Wakazi wawili wa Chanika jijini Dar es Salaam, Abdallah Hamis (30) na Adam Kawambwa(35) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na Meno ya Tembo yenye thamani ya zaidi Sh.Bil.1 na utakatishaji.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwizile Wakili wa serikali Candid Nasua amedai, washtakiwa wametenda makosa hayo Februari 11, 2019 maeneo ya Chanika kwa Zoo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa siku ya tukio washtakiwa walikutwa na vipande 47 vya Meno ya Tembo vyenye thamani ya USD 465,000 ambayo ni sawa na Sh. Bilioni 1,081,375,500 mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Katika shtaka la pili inadaiwa siku na mahali hapo, washtakiwa hao walikutwa na vipande hivyo vya Meno ya Tembo huku wakijua kuwa wamepata vipande hivyo kutokana na kutenda kosa la ujangili.
Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida zinasikilizwa Mahakama Kuu au hadi kitakapotolewa kibali kutoka kwa DPP.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika ambapo kesi imeahirishwa hadi Machi 25,2019 kwa ajili ya kutajwa.
RC MBEYA KAACHANA NA V8 KANASWA NDANI YA DALADALA AKIWA NA DC, MKURUGENZI