Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu anamuuguza Mbunge mwenzie wa Bunda Ester Bulaya.
Mdee alishindwa kufika mahakamani hapo katika kesi inayomkabili ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli.
Hayo yameelezwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na mdhamini wa Mdee, Faris Lupomo wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Lupomo alidai kuwa aliwasiliana na Mbunge huyo na kumueleza kuwa atashindwa kufika mahakamani kwa kuwa anamuuguza Mbunge mwenzie Bulaya mjini Dodoma.
“Niliwasiliana naye jana (juzi) akanijulisha kuwa anamuuguza Mbunge mwenzie Ester Bulaya ambaye anaishi naye Dodoma nyumbani kwake na anamuuguzia hospitali ya Bunge Dodoma, “ alidai shahidi huyo.
Wakili wa Utetezi Hekima Mwasipu naye alikiri kuwa mshtakiwa huyo hayupo Mahakamani na amepewa taarifa na mdhamini huyo kuwa anamuuguza Bulaya mjini Dodoma.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba alisema kuwa sababu zilizotolewa na mdhamini huyo kuhusiana na kushindwa kufika kwa mshtakiwa kufika zinaleta ukakasi na kubainisha kuwa zina lengo la kuifanya kesi hiyo isimalizike kwa wakati.
“Mdhamini ulichokiongea kinaleta ukakasi wa kutosha, kwa sababu wapo Madaktari na Wabunge wengine wanawake ambao wanaweza kumuuguza, sasa tukiruhusu haya yaendelee tutashindwa kumaliza kesi”
“Kiukweli jambo hili linakwaza na linatia wasiwasi kama hii kesi tutaweza kumaliza kwa mwendo huu, tunakubali sababu hiyo ya kuuguza lakini kwa shingo upande, “ Alisema Hakimu Simba
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi, Februari 28, 2019 kwa ajili ya kesi hiyo kuendelea na ushahidi.
Mpaka sasa mashahidi watatu wamekwisha kutoa ushahidi katika kesi hiyo akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu wa Polisi Batseba Kasanga.
Mdee anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 3, mwaka jana maeneo ya Ofisi za CHADEMA zilizopo Mtaa wa Ufipa Wilayani Kinondoni, DSM ambapo alimtukana Rais Dk John Magufuli kwamba “anaongea hovyohovyo anatakiwa afunge break”, kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
“HAJI MANARA KAPOTOSHA, TUTAMUITA” MWANASHERIA