Mahakama ya Rufani imetupilia mbali maombi ya marejeo ya aliyekuwa Mkuu Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Bageni alikuwa anaiomba Mahakama hiyo ibadilishe uamuzi wa hukumu yake ya kunyongwa.
Kutokana na uamuzi huo, Bageni hana namna nyingine ya kukata rufaa wala kutafuta namna kisheria kwani hakuna ngazi nyingine ya Hahakama nchini wala hatua nyingine ambayo anaweza kuichukua badala yake atasubiri utekelezwaji wa hukumu hiyo ya kunyongwa.
Maombi ya Bageni yametupwa na Jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza maombi hayo, ambapo uamuzi huo umesomwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu.
Jopo la majaji hao waliosikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo namba 63 ya mwaka 2016 ni Stella Mugasha (kiongozi), Ferdinarnd Wambali na Rehema Kerefu.
Afisa huyo wa zamani wa Polisi alihukumiwa na mahakama hiyo adhabu hiyo Septemba 11, 2016, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam.
HAKUNA NAMNA MKUU WA UPELELEZI KINONDONI LAZIMA ANYONGWE