Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa amewataka Watumishi katika Halmashauri ya Mbeya kuweka kando changamoto zinazowakabili na badala yake wawe wabunifu kwa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kufikia malengo ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Naibu Waziri ametoa rai hiyo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbeya ambako pia ametoa miezi miwili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo na kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Steven Katemba amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya muda alioutoa kwa vile majengo yote yanayohitajika yapo katika hatua ya umaliziaji.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Yahaya Msuya amesema katika ujenzi wa Hospitali hiyo wameanza na majengo saba ya kimkakati ambayo wanayajenga kwa kutumia mtindo wa force account huku Halmashauri ikishirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo.