Ligi kuu ya Vodacom iliendelea wikiendi hii kwa michezo kadhaa kupigwa katika viwanja tofauti nchini.
Mabingwa watetezi Yanga walikuwa katika dimba la Mkwakwani kukipiga na Mgambo, matokeo ya mchezo Yanga walipoteza mchezo wa jana kwa kipigo cha magoli 2-1, kipigo ambacho kimewashitua mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakidai kwamba kuna mkono wa mtu.
Mashabiki hao ambao wengi wao walitoka Dar es Salaam, walichanganyikiwa zaidi baada kusikia Azam FC imeipiga Simba mabao 2-1 jijini Dar es Salaam na kuwaacha kwa pengo la pointi saba kileleni katika mbio za kuelekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Azam sasa imefikisha pointi pointi 53 ambazo zimewaweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza tangu iasisiwe Juni 24, 2007.
Yanga imebaki kwenye nafasi ya pili na pointi 46 huku Mbeya City ikifikisha pointi 45 na kuzidi kujikita nafasi ya tatu baada ya kuilaza Prisons bao 1-0 pia jana Jumapili na kufufua matumaini ya kuwania nafasi ya pili.
Pointi 53 zinaweza kufikiwa na Yanga au Mbeya City pekee. Matokeo ya Azam na Simba, yanawafanya Wekundu wa Msimbazi kubaki nafasi ya nne na pointi zao 36 baada ya mechi 23.
Mbeya City nao waliwashikisha adabu ndugu zao Prisons kwa kuwafunga 1-0 katika dimba la Sokoine Mbeya.
Coastal Union walifungwa 3-1 na Mtibwa Sugar. Kagera Sugar wakatoka sare na Ruvu Shooting.