Utaratibu na hatua za kuwasilisha malalamiko Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na Kanuni za Kumlinda Mtumiaji vimeainisha utaratibu wa kuwasilisha malalamiko.
Utaratibu huu una hatua nne ambazo ni kuwasilisha malalamiko kwa mtoa huduma, kuwasilisha malalamiko kitengo cha malalamiko TCRA, kukata rufaa kwa Kamati ya Malalamiko iwapo kitengo hakikupata suluhu na kukata rufaa kwa Tume ya Ushindani wa Haki iwapo upande wowote haujaridhika na maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Malalamiko.
Kuwasilisha Malalamiko kwa Mtoa Huduma Hii ni hatua ya kwanza na ya muhimu kwenye
mtiririko wa kuwasilisha malalamiko. Mlalamikaji anatakiwa kutoa taarifa kwa mtoa huduma wake
na kuweka kumbukumbu ya malalamiko yake kwa maandishi.
Inashauriwa kwamba iwapo baada ya siku 30 Mlalamikaji hajajibiwa au hajaridhika na majibu ya Mtoa huduma, anatakiwa kuwasilisha rufaa ya malalamiko yake TCRA.
Kuwasilisha malalamiko TCRA Mlalamikaji anapowasilisha malalamikoTCRA anatakiwa
kuambatanisha nakala ya mawasiliano ya barua au baruapepe kati yake na mtoa huduma wake pamoja na vielelezo vingine vyovyote vinavyohusu shauri husika.
Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa barua, kwa barua pepe, au kwa kufika kwenye ofisi za TCRA, makao makuu Dar Es Salaam, ofisi ya Zanzibar na kwenye ofisi za kanda ambazo ziko Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Dar Es Salaam.
Baada ya kupokea malalamiko kitengo cha kushughulikia malalamiko cha Mamlaka kitafuatilia kwa mtoa huduma na kumjulisha mlalamikaji kila hatua. Mamlaka itawakutanisha mlalamikaji na mtoa huduma kutafuta suluhu na suluhu ikishindikana mlalamikaji atajaza fomu ya malalamiko ili suala lake lisikilizwe na Kamati ya Malalamiko.