Viongozi wa Iran na makundi ya wapiganaji wanaowaunga mkono wameapa kulipiza kisasi baada ya mauaji ya Kamanda wa ngazi ya juu wa Iran Qasem Soleimani na Kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Hashd al-Shaabi nchini Iraq Abu Mahdi al-Mohandes katika shambulizi la Marekani mjini Baghdad.
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ametishia kulipiza kisasi dhidi ya Marekani. Rais Hassan Rouhani amesema nchi yake italipiza kisasi kifo hicho kauli iliyoungwa mkono na maelfu ya watu waliofanya maandamano ya kuipinga Marekani kote nchini humo.
Meja Jenerali Abdoulrahim Mousavi wa ni Kamanda wa Jeshi la Iran. Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul Mahdi amesema shambulizi hilo ni kitendo cha uchokozi dhidi ya Iraq na ukiukaji wa uhuru wake na litasababisha vita nchini Iraq, Kanda hiyo na ulimwengu kwa jumla.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Marekani inahitaji pongezi zote kwa kuchukua hatua hiyo. Umoja wa Ulaya, China na mataifa mengine yenye nguvu duniani yameomba utulivu na kuzitaka pande zote kujizuia.