Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.
Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa leo na Balozi wa Kenya nchini, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam.
Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya Mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.
Kwa upande wake Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo msimamo wa Wakenya na Serikali yao.
Balozi Kazungu amesema Msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.
WAZIRI LUGOLA AWATUMBUA VIGOGO WATATU WA NIDA, ATANGAZA MSAKO SAA 12 LEO