Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wengi zaidi kujitokeza kufuga wanyamapori kupitia bustani za wanyama (Zoo), ili kuongeza idadi ya wanyama hao na hivyo kupanua fursa za utalii na ajira.
Rais Magufuli amewapongeza baadhi ya Watanzania walioanzisha Zoo hizo wakiwemo Lut. Jen Mstaafu Samwel Ndomba (Lugari Mini Zoo – Mbinga), Dar es Salaam Zoo, Bahari Zoo na wengine ambao wamefuga wanyamapori katika bustani na mashamba yao.
Amefafanua kuwa ufugaji wa wanyamapori unaruhusiswa kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kwamba Watanzania wanayo haki ya kuwapata wanyamapori hao kwa mujibu wa sheria na taratibu, kuwafuga mahali popote panapofaa na patakapowezesha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea.
“Kuna nchi nyingi ambazo wenzetu wananufaika sana kwa ufugaji huu wa wanyamapori ikiwemo Afrika Kusini, wanapata watalii wengi, watu wao wanapata ajira na wanaowekeza kwenye ufugaji huu wanapata fedha, sioni sababu kwa nini sisi Watanzania tusifuge wanyamapori wakati sheria zinaruhusu kufanya hivyo” JPM
Changamkieni fursa hii ndugu zangu, wataalamu wa wanyamapori wafundisheni wananchi kufuga wanyamapori na wahamasisheni kufanya hivyo, viongozi wastaafu jitokezeni kuonesha mfano kama alivyofanya Lut. Jen. Mstaafu Ndomba kule Mbinga, maeneo ya kufuga yapo mengi” Rais Magufuli
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kupanua na kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii ambapo katika miaka 4 iliyopita Hifadhi za Taifa zimeongezwa kutoka 16 hadi 22 na nyingine zikiwa mbioni kuanzishwa, kutokana na kutambua kuwa utalii ni sekta inayochangia vizuri katika pato la Taifa na inayotoa ajira kwa Watanzania wengi.
Kwa sasa Tanzania ina Zoo 23, Mashamba ya wanyama 20 na ranchi 6.