIDI KENYA: RAIS MAGUFULI NA KENYATTA WAMEZUNGUMZA