Wakazi wa kijiji cha Kanyala, Kata ya Bulyaheke katika halmashauri ya Buchosa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wamesema kukamilika kwa ukarabati wa gati la kushushia na kupandishia mizigo na abiria katika bandari ya Lushamba kutaongeza kasi ya biashara katika visiwa vinavyozunguka bandari hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika bandari hiyo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Benjamini Nhungwizi alisema awali biashara ilikuwa inasuasua katika eneo hilo kutokana na kukosekana kwa miundombinu hiyo.
Alisema kabla ya kujengwa kwa gati hilo, watu walikuwa wakilazimika kuwekewa ngazi ya kupita au kubebwa na vijana waliokuwa wamejiajiri kwa ajili ya kazi hiyo ya kupandisba watu kwenye boti kwa ajili ya kusafiri kwenda visiwani.