Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefanya usajili wa laini yake ya simu kwa kutumia alama za vidole na kuwasisitiza Watanzania wote wahakikishe laini zao za simu zinasajili kwa alamu za vidole kama ilivyoelekezwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Rais Magufuli amefanya usajili huo Chato Mjini katika Mkoa wa Geita.
Hata hivyo, Rais Magufuli ameongeza siku 20 kuanzia tarehe 01 Januari, 2020 hadi tarehe 20 Januari, 2020 kwa wote ambao watashindwa kusajili laini zao katika kipindi cha kuishia tarehe 31 Desemba, 2019 kama ilivyotangazwa na TCRA kutokana sababu mbalimbali zikiwemo kuugua na kukamilisha upataji wa namba ama Vitambulisho vya Taifa.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa baada ya muda huo hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na ameagiza TCRA kuhakikisha laini ambazo hazijasajiliwa zinazimwa.
Amefafanua kuwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni muhimu kwa usalama wa nchi ikiwemo kuepusha vitendo vya utapeli na ujambazi vinavyofanywa na wahalifu, ambao licha ya wengi wao kukamatwa na vyombo vya dola wameendelea kusababisha usumbufu na upotevu mali za wananchi hususani fedha.
Pamoja na kuwasalimu wananchi wa Chato Mjini waliojitokeza kushuhudia wakati akisajili laini yake kwa alama za vidole, Rais Magufuli amewasalimu na kusikiliza maoni yao kuhusu zoezi hili na pia mwananchi Steven Joseph Wandwi anayefanya biashara ya kuuza chipsi na mishikaki akawaongoza wenzake kumuombea Mhe. Rais Magufuli na kumshukuru kwa utumishi wake mzuri ulioongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa hasa vijana ambao sasa wanachapa kazi bila bughudha.
Kabla ya kwenda kusajili laini yake ya simu, Rais Magufuli ametembelea Mtaa wa Chato Kati na ametoa pole kwa familia ya Marehemu Atanasi Masansa Mnaku aliyefariki dunia juzi tarehe 25 Desemba, 2019 na mazishi yake yamepangwa kufanyika kesho.