Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mtu yoyote anayekwaza wawekezaji nchini atachukuliwa hatua kali na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kumchukulia hatua Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara, Maisha Selemani Mtipa baada ya kumtoza mwekezaji sh. milioni 31.6.
Ametoa agizo hilo wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho ya Biashara mkoa wa Mtwara lililofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu Mtwara, baada ya kubaini kuwa Mkurugenzi alimtoza mwekezaji kiasi hicho kwa ajili ya gharama za vikao ili apatiwe eneo.
“Yoyote anayekwaza uwekezaji nchini kwa kuwasumbua wawekezaji tutamshughulikia kabla ya yeye kuwasumbua wawekezaji” Waziri Mkuu
Amesema Mtipa alimwandikia barua mwekezaji wa kampuni ya MBR Internation Company Limited akimtaka alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili ya kulipa kamati mbalimbali zikiwemo sh. milioni 1.95 kwa kamati ya Menejimenti ya Halmashauri.
Waziri Mkuu ameendelea kusema, “fedha nyingine sh. milioni 2.27 kwa kamati ya kugawa ardhi ya wilaya, sh. milioni 4.43 kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango sh. milioni 5.14 na sh milioni 17.79 Baraza la madiwani ili wagawane tu, huu ni utaratibu wa wapi?, huku ni kufukuza na kukwaza wawekezaji”.