Kampuni ya K-Finance ambayo hutoa huduma za kifedha na mafunzo ya kibiashara kwa wajasiriamali na kwa watu binafsi, imetoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini kujengea utamaduni wa kukopa na kupata ushauri wa kibiashara kwa ajili ya kukuza mitaji yao, Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Judith Minzi wakati ya Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
K-Finance ilianzishwa kwa lengo maalumu la kuwasaidia wafanyabiashara wadogowadogo ili kufanikisha matarajio yao kwa ukuaji wa biashara zao na hivyo basi, kukuza na kuchangia uchumi wa nchi. Ukuaji wa biashara sio tu kwa manufaa au kwa faida ya wajasiriamali wenye biashara hizo lakini pia kuna manufaa kwa uchumi kwa ujumla’ Minzi alisema.
Aliongeza kuwa huduma zitolewazo ni pamoja na mkopo wa muda mfupi kwa kiasi cha fedha kinachoanzia na shilingi milioni 1 hadi millioni 50 kwa ajili ya mahitaji binafsi na ya wajasiriamali wenye biashara zinazoendeshwa na zilizosajiliwa kwa taratibu za kisheria ambazo zinahitaji mkopo ili kuendeleza bishara hizo.
Ikiwemo kulipia sehemu za uwekezaji mfano ardhi, fedha kwa ajili ya tenda, pamoja na fedha za kufanyia oda mbalimbali bila kusahau mikopo ya watumishi walioajiriwa katika sekta binafsi kuwapatia fedha za kujikimu, kulipia ada ya shule na kulipa bili mbalimbali. Mikopo inatolewa ndani ya masaa 48 baada ya makubaliano kukamilika na malipo ya mkopo ni kwa muda wa mwezi mmoja(1) mpaka miezi kumi na mbili(12).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi wa K-FINANCE Devotha Minzi alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo kumeleta matokeo chanya kwa jamii kwa kutoa huduma za kifedha kwa watu wenye kipato cha chini na cha kati kwa kuwapa mikopo inayowafaa kutokana na mahitaji yao na kuwasaidia kukua kiuchumi na kuwakomboa pindi wanapokuwa na hali ngumu.
K-Finance, imekuwa moja kati ya kampuni kubwa zinazotoa mikopo midogomidogo jijini, na inazidi kuwa kwa kasi mwaka hadi mwaka, alisema mwenyekiti huyo wa bodi huku akiongeza kuwa kampuni hiyo inatarajiwa kuandaa semina kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kibiashara Januari 18 mwakani pale Hekima Garden kwa lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali katika kukuza biashara zao na kusihi wote kuhudhuria tukio hilo la kipekee